30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Bashiru Ally atoa onyo kali

  • Asema wanaodai CCM kuna mpasuko ni wapuuzi
  • Apiga marufuku wanaotaka uongozi kugawa kofia, madera

Mwandishi wetu-DODOMA

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Bashiru Ally, ameonya watu wanaosema chama hicho kimepasuka.

Ameonya pia wanachama wa chama hicho kujiepusha na malumbano ya suala hilo.

Dk. Bashiru alitoa kauli hiyo jana ikiwa ni siku chache tangu makatibu wakuu wastaafu wa chama hicho, Abdulrahman  Kinana na Yusuf Makamba, kutoa  waraka wakilalamikia kuchafuliwa na mtu anayejiita mwanaharakati na mtetezi wa Serikali.

Baada ya kutoka kwa waraka huo, siku chache zilianza kusambazwa kwenye mitandao ya kijamii sauti za mawasiliano ya simu za wanaodaiwa kuwa ni makada wa chama hicho wakisema ndani ya chama hicho kuna mpasuko mkubwa.

Akizungumza Dodoma jana, Dk. Bashiru alisema; “wakati mwingine mimi ni mwalimu wa Kiswahili, ukichambua misamiati inayotumiwa kutangazia dunia kwamba CCM kuna mpasuko, na huu mpasuko si wa kawaida ni wa mwaka, kwamba CCM imetumbuka na kutumbuliwa na kila aina ya kejeli, kwakweli Kiswahili chepesi wapuuzeni hao wapumbavu (wanaosema kuna mpasuko).

“Na ole wake mwana CCM abainike anafanya malumbano ya rejareja, tutachukua hatua, manake kuna wakati mwingine hapa watu wengine watataka kutumia upuuzi unaoendelea kujifanya wao ndio makada kuliko wengine kutafuta kiki za kisiasa.

“Wale wanaleta ‘clip’ wanauza kwangu utafukuzwa, kwa sababu tunazo taratibu zetu, tuna kanuni zetu, tuna katiba yetu, tuna mila na desturi na utamaduni wetu na miiko yetu.

“Ole wake mwana CCM atakayetaka kutumia fursa ya upumbavu wa wapumbavu wa mwaka kutafuta kiki ya kisiasa ili achaguliwe kwenye Serikali za Mitaa.”

Dk. Bashiru aliendelea kusema; “hatuogopi kukosolewa sisi, lakini hatuko tayari kudharauliwa, kutukanwa na kubezwa, na kuitwa majina ya kejeli kwa watu ambao hawana shukrani, hatujafunzwa hivyo, hatujazoea hivyo.

“Ninachowaomba wana CCM jifunzeni kutoka kwa kiongozi wetu, ambaye wakati wote hana muda wa malumbano, wakati wote amevumilia wanaomtusi, wengine wana umri wa watoto wake, amewavumilia na yupo tayari kuwasamehe pia, lakini kwa kufanya hivyo si kwamba ni mwoga.

“Kazi ya kujenga chama chetu ni ya kufa na kupona kwa wana CCM, kazi ya kutetea na kutangaza mafanikio ya utekelezaji wa ilani ya CCM ni kazi ya kufa na kupona kwa kila mwana CCM.

“Kazi ya kujenga umoja na mshikamano miongoni mwetu na baina yetu na Watanzania wenzetu ni kazi ya kufa ama kupona kwa mwana CCM.”

Alisema uongozi wa CCM ni imara, hivyo kuwataka Watanzania kuwapuuza wale wanaowasema vibaya.

“Uongozi mzima wa chama chetu ni imara kimuundo, kimfumo, kiitikadi, kiuongozi na kifalsafa, wapuuzeni hao wapumbavu, hatupo tayari kudharauliwa na kubezwa na kuitwa majina ya kejeli kwa watu ambao hawana staha, hawajafundwa, hatujazoea hivyo,” alisema.

Alisema pia CCM ni chama cha siasa kilichojikita katika ukombozi, tofauti na vyama vingine ambavyo vimejikita katika siasa za kipuuzi.

“Hiki chama ni chama cha kisiasa, lakini tofauti na vyama vyote Afrika, hiki ni chama cha siasa cha kikombozi, sio cha siasa za kipuuzi.

 “Majira haya ni ya uchaguzi, na mimi mtu anayenichokoza ajue anamchokoza namba moja, ni Mkurugenzi wa Uchaguzi wa CCM ambaye ni mimi, sichokozeki na chini yangu kuna wakurugenzi ambao wananisaidia ngazi ya mkoa, na katibu wa chama mkoa ukichokozeka mara ya kwanza ya pili na tatu nakutumbua.

“Kwa sababu mmepewa dhamana kubwa, shughuli za kila siku chini yake kuna wakurugenzi kila wilaya, Kondoa, Chemba kote huko wapo msichokozeke.

“Acheni wao wenyewe wabwabwaje kitoto toto watachoka wenyewe, ukitaka kujua huu ni mchezo wa kitoto wapinzani wameanza kuuchangamkia, hii CCM ni ya ngazi ya viwango vya juu na ni kiwango cha kimataifa.

“Ukiona wapinzani wamechangamkia porojo na upuuzi ndani ya CCM, ujue hao walioanzisha upuuzi huo hawakitakii mema chama chetu, hawakijui vizuri chama chetu, mchezo wa kitoto waachiwe vyama vya upinzani maana viwango vyao ndio vya kucheza,” alisema.

RUKSA KWENDA UPINZANI

Alisema wale watakaoshindwa kuendana na kasi ya CCM ruhusa kwenda upinzani.

“Mimi msanii, pia watu watapata shida hata kuelewa nilichosema, tunajadili masuala mazito ya kitaifa, chama ni kikubwa, wapo watakaoshindwa mchezo wa kisasa, lazima wakacheze cha ndimu.

“Tuwavumilie, tutawatafutia  kocha mzuri kama Jamila (Katibu wa CCM Dodoma) awachezeshe chezeshe halafu  atakuwa mmoja mmoja akiwapandisha daraja, wakiona kasi imezidi waende vyama vya upinzani, ruksa,” alisema.

MARUFUKU KUGAWA MADERA, TISHENI

Dk. Bashiru alisema wakati wakielekea katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu, ni marufuku kutoa msaada wa aina yoyote.

Alisema msaada huo unatakiwa kupelekwa katika kamati za siasa za wilaya ambao wao ndio wataamua.

“Tuje kwenye msimu wa uchaguzi, wapo watu wanataka kupita na vifedha vyao, wavilete kwenye kamati ya siasa za wilaya wazisajili.

Alisema wale ambao watafanya mambo hayo wanatakiwa wafukuzwe mara moja.

 “Ukiona mtu anapitapita anajenga mradi, anaendesha kampeni, ana kikundi cha sanaa, ana ligi ya mpira, anagawa pikipiki, baiskeli, anagawa vitenge, anagawa madera fukuza.

“Tumeweka utaratbu mzuri sana, kama una kitu sajili kwenye kamati yako ya siasa,” alisema.

WANAOLALAMIKA MAISHA MAGUMU

Alisema wote wanaolalamika maisha yamekuwa magumu wengi walikuwa ni wezi.

Alisema Watanzania wameibiwa vya kutosha na sasa Serikali ya awamu ya tano imejipambanua kumsaidia Mtanzania.

“Vyuma vimekaza kweli kweli, kabla ya mfumo huu wa kubana wezi hali ya chama ilikuwa mbaya, lakini sasa hivi ipo vizuri. Wakati huo mishahara ilikuwa inalipwa tarehe 40, leo akaunti inasoma bilioni 22,” alisema.

MIZENGO PINDA

Kwa upande wake, Waziri Mkuu mstaafu Pinda, alisema amefanya kazi na marais wote waliopita, hivyo Mwenyekiti wa CCM, Rais Magufuli anatakiwa aachwe achape kazi kwani kibaya chajiuza na kibaya chajitembeza.

“Siku zote tunaambiwa chema chajiuza na kibaya kinajitembeza, sasa huyu bwana huyu mpende msimpende ni chema kinachojiuza,” alisema.

Aidha aliwataka viongozi wa CCM kuwa na mshikamano ili chama kiweze kusonga mbele.

Aliwataka wana CCM kujitokeza kwa wingi kujiandikisha kwenye dadtari la wapigakura na kujitokeza siku ya uchaguzi.

KATIBU WA CCM MKOA

Katibu wa CCM Mkoa wa Dodoma, Jamila Yusufu, alisema mradi huo wa vibanda hadi kukamilika ulitakiwa kutumia zaidi ya Sh milioni 253, lakini wao wameukamilisha kwa kutumia Sh milioni 133.

Alisema kwa sasa mradi huo umekamilika kwa asilimia 90 na utasaidia kuongeza mapato ya chama kwa mwaka.

“Tulikuwa tunakusanya Sh milioni 599 mwaka 2017 -2018, lakini mwaka 2018-2019 tumekusanya Sh milioni 914 na tutakuwa tukipata zaidi ya Sh milioni 87 kama kodi kutokana na vibanda hivyo,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles