28.1 C
Dar es Salaam
Wednesday, July 24, 2024

Contact us: [email protected]

Kamishna wa Maadili awataka watumishi kulinda siri

Na Clara Matimo, Mwanza

Kamishna wa  Maadili nchini Jaji wa Rufani Sivangilwa Mwangesi, amewataka watumishi  wa sekretarieti ya maadili ya viongozi wa umma kulinda siri za watoa taarifa kuhusu malalamiko ya ukiukwaji wa maadili ya viongozi wa umma ili  kujenga imani ya wananchi kwa serikali yao.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza, Ngusa Samike, akitoa utambulisho wa washiriki wa kikao cha pamoja na  Kamishna wa  Maadili nchini, Jaji wa Rufani Sivangilwa Mwangesi.

Aidha, Jaji Mwangesi amewataka watumishi wa umma kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu wakijiepusha na shughuli zinazosababisha mgongano wa maslahi wanapotekeleza majukumu yao kwani hiyo ndiyo changamoto kubwa inayowakabili.

Jaji Mwangesi,ametoa agizo hilo jijini hapa leo Alhamisi Juni 16, 2022  wakati akizungumza na viongozi wa Mkoa wa Mwanza ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya wiki ya utumishi wa umma ambayo huadhimishwa  Juni 16 hadi 23 kila mwaka.

“Msijinufaishe na taarifa mnazozipata kutokana na nafasi zenu  kwa kujinufaisha nyie wenyewe binafsi, ndugu, jamaa au  rafiki zenu  kwa kufanya hivyo mtakuwa mnakiuka sheria ya maadili ya viongozi wa umma namba 13 ya mwaka 1995 sura ya 398 ambayo inalenga kuenzi na kudumisha suala zima la utawala bora, kujenga na kudumisha amani na utulivu nchini.

 “Mgongano wa maslahi ndiyo changamoto kubwa inayotukumba watumishi wa umma  mfano serikali inaweza kuwa inataka kutoa ajira ambazo bado haijazitangaza lakini wewe mtumishi ukajua unaanza kuwaambia ndugu, jamaa au rafiki zako ili waanze kujiandaa  kwa kufanya hivyo unawaondolea wengine ambao hawajajua haki ya kushiriki kupata nafasi hiyo kikamilifu, au kutokana na nafasi yako labda nafasi za ajira zimetoka unamshinikiza yule anayesimamia nafasi hizo kumpa kipaumbele mwanao, ndugu au jamaa yako,” amesema Jaji Mwangesi.

Baadhi ya viongozi wa Mkoa wa Mwanza, wakiwa katika kikao cha pamoja na  Kamishna wa  Maadili nchini, Jaji wa Rufani Sivangilwa Mwangesi.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel, alisema ataendelea kutoa kipaumbele kushirikisha jamii nzima kupambana na vitendo vya ukiukwaji wa maadili, haki za binadamu, uwajibikaji, utawala bora na mapambano dhidi ya rushwa.

“Suala la kujenga, kukuza na kusimamia maadili ni jukumu la kila mmoja wetu hivyo nitoe  rai kwa jamii nzima tushirikiane sote kwa pamoja katika ngazi zote na hasa  sisi tulioshiriki kikao hiki  tuwe mabalozi wa kwanza kufikisha ujumbe vizuri kwa watumishi wenzetu ambao hawajapata  fursa ya kuhudhuria kikao hiki na kwa jamii nzima.

Kwa mujibu wa Mhandisi Gabriel, lengo la kikao hicho ni kuendelea kutambua dhamira ya kuufanya utumishi wa umma kuwa wenye ufanisi, kuheshimika, watumishi wa umma  kufuata sheria ya utumishi wa umma, kanuni pamoja na kuzingatia viwango vya juu vya maadili ili kukuza utu, uwazi, uadilifu, uwajibikaji na kuimarisha imani ya wananchi kuhusu utendaji kazi serikalini.

CAPTION

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles