Na Derick Milton, Mwanza
Baaada ya kuitumikia Taasisi ya UTPC – Union of Tanzania Press Clubs (Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania) kwa zaidi ya miaka 19 kama Mkurugenzi Mtendaji, Abubakar Karsan ametangaza rasmi kustaafu kuitumikia taasisi hiyo.
Karsan ameitumikia taasisi hiyo tangu mwaka 2003, ambapo amesema kufikia Desema, mwaka huu ataachia ngazi rasmi kuitumikia UTPC ambayo ameeleza imekuwa taasisi imara na kubwa nchini.
Akifungua mkutano wa kupitia kanuni za maadili ya vyombo vya habari mtandaoni jijini Mwanza leo Ijumaa Juni 17, Karsan ametanga uhamuzi huo mbele za waandishi wa habari na kubainisha kuwa ameamua kwa hiari yake yeye mwenyewe kustaafu.
“Toka mwaka jana niliomba mimi mwenyewe kwenye bodi ya wakurugenzi nistaafu, nikapumzike na niweze kuwaachia vijana, lakini bodi ilikataa wakaniomba niendelee mwaka mmoja hadi mwaka 2022,” amesema Karsan.
“Niliwakubalia bodi na sasa ule mwaka mmoja utamalizika Desema, Mwaka huu, nami nakwenda kupumzika ili niwaachie wengine waweze kuendeleza taasisi hii,” ameeleza Karsan.
Mkurugenzi huyo amesema kuwa UTPC tayari imefanya mchakato wa kumpata Mkurugenzi mpya, ambapo amewaomba waandishi wa habari nchini kutoa ushirikiano mkubwa kwake.
“Mchakato wa kumpata Mkurugenzi mpya wa UTPC ulinza muda mrefu na tayari amepatikana, hivyo niwaombe waandishi wa habari nchini kutoa ushirikiano mkubwa kwake,” amesema Karsan.
Amesema tangu kuanzishwa kwa UTPC wamepitia changamoto nyingi ambazo zimefanya taasisi hiyo kusimama na kuwa imara zaidi.