Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
UNAWEZA kusema kwamba Mr Eazi, msanii wa muziki kutoka nchini Nigeria aliyepata umaarufu mkubwa kupitia wimbo wake wa Leg Over, amepiga ndege wawili kwa jiwe moja baada ya kuachia ngoma mpya ya ‘Legalize’ ambayo wakati wakishoot video yake, amemvalisha pete ya uchumba mpenzi wake wa muda mrefu, Temi Otedola.
Mr Eazi na Temi Otedola ambaye ni mtoto wa bilionea mkubwa nchini Nigeria, Femi Otedola, wamevishana pete ya uchumba wakiwa London nchini Uingereza wakiwa wanarekodi video ya wimbo wa Legalize ambao staa huyo amekiri kwamba ni maalum kwa ajili ya mpenzi wake huyo.
Baada ya kuvishana pete, wawili hao walisafiri pamoja mpaka Venice, Italia ambako kazi ya kurekodi video iliendelea, mwanadada huyo akiwa ndiye ‘video vixen’ wa wimbo huo ambao tayari umeshakuwa gumzo kwenye mitandao ya kijamii na vyombo vya habari kutokana na ubora wake.
Legalize unatajwa kuwa wimbo wa kwanza katika albamu mpya ya staa huyo ambayo bado hajaweka wazi jina lake ambapo umetayarishwa na maprodyuza wa kimataifa akiwemo Michael Brun mwenye asili ya Haiti na Marekani, E Kelly wa Nigeria na Nonso Amadi kutoka Canada.
Video ya wimbo huo, imeongozwa na dairekta kutoka Italia, Federico Mazzarisi ambapo ndani yake kuna vivutio vingi vinavyopatikana Venice ikiwemo hoteli maarufu ya Ca’ Sagredo na makumbusho mashuhuri ya The Punta Della Dogana na Palazzo Grimani.