27.7 C
Dar es Salaam
Wednesday, February 21, 2024

Contact us: [email protected]

Kamati ya Siasa Kilimanjaro yakerwa na matumizi mabaya ya fedha za mradi

Na Safina Sarwatt, Mwanga

Kamati ya Siasa ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Kilimanjaro imesema haijaridhishwa na matumizi ya fedha zilizotumika Sh milioni 400 katika ujenzi mradi majengo matatu ya upasuaji, maabara na jengo la Mama na Mtoto hospitali ya wilaya Mwanga Usangi na kuiagiza halmashauri hiyo kupeleka BOQ.

Kauli hiyo imetolewa Februali 4, 2021 na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Patrick Boisafi katika ziara ukaguzi wa utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ambapo amesema kuwa fedha zilizotumika haziendeni na mradi huo.

Boisafi amesema kuwa fedha zilizotumika ni nyingi kuliko uhalisia wa mradi na kuiagiza halmashauri ya mwanga kuleta BOQ ya mradi huo.

“Maeneo mengine wametumia Sh million 400 majengo manne lakini hapa majengo matatu Sh milion 400 mkurugenzi wa wilaya fuatilieni leteni BOQ ya huu mradi, manunuzi yamefanyikaje binafsi sijakubaliana na fedha zilizoyumika hapa,”amesema Boisafi.

Amesema Serikali inatenga fedha nyingi ili kuboresha utoaji wa huduma za afya katika hospitali za wilaya, vituo vya afya, zahanati na hospitali za rufaa hapa nchini na kwamba CCM haiko tayari kuona miradi inatekelezwa chini ya viwango.

“Mkuu wa wilaya na Mkurugenzi ujenzi umekamilika ila tunataka mtuandalie BOQ za gharama za ujenzi wa majengo matatu yaliyotumia Sh milioni 400 za serikali katika hospitali hii ya Mwanga, Usangi,” amesema.

Amesema viongozi hao pia hawana budi kuhakikisha vituo vya afya na hospitali zote zinapata madawa ya kutosha na kutoa huduma kwa wananchi ili kusiwepo mgonjwa anayefariki dunia kwa kukosa dawa.

Ameongeza kuwa serikali imeongeza mara dufu bajeti ya manunuzi ya dawa na vifaa tiba kukarabati na kujenga vituo vya afya, zahanati,hospitali za wilaya,rufaa na kanda ili kuwawezesha wananchi kupata huduma bora za afya na hakuna mtu atayekufa kwa kukosa dawa.

Ametoa wito kwa wananchi kutunza miradi ya maendeleo ikiwemo afya na elimu na hakuna mwananchi ama mfanyakazi wa serikali atakayehujumu miradi hiyoinayojengwa kwa gharama kubwa na nguvu za wananchi.

Amesema viongozi wasijaribu kuihujumu miradi ya serikali inayoletwa na serikali kwa kuiba dawa na vifaa tiba.

Mkuu wa wilaya ya Mwanga, Thomas Apson, amesema wameshachukua hatua ya kukabiliana na wafanyakazi na wakuu wa idara wasiokuwa waaminifu katika idara ya manunuzi ya vifaa vya umma ambapo taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa (takukuru) imeburuza baadhi ya watumishi mahakama kwa tuhuma ujenzi wa miradi chini ya kiwango.

Mganga Mfawidhi wa wilaya ya Mwanga, Dk. Abdul Msuya, amesema ujenzi wa majengo hayo upo tayari na kwamba yataanza kutumika kabla ya mwezi Februari 20, mwaka huu na wananchi wakiwemo akina mama kuanza kupata huduma za upasuaji na vipimo vya kisasa vya maabara.

Mganga huyo ameiomba serikali kuisaidia wilaya hiyo kupata madawa ya kutosha na vifaa tiba vya maabara na jengo la upasuaji ili fedha za serikali zisipotee bure na wananchi wakakosa huduma za maabara na upasuaji.

Amesema kiwango cha upatikanaji wa dawa kutoka MSD kimeshuka kutokana na baadhi ya vituo vya afya kuwa na malimbikizo makubwa ya madeni yaliyokaa kwa muda mrefu.

Msuya amesema hadi kifikia Desemba, mwaka jana walifanikiwa kupunguza kiasi cha Sh 253,234,578.83 na kwamba wananchi wa Mwanga wamekuwa wakipata madawa kwa kutumia mshitiri wa makusanyo ya papo kwa hapo, mfuko wa afya ya jamiii ulioboreshwa (iCHF)na mfuko wa taifa wa bima ya afya (NHIF).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
583,000SubscribersSubscribe

Latest Articles