30 C
Dar es Salaam
Monday, November 18, 2024

Contact us: [email protected]

KAMA TRUMP ANGEKUWA TANZANIA…

KATI ya mambo ninayoyapenda sana katika demokrasia ya Marekani, ni utaratibu wa nchi hiyo kuwa na wanahabari maalumu kwa ajili ya kuripoti masuala yoyote kutokea Ikulu ya Marekani.  Wanajulikana kama White House Correspondents na Ikulu ya nchi hiyo imewatengea hata maeneo ya kufanyia kazi kwenye jumba hilo.

Utaratibu huo unanifurahisha sana, kwani huwapa uwezo wanahabari hao kuripoti matukio yoyote yenye uhusiano na nchi hiyo kwa haraka zaidi, jambo linalosababisha hata wasemaji wa Ikulu kutoa majibu kwa haraka ili dunia ifahamu ukweli wa yanayoendelea.

Utaratibu huu unadhihirisha msemo kwamba vyombo vya habari ni mhimili wa nne wa dola na kwamba ili habari yoyote iwafikie watu kwa haraka na bila kupotoshwa, basi ni lazima ufanye kazi na vyombo vya habari, na kuwafanya kuwa rafiki – si adui.

Kwa wiki kadhaa sasa, Rais wa Marekani, Donald J. Trump, amekuwa gumzo kila kona kutokana na kuanzisha vita na vyombo vya habari.  Vyombo vikubwa kama CNN na gazeti la New York Times vimekuwa vikishutumiwa na Trump kwa “kupotosha” habari mbalimbali zinazohusiana na Serikali yake na namna anavyoiendesha.

Trump anaelekea kutopendezwa kabisa na vyombo hivyo, kiasi cha kuviita “Fake News” na hata kuvishambulia kila anapozungumza – kuanzia hadharani, hadi kwneye mtandao wa kijamii anaopenda zaidi kuutumia, wa Twitter.

Imefikia hatua, siku kadhaa zilizopita, White House iliwazuia wanahabari kutoka CNN, BBC, New York Times, BuzzFeed, Daily Mail, the Guardian na wengineo kuhudhuria mkutano wa kila siku wa wanahabari, katika mwendelezo wa vita hiyo kati ya Trump na vyombo vya habari.  Wakati huo huo, vile vyombo rafiki kwa Trump, kama vile Washington Times, CBS, Fox na ABC viliruhusiwa katika mkutano huo.  Japokuwa wanahabari kutoka Associated Press na Time walialikwa, waligoma kuhudhuria mkutano huo.

Kinachoendelea Marekani kati ya Trump na vyombo vya habari, kinanifanya nijiulize ingekuwaje endapo Rais huyu angekuwa wa Tanzania.  Jaribu kufikiri angechukua hatua gani dhidi ya vyombo vyote vya habari vinavyomkosoa, huku kukiwa na Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976 inayompa mamlaka ya kufungia gazeti lolote linalokwenda kinyume na matakwa yake.

Ama unadhani angechukua hatua gani chini ya Sheria ya Utangazaji ya mwaka 1993, ambayo imeshawahi kutoza faini vituo kadhaa vya utangazaji kutokana na kuripoti mambo ambayo hayatakiwi kusikika? Jaribu kufikiri hatua ambazo zingechukuliwa dhidi ya vyombo hivyo ambavyo Trump anaviita “Fake News”.

Mashambulizi ya Rais huyo wa nchi yenye nguvu kubwa zaidi duniani hayajaishia katika kuwakatalia wanahabari hao kuuliza maswali kwenye mikutano yake, au kuwazuia kupata habari kutoka White House; anayaendesha kwenye mitandao ya jamii.  Anaviita vyombo hivyo kuwa ni chama cha upinzani na adui wa watu wa Marekani.

Najaribu kufikiria dunia bila ya uwepo wa CNN au BBC, ulimwengu bila ya uwepo wa vyombo vya habari ambavyo vinaripoti yale ambayo watawala hawataki yasemwe, ulimwengu ambao Rais wa nchi yupo bize akituma mashambulizi kupitia mitandao ya jamii dhidi ya wale wasiokubaliana naye.  Rais ambaye anataka kusifiwa tu na kupongezwa kwa kila jambo, hata yale ambayo hajayafanya.

Najaribu kufikiria dunia ambayo wananchi wanalazimika kusikia habari ‘nzuri nzuri’ tu kutokana na kila linalotokea.  Dunia ambayo hakuna changamoto, hakuna kukosoana, hakuna kuumbuana, hakuna kugombana – yaani dunia ambayo ipo tu bila jipya lolote la maana.

Najaribu kufikiria dunia ambayo mtawala akikosolewa kidogo, basi hatua kali zinachukuliwa dhidi ya mkosoaji.  Kwamba hata kama uchaguzi wa Rais ulikuwa na kasoro nyingi zilizo dhahiri ambazo zinahusishwa na mataifa ya nje, hilo lisiripotiwe, kwani mtawala huyo anaona kwamba wananchi wake, walipa kodi wa nchi hiyo ambao wameshiriki kulipia gharama za uchaguzi huo, hawastahili kuujua ukweli.

Najaribu kufikiria dunia ambayo zipo sheria za magazeti na sheria za utangazaji zinazompa mtawala mamlaka ya kushughulika na vyombo vya habari, iwe kwa njia ya kuvifungia, ama kuvitoza faini. 

Kwa kifupi, najaribu kufikiria ingekuwaje kama Trump angekuwa Tanzania.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles