25.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

ASANTE MAGUFULI KWA KUIKATAA EPA LAKINI……..

HATIMAYE  Rais John Magufuli ameonyesha waziwazi kuwa hafurahishwi na mpango wa ushirikiano wa kibiashara baina ya nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya, Afrika, Karibiani na Pasifiki ambao unajulikana kwa kifupi kama EPA.

Akizungumza pamoja na Rais Yoweri Museveni wa Uganda Ikulu mwishoni mwa wiki iliyopita, Rais Magufuli aliufananisha mpango huo na aina ya ukoloni mpya. Kwa wanaoelewa ubaya wa ukoloni watakuwa wamefahamu ni kwa kiwango gani Rais Magufuli ameonyesha kutoupenda mpango huo wa EPA.

Ni vema kuwa baada ya awali kuonyesha mashaka na wasiwasi wa chini chini kuhusiana na mpango huo, hatimaye Rais Magufuli ameamua kukitoa kile kilichoujaza moyo wake kuhusiana na EPA. Awali alionyesha dalili ya kutokubaliana na mpango huo kutokana na jinsi ambavyo katika dakika za mwisho alikataa Tanzania kusaini makubaliano hayo.

Labda kutokana na kutaka kuonyesha diplomasia kidogo, Rais Magufuli, akatumia wadhifa wake kama Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki aliwaomba wanachama wenzake waendeleze majadiliano kuhusiana na mpango huo.

Ingawa kilichokubaliwa katika majadiliano hayo bado hakijawekwa hadharani, lakini kwa kauli ya Rais Magufuli majuzi, wenye akili wameshafahamu ya kuwa itakuwa ni vigumu sana Tanzania kusaini makubaliano hayo kwa jinsi yalivyo. Lakini hiyo haimaanishi kuwa Tanzania haiwezi kusaini. Tanzania inaweza kusaini iwapo yatafanyika mabadiliko makubwa katika mpango huo.

Kimsingi, watu wengi wanaupinga mpango huo, akiwamo Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa na wabunge wengi, ambao walionyesha kupinga kwao wakati mpango huo ulipopelekwa bungeni kujadiliwa.

Huu si mpango mzuri hasa kwa nchi kama Tanzania ambayo imeamua kuimarisha sera ya kujenga uchumi wa viwanda kwa sababu unalenga kuyageuza mataifa ya Afrika na Pasifiki kuwa masoko ya bidhaa za Ulaya.

Ni mpango ambao unataka kuweka aina fulani ya uwiano wa kibiashara ambapo nchi za Afrika zitapewa uhuru wa kuuza bidhaa zake katika nchi za Ulaya bila vikwazo vingi (hasa vya kikodi). Lakini kwa upande mwingine, nchi za Ulaya nazo zitapewa uhuru kama huo kuleta bidhaa zake Afrika.

Ingawa kwa kuanzia nchi za Ulaya zitakuwa zikiruhusiwa kuleta bidhaa chache tu, lakini kiwango hicho kitakuwa kikiongezeka jinsi muda unavyoenda mbele.

Tatizo hapa ni kuwa kwa mazingira ya uchumi wa Afrika, ni vigumu sana kuzalisha bidhaa ambazo zitakuwa na viwango vinavyokidhi masharti ya Soko la Ulaya kwa gharama nafuu na kwa uwingi unaohitajika. Mazingira ya uzalishaji bidhaa Afrika unazifanya bidhaa zinazozalishwa kuwa za bei juu kutokana.

Kwa upande mwingine, kutokana na kukua kwa sayansi, teknolojia na uhakika wa mitaji, Ulaya inaweza kuzalisha bidhaa bora kuliko zinazozalishwa Afrika kwa gharama za chini sana. Kwa maana hiyo, bidhaa zinazozalishwa Ulaya zitakuwa na bei ya chini sana ukilinganisha na bidhaa zinazozalishwa Afrika.

Inaweza kuwa inashangaza lakini ni kweli kuwa kuna uwezekano nchi za Ulaya zikanunua maziwa ghafi kutoka Afrika, wakayasafirisha kwao, wakayachakata na kuyafunga na kuja kuyauza Afrika kwa bei ya chini kuliko maziwa hayo hayo ambayo yatakuwa yanazalishwa,  kuchakatwa na kufungwa Afrika.

Kwa msingi huo, itakuwa ni ajabu kwa wakazi wa Ulaya kukubali kununua bidhaa (ambazo ubora wake watakuwa wanautilia mashaka) ambazo zinauzwa kwa bei ya juu wakati tayari wana bidhaa zinazouzwa kwa bei ya chini.

Matokeo yake, Afrika itashindwa kusafirisha bidhaa zake Ulaya na yenyewe kubaki kuwa mpokeaji wa bidhaa kutoka Ulaya. Hapo tayari itakuwa imegeuzwa soko.

 

Itaendele

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles