Na RENATHA KIPAKA
SERIKALI mkoani Kagera imeanza kubainisha maeneo ya malisho ya mifugo Wilaya ya Muleba kudhibiti tatizo la uvamizi holela wa misitu ambayo imetengwa kwa ajili ya hifadhi ya taifa.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Meja Jenerali mstaafu, Salum Kijuu, alisema kwa sasa yameanza kubainika maeneo ya malisho na yataendelezwa kwa lengo la kuufanya ukanda wa eneo la Mwisa kuwa la wafugaji wenye tija na endelevu wenye tija.
Alisema pamoja na kuwatengea wafugaji maeneo pia watahakikisha wanaviendeleza vijiji vinavyozunguka eneo hilo kwa kupunguza umasikini kwa wananchi wake.
Jenerali Kijuu alisisitiza kuwa wafugaji watakaopewa maeneo hayo watapaswa kufuga kisasa.
“Tunabainisha maeneo haya ili kuyatenga kwa lengo la kuondoa ufugaji holela na ukataji miti ovyo.
“Tutawawezesha wafugaji wafuge kisasa na kuuendesha ufugaji kama biashara bila ya kuharibu mazingira kwa faida ya kizazi cha sasa na kijacho,” alisema.
Aliyataja maeneo mengine kuwa ni katika Ranchi ya Kagoma kwenye bonde la Ziwa Burigi hadi katika Pori la Akiba la Burigi lenye zaidi ya ukubwa wa hekta 60,000.
RC alisema kuwa ili kuondoa migogoro katika maeneo hayo serikali itayatenga katika vitalu kwa kuweka alama kulingana na jiografia ya eneo husika kuwawezesha kupatikana malisho na makazi.