SAADA SALIM
KIPA wa Yanga, Ramadhan Kabwili, ambaye alipata majeraha kwenye mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya African Lyon, amewaambia mashabiki wa Wanajangwani hao watulize presha kwani anaendelea vizuri.
Kabwili aliumia kwenye mchezo huo uliochezwa Uwanja wa Sheikh Amri Abeid uliomalizika kwa Wanajangwani hao kuibuka na ushindi wa bao 1-0 ambapo nafasi yake ilichukuliwa na Klaus Kindoki.
Kipa huyo kwa sasa ndiye tegemeo licha ya umri wake kuwa mdogo hasa baada ya Beno Kakolanya, kutofautiana na kocha wake mkuu, Mwinyi Zahera, kutokana na kukacha mazoezi kwa madai ya kutokulipwa stahiki zake na uongozi.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Kabwili, alisema anaendelea vizuri na muda wowote atarudi kuipambania timu yake ambayo inausaka ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, kwa kila namna.
“Nashukuru wale wote walioniombea, kwa sasa hali yangu inaendelea vizuri, suala la kucheza litakuwa chini ya daktari na kocha kutokana na hali ambayo ninayo kwa sasa,” alisema. Kikosi hicho cha Yanga, kinajiandaa na mchezo wa Kombe la Shirikisho maarufu kama FA, dhidi ya Tukuyu Stars kesho Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam ambapo huenda Kabwili akaukosa kutokana na maumivu hayo