29.8 C
Dar es Salaam
Monday, October 7, 2024

Contact us: [email protected]

Simba ni kufa au kupona leo

TIMA SIKILO-DAR ES SALAAM

TIMU ya Simba inashuka dimbani leo kuivaa Nkana Red Devils ya nchini Zambia, katika mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika, utakaopigwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Katika mchezo wa kwanza uliopigwa Uwanja wa Nkana mjini Kitwe, Simba ililala mabao 2-1.

Bao la Simba lilifungwa kwa mkwaju wa penalti na John Bocco, huku yale ya Nkana yakiwekwa kimiani na Ronald Kampamba na Kelvini Kampamba.

Ili kusonga mbele, Simba inatakiwa kuhakikisha inapata ushindi wa idadi yoyote ya mabao leo, lakini wakati huo huo ikiepuka kuruhusu wavu wake kutikiswa.

Hatua hiyo inatokana na faida ya bao moja iliyonayo kwa sasa.

Katika mchezo huo, Simba itaendelea kuwategemea washambuliaji wake, Emmanuel Okwi, Meddie Kagere na John Bocco, kuipenya ngome ya Nkana na kufunga mabao.

Kwa upande mwingine, Nkana itaendelea kuwaamini wachezaji wao Kelvin na Andrew, lakini wakiwa chini ya uongozi wa nahodha wao, Walter Bwalya.

Akizungumza katikati ya wiki hii, Kocha Mkuu wa Simba, Patrick Aussems, alisema wachezaji wake wana morali ya hali ya juu ya kutaka kupindua matokeo ili kutinga hatua ya makundi.

“Tuko vizuri, mchezo wa kwanza tuliwakabili wapinzani wetu huku nikiwa siwafahamu vizuri, lakini kwa sasa nimefahamu mbinu zao na namna wanavyocheza.

“Kama wao walifanikiwa kushinda kwao hakuna jambo la kushangaza na sisi tunaweza kupata mabao mengi nyumbani, lengo ni kufuzu hatua inayofuata,” alisema Aussems.

Kwa upande wake kocha wa Nkana, Beston Chambeshi, ana imani kikosi chake kitapata ushindi ugenini na kusonga mbele hatua inayofuata.

“Tumekuja Tanzania kwa lengo moja la kupata ushindi na kufuzu hatua inayofuata, tunafahamu ugumu wa mchezo huu, lakini tupo tayari kwa mapambano,” alisema Chambeshi.

Mchezo huo utachezeshwa na mwamuzi Peter Waweru kutoka nchini Kenya akisaidiana na mwamuzi Tony Kidiya na  Anthony Ogwayo, wote kutoka nchini humo.

Simba imefika hatua hiyo baada ya kuitimua mashindanoni Mbabane Swallows ya Uswatini (zamani Swaziland) kwa ushindi wa jumla ya mabao 8-1, ikishinda mabao 4-1 nyumbani Uwanja wa Taifa kabla ya kushinda mabao 4-0 ugenini.

Kwa upande wa Nkana FC, kabla ya kukutana na Simba iliicheza na Desportiva Do Songo ya Msumbiji na kuitandika jumla ya mabao 3-1, ikishinda 2-1 ugenini, kabla ya kutakata bao 1-0 nyumbani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles