Na AMINA OMARI-TANGA
MKOA wa Tanga unatarajiwa kufanya mkutano wa jukwaa la biashara litakalotumika kutangaza fursa za kiuchumi, kiuwekezaji pamoja na
biashara zilizoko katika mkoa huo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martine
Shigella, alisema mkutano huo unatarajiwa kufanyika Agosti 17, mwaka huu jijini Tanga.
Kupitia mkutano huo, Shigella alisema wanatarajia kubainisha aina za fursa za uwekezaji pamoja na biashara zilizoko katika wilaya zote mkoani hapa.
“Tayari tumeshafanya mkutano wa wadau wa kuwahamasisha kushiriki
mkutano huo kwani tumejipanga kuwaonyesha fursa zilizopo ikiwamo masoko kwa ajili ya wazalishaji watakaokuja na bidhaa zao.
“Katika hili, baadhi ya kampuni za uwekezaji kutoka nje ya nchi zimeshathibitisha ushiriki wao pamoja na wadau wa sekta binafsi walioko nchini.
“Kwa hiyo, halmashauri zote zilizoko mkoani hapa lazima sasa zianze mchakato wa kuainisha vikundi vya wafanyabiashara katika maeneo yao
pamoja na wawekezaji walioko katika maeneo yao.
“Pia, wakurugenzi wote lazima waainishe maeneo ya uwekezaji ili watumie fursa hiyo ya mkutano kuweza kujitangaza kwa wageni
watakaohudhuria katika mkutano huo.
“Nasisitiza hayo kwa sababu kuna watu watakaokuja kwa ajili ya kuangalia Tanga kuna fursa gani za kiuchumi na kujifunza namna bora zaidi ya kuboresha biashara zao pamoja na kutafuta masoko ya biashara hizo,” alisema Shigella.