NA FRANCIS GODWIN, IRINGA
RAIS Dk. John Magufuli amesema Serikali yake imeanza kulipa Sh bilioni 650 za madeni yake kila mwezi.
Hayo aliyasema jana alipokuwa akiwahutubia wananchi wa Kijiji cha Ndolela, Wilaya ya Iringa wakati akifungua barabara iliyojengwa kwa kiwango cha lami ya Iringa-Migori-Fufu yenye urefu wa kilomita 189.
Alisema madeni hayo ni yale yaliyokopwa na Serikali za awamu zote.
“Tumeanza kulipa madeni haya, kila mwezi tutatoa Sh bilioni 650…madeni haya yalikopwa na awamu zote zilizopita, inawezekana deni langu ninalokopa sasa likalipwa wakati mimi sipo duniani,” alisema Rais Dk. Magufuli.
Alisema deni linalokopwa sasa linaweza kulipwa hata miaka 50 ijayo kwa sababu linafuata taratibu zilizopo.
“Pamoja na kazi nzuri hii, unaweza kukutana na mtu anasimama bungeni, tena anatoka huku huku Iringa akipita katika barabara hii, alafu anahoji mbona Serikali inakusanya fedha nyingi zinakwenda wapi, jambo hili linashangaza,” alisema.
Kutokana na hali hiyo, aliwataka Watanzania kutambua uchumi wa nchi unazidi kukua ukilinganisha na nchi nyingine za Afrika, kwani umefikia asilimia saba na bado unaendelea kukua.
“Serikali ninayoiongoza ina lengo kubwa la kuwasaidia wananchi ambao ni masikini, tutahakikisha wananchi wananufaika na rasilimali zilizopo bila kubughudhiwa,” aliongeza.
Katika hatua nyingine, Rais Dk. Magufuli alisema sasa ni zamu ya Mkoa wa Iringa kujengewa miundombinu mizuri kama ilivyo Kanda ya Kaskazini ili Hifadhi ya Taifa ya Ruaha ipate watalii wengi.
Alisema hifadhi hiyo ina wanyama wa aina zote na wengi kuliko hifadhi nyingine, ila imekosa watalii wengi kutokana na kukosekana kwa miundombinu mizuri.
“Tumejipanga kujenga uwanja wa ndege wa Nduli kwa kiwango cha lami ili ndege kubwa ziweze kutua,” alisema.
Rais Dk. Magufuli aliongeza kwamba, ujenzi wa uwanja huo na barabara ya kiwango cha lami kutoka Iringa Mjini kwenda Hifadhi ya Ruaha, kutaongeza watalii zaidi.
Alisema kukamilika kwa barabara hiyo iliyojengwa kwa ufadhili wa Benki ya Maendeleo ya Afrika na Serikali ya Japan kwa kutoa mikopo yenye riba nafuu, kutawezesha ukuaji wa uchumi zaidi kwani barabara hiyo kutoka Afrika Kusini hadi Cairo nchini Misri, ilikuwa haijakamilika upande wa Tanzania pekee.
“Barabara hii ilikuwa na changamoto kubwa, wasafiri walikuwa wanatumia saa nyingi kufika Dodoma ama mikoa ya jirani, sasa wanatumia saa mbili na kidogo, tuitunze ili iwanufaishe wananchi,” alisema.
Kwa habari zaidi jipatie nakala ya gazeti la MTANZANIA.