Na GRACE SHITUNDU- DAR ES SALAAM
JOTO la kuelekea Uchaguzi Mkuu 2020 ni wazi limeanza kupanda, baada ya wenyeviti wa vyama vikubwa vya siasa nchini Rais Dk. John Magufuli wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na Freeman Mbowe wa Chadema wiki hii kutoa kauli kuhusiana na mikakati na mipango ya uchaguzi huo.
Kauli hizo zilizotolewa kwa nyakati tofauti na wenyeviti hao zimeonyesha wazi kuwa kila upande umejipanga kwa kiwango cha juu kuelekea uchaguzi huo 2020.
Wakati Mwenyekiti wa CCM, Dk. Magufuli akitoa maagizo ya kuandaliwa kwa Ilani ya Uchaguzi ya 2020/25 itakaainisha mambo muhimu yanayogusa wapigakura na kuwataka wanachama wa CCM kuacha kubweteka na kuacha kufanya kazi kwa mazoea kwani wanaweza kupoteza dola.
Kwa upande Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe mbali na kuonyesha kujipanga kuhakikisha hawafanyiwi figisu na kutoa tahadhari ya mzozo utakaotokea kusuluhishwa na Katibu wa Umoja wa Mataifa (UN), pia ameanika baadhi ya mikakati na kutoa maelekezo makali kwa viongozi wake wa chini.
Kauli hiyo ya Mbowe ilikuja zikiwa zimepita siku mbili tu baada ya kuonekana kwenye jukwaa la kitaifa katika sherehe za kuadhimisha miaka 58 ya Uhuru ambapo alitoa wito mbele ya Rais Magufuli ya kufanyika kwa maridhiano ili kuleta amani na utengamano.
Watu wanaofuatilia siasa wanasema kauli hizo za wenyeviti hao ambao vyama vyao vilichuana vikali katika Uchaguzi Mkuu uliopita wa 2015, vinaonekana kila upande kuwa na presha na uchaguzi huo.
Katika matokeo ya mwaka 2015 kwa nafasi ya Rais CCM kupitia Dk. Magufuli walishinda kwa asilimia 58.46 akiwa na kura 8,882,935 huku mgombea wa Chadema, Edward Lowassa alipata kura 6,072, 848 sawa na asilimia 39.97
Lowassa alisimama kugombea kiti cha uraisi kupitia Chadema wakiwa katika muunganiko wa vyama vinne vya Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD, uliounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA).
MAGUFULI
Wakati akifungua mkutano wa majadiliano ya wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC) jijini Mwanza, Rais Magufuli alitoa maagizo kwa NEC kuhakikisha inatengeneza ilani ya chama hicho kwa mwaka 2020/25 sambamba na sera au mpango wa utekelezaji wa serikali katika miaka 10 ijayo(2020/30) yenye mwelekeo wa kiuchumi unaotegemea sekta ya viwanda na kulifanya Taifa lijitengemee kiuchumi.
“Lazima ilani hii tutakayokuwa tumeitengeneza ama uelekeo wa Chama cha Mapinduzi , ujielekeze kwenye namna tunavyoweza kutumia rasilimali tuliyopewa na Mwenyezi Mungu kujiletea maendeleo na mabadiliko makubwa kiuchumi sisi kama taifa”alisema Rais Magufuli.
Miongoni mwa mambo ambayo Rais Magufuli aliwataka wajumbe wa NEC kuyapa kipaumbele ni pamoja na afya, elimu, maji, kilimo na mifugo, madini, utalii na miundombinu.
Kuhusu Afya Rais aliwataka wajumbe kuhakikisha wanazingatia sera ya kuwa na kituo cha kutoklea huduma ya afya kila kata, kijiji na mtaa.
Pia Rais alisisiza sekta ya elimu kupewa kipaumbele kwa kujikita kuinua ubora wa elimu ya msingi, sekondari na kuhakikisha zinakuwa na mazingira yanayofaa.
Kuhusu sekta ya maji alisema lengo liwe kuongeza vyanzo vya maji na kasi ya usambazaji ili kujitosheleza mahitaji kwa asilimia 100 mjini na vijijini.
Kilimo na mifugo alisema ni vyema sekta hiyo ikapewa msukumo mpya wa kipekee, kwa kuwa ndio kichochea cha sekta ya viwanda.
Kwa upande wa madini Rais Magufuli alisema ilani iwe na lengo la kuhakikisha madini yote yanasindikwa na kuongezwa thamani kabla ya kuuzwa na kuwajengea uwezo wazawa wa kuwekeza kwenye sekta hiyo.
Kuhusu miundombinu, alisema lengo ni kuendelea kujenga mtandao wa barabara kwa uunganisha wilaya zote na kuhakikisha barabara mapaka mitaa zinajengwa.
Pamoja na maagizo hayo Mwenyekiti huyo wa CCM aliwataka viongozi wa kupitia chama hicho kutojisahau na kufanya kazi kwa mazoea kwa kuwa hata CCM inaweza kuanguka kama ilivyotokewa kwa vyama vingine vikongwe duniani.
Rais katika kauli zake pia alikipongeza chama chake kwa kushinda uchaguzi wa Serikali za Mitaa na kusema kuwa ni dalili nzuri kwa uchaguzi mkuu ujao.
MBOWE
Mbowe ambaye alikuwa kama akijibu hoja za Rais Magufuli mbali na kutahadharisha kushtaki kwa Katibu Mkuu wa UN, alianika jinsi chama hicho kilivyokwishaanza kujipanga kuanzia ngazi ya mashina.
Mbowe alitoboa siri hiyo katika mkutano mkuu wa Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha) uliofanyika jijini Dar es salaam.
Alisema pamoja na kuzuiliwa kufanya mikutano ya hadhara walikuwa wakiendelea kufanya siasa kimya kimya za mtu kwa mtu, nyumba kwa nyuma na kitongoji kwa kitongoji na kusajili wanachama zaidi ya milioni sita
“Leo hii sitamani mikutano ya hadhara, natamani kufanya siasa za namba, namba hazidanganyi tuliamua kufanya kimyakimya pasipo kushirikisha au kutangaza kwenye vyombo vya habari na tulifanikiwa”alisema Mbowe.
Mbowe pia alitahadharisha viongozi wavivu na wasiofanya juhudi ya kuleta wanachama wapya kuwa watafukuzwa.
“Unakuwa kiongozi unawanachama 3,000, mwaka wa kwanza wanakuwa 2,000, na wa tatu 10,000 halafu tukuache uendelee kuongoza eneo husika tunakufukuza” alisema Mbowe.
Aliongeza kusema, “Nawaambia Bawacha , Uchaguzi Mkuu (uchaguzi wa ndani ya chama hicho ) ukimalizika Disemba 19 hakuna muda wa kupumzka wala kusubiri ratiba ya kampeni ya Tume ya Uchaguzi (NEC)”
Pia alieleza walivyojipanga kidigitali na kwamba Desemba 18 mwaka huu watazindua mfumo wa wa taarifa.
“Tutazindua mfumo wa digitali (Chadema digital) katika mfumo wa taarifa, kila kitu kitafanyika kidigitali, zikiwemo taarifa za chama na kampeni zetu,” alisisitiza Mbowe.
Mbowe pia alibainisha kuwa chama hicho kina wanachama milioni 6 ambao endapo watakichangia watakusanya Sh. Bilioni 12 ambazo zitasaidia katika kampeni za uchaguzi mkuu mwakani.
Katika uchaguzi wa 2020 CCM kimevuna wanachama wengi waliokuwa upinzani na hivyo kuwa na mtaji mkubwa wa kuingia nao.
Lakini kwa upande wa vyama vya upinzani hasa Chadema wanatarajia kuingia katika uchaguzi huo wakiwa maumivu ya wanachama wake wengi kuhamia CCM, kuzuiliwa kufanya mikutano ya hadhara na pia maumivu ya kususa kushiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa madai ya kufanyiwa figisu.