27.1 C
Dar es Salaam
Thursday, December 7, 2023

Contact us: [email protected]

Askofu Gwajima apata mtikisiko mkubwa

Na FARAJA MASINDE-DAR ES SALAAM

ASKOFU  wa Kanisa la Ufufuo na Uzima (GCTC), Josephati Gwajima, amepata pigo baada ya baadhi ya wachungaji wa makanisa yake wakiwamo viongozi wa makao makuu, kuandika barua za kuachia nyadhifa zao ndani ya kanisa hilo.

Wachungaji hao wametangaza kujiuzulu kulitumikia kanisa hilo kwenye maeneo mbalimbali nchini huku baadhi yao wakitoa sababu ya kupewa maelekezo na Mungu.

Barua hizo ambazo MTANZANIA lilifanikiwa kupata nakala zake, baadhi ya wachungaji wameshindwa kutaja sababu za moja kwa moja ambazo zimewafanya kuachia nyadhifa zao wakiishia kusema sababu ni matatizo ya kifamilia na wito wa Mungu.

Mmoja ya Wachungaji hao ambaye aliandika barua ya kuomba kuachia nyadhifa zake ndani ya kanisa hilo ni, Frederick Fussi, ambaye ametangaza kujiuzulu nafasi za Uchungaji ngazi ya Ap/Rp, Ujumbe wa bodi ya masmit.

Nafasi nyingine aliyotangaza kuachia ni ya Mkurugenzi Mkuu wa kurugenzi ya Habari na Mahusiano, Mkurugenzi Mkuu wa Kurugenzi ya usimamizi wa Mali za Ufufuo na uzima duniani na Katibu Mkuu Msaidizi wa Kanisa la Glory of Christ Tanzania Church (GCTC).

“Baada ya kutumika chini ya uongozi wako ukiwa kama baba na mlezi wangu kiroho kwa miaka 13 tangu mwaka 2006, itoshe kusema kuwa imani yako kwangu haikuwahi kutiliwa mashaka.

ASKOFU  wa Kanisa la Ufufuo na Uzima (GCTC), Josephati Gwajima

“Ukiwa kama Askofu Mkuu wa Makanisa ya Ufufuo na Uzima Duniani natumia fursa hii, kwa namna ya kipekee kabisa, kukushukuru kwa kuamua kunipatia fursa mbalimbali chini ya uongozi wako na kuniteua kushika nyadhifa zote ambazo zimetajwa katika kichwa cha barua hii. 

“Hivyo kwa kulitambua hilo, mimi Frederick Fussi, kwa dhati ya moyo wangu nimeamua, tarehe 5 Desemba, 2019 kujiuzulu nafasi zangu zote chini ya uongozi wako, aidha najiuzuru nafasi nyingine yoyote ambayo sikuitaja (kama ipo). 

“Nimekwisha wasilisha nyaraka zote zilizokuwa chini yangu kwa Mkuu wa Utawala na Fedha,” inasema barua hiyo ya Fussi.

Barua nyingine ambayo gazeti hili imeiona ni ya Adriano Makazi, ambaye alikuwa Mchungaji wa Kanisa la Glory of Christ (T) Church lililoko Ubungo Chai Bora jijini.

“Leo Desemba 13, 2019 kwa ridhaa yangu mwenyewe nimeamua kujiuzulu nafasi ya uongozi ya Resident Pastor (Rp) na kazi zote nilizokuwa nazifanya kwenye ngazi hiyo, maamuzi haya nayafanya nikiwa naakili zangu timamu kabisa bila kushawishiwa na mtu au kitu chochote hivyo nachukua nafasi hii kusema kuwa mimi siyo tena Resident Pastor (Rp) wa Glory of Christ (T) Church kuanzia leo,” alisema Makazi kupitia barua hiyo.

Barua nyingine ambayo Mtanzania iliiona ni ya Dk. Gwandumi Mwangasa (MD) wa Moshi Kilimanjaro ambayo ilisema “nimekuwa na mikutano tofauti na Bwana Yesu Kristo akinitaka niweke kando mgawo mpya alioutoa. 

“Kuhusu andiko 1 Samweli 15:22 …. Tazama, kutii ni bora kuliko dhabihu …. nilijikuta sina chaguo lingine ila kutii sauti ya Mungu (Rhema) kabla ya mbio mbaya dhidi yangu. 

“Siku zote nimekuwa mwaminifu kwa maono, misheni na malengo ya GCTC kwa miaka (21), kwa kuwa Bwana amenipa mgawo mpya ambao unaashiria mwanzo wa maono mapya katika maisha yangu, nimeona ni busara kujitokeza ili kuepusha machafuko katika uwakili wangu kwa mwili wa Kristo. ninashukuru kwa dhati na kuhisi kuheshimiwa kubezwa na kukuzwa na wewe hadi siku hii ya leo.

“Ninalazimika kutoa njia hii kwa kuwa niko nyuma kwa safari yangu kwenda nje ya nchi kwa jambo muhimu sana, kumtumikia Bwana huko,” alisema Dk. Gwandumi Mwangasa (MD) kupitia barua yake.

Mwingine ni Bruno Massae ambaye alikuwa Askofu  wa Kanisa hilo mkoani Iringa, ambaye ametangaza kujivua nyadhfa zake kwa kile alichoeleza kwenye barua hiyo kuwa anataka kutumika kwenye eneo jingine kutokana na maelekezo aliyopewa na Mungu.

Pia barua nyingine ilikuwa ni kutoka kwa Mchungaji Frank Andrea ambaye alitangaza kujiuzuru nafasi za uongozi wa kanisa hilo mkoani Arusha kwa sababu za kifamilia.

ASKOFU  wa Kanisa la Ufufuo na Uzima (GCTC), Josephati Gwajima

“Ninaandika kukujulisha kuwa ninajiuzulu uongozi katika nafasi zote nilizokuwa nazo katika Kanisa la Ufufuo na Uzima mara moja kuanzia leo kutokana na sababu za kifamilia, kwa sababu hiyo kutokana na matatizo ya kifamilia ninalazimika kusafiri kwenda Mwanza ilikutatua matatizoya kifamilia, nimekuwa na changamoto ya kifamilia inayonifanya nishindwe kabisa kuendelea na kazi hii mpaka nimalize haya matatizo.

“Hivyo nimeona ni busara kutochanganya mambo ndani ya Kanisa la GCTC, hivyo imenilazimu kuchukua maamuzi haya ya kujiuzulu nafasi zangu zote za uongozi katika Kanisa la Glory of Christ Tanzania (GCIC) na baada ya kumaliza matatizo hayo nitakuja Dar es Salaam kukuaga Baba yangu, naomba mtu mwingine atumwe ili aendeleze hii kazi ya Mungu hapa Arusha, kwa sasa SNP Godfrey Kaulua mwangalizi wa Longido- Namanga yupo anaendelea na kulisimamia kanisa,” ilisema barua hiyo.

Mwingine ni Mchungaji, Kelvin Mwaipopo, ambaye kupitia barua yake amesema amejiuzulu nafasi zake zote za uongozi ndani ya kanisa hilo.

“Mimi ni Mwangalizi wa Kanisa Wilaya ya Nzega mjini niliyeteuliwa na Askofu Mkuu tangu Desemba 2015, barua hii inahusu kujiuzulu nafasi zangu za uongozi kwa sababu zisizo zuilika za kifamilia.

“Toka baba yangu amefariki nikiwa kama mtoto mkubwa katika familia yetu, ninahitajika kwenda kusimamia masula aya kifamilia ambayo yataniweka mbali na kwa muda mrefu sana na huduma ya Nzega hivyo sitaweza kutumikia nafasi zangu za kihuduma hivyo nafasi zangu ni vyema akawekwa mtu mwingine,” alisema Mwaipopo kupitia barua yake.

Gazeti hili liliwatafuta baadhi ya wachungaji hao ili kujiridhisha iwapo barua hizo ni za kwao, ambapo mmoja wa waliozungumza ni Frederick Fussi, ambaye alikiri barua hiyo kuwa yake.

“Ni kweli, hiyo ni barua yangu na sababu ni kama nilivozitoa kwenye barua hiyo,” alisema Fusi.

Wachungaji wengine ambao ni Frank Andrea na Kelvin Mwaipopo walidai kuwa wako kwenye maeneo yasiyo rafiki na hivyo watafutwe baadaye. 

Gazeti hili lilimtafuta Askofu Gwajima ili kutolea ufafanuzi wimbi hilo la kukimbiwa na wachungaji wake lakini simu yake ya mkononi ilikuwa haipatikani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
580,000SubscribersSubscribe

Latest Articles