31.2 C
Dar es Salaam
Monday, July 22, 2024

Contact us: [email protected]

JPM ashusha nyundo 10 kwa aliowatumbua

NORA DAMIAN Na ANDREW MSECHU

-DAR ES SALAAM

RAIS Dk. John Magufuli ameeleza hadharani sababu 12 zilizosababisha atengue uteuzi wa aliyekuwa Waziri wa Viwanda na Biashara, Joseph Kakunda na Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Charles Kichere.

Alisema jukumu lake ni kuteua na anapotengua uteuzi wa mteule wake, si kwamba anamchukia mtu bali anataka kuona matokeo ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM.

Akizungumza jana baada ya kuwaapisha Waziri wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa, Kamishna wa TRA, Dk. Edwin Mhede na Katibu Tawala wa Mkoa wa Njombe, Charles Kichere, alisema anapomteua mtu anataka kuona matokeo mazuri.

“Nampongeza Kakunda kwa kuja hapa, huku ndiko kukomaa kisiasa, hizi kazi ni ‘temporary’, lakini ni ukweli kwamba kwenye wizara ‘hakui–push’ ninavyotaka mimi.

“Changamoto za wafanyabiashara, kwani palikuwa na ubaya gani naibu waziri, katibu mkuu, waziri mwenyewe, si wangeshapanga mikutano na wafanyabiashara msikililize shida zao, nani aliwakataza.

“Ndiyo maana wanakuja wanasema hawajawahi kumuona, lakini hata ningewauliza labda (Naibu Waziri Stella) Manyanya wangesema hawajawahi kumuona,” alisema Rais Magufuli.

Alisema licha ya wizara hiyo kuwa na jukumu la kufanya biashara, imeshindwa kutafuta masoko ya mazao mbalimbali, ikiwemo korosho iliyokusanywa katika maghala.

Alisema Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Jeshi la Wananchi ilikusanya korosho tani 223,000 lakini Wizara ya Viwanda na Biashara imebangua tani 2,000 tu.

“Zingine wanasubiri mpaka nani ateremke ndio awaambie, sasa mnatakiwa kuuza hizi korosho, wizara inaitwa Viwanda na Biashara ni biashara gani imefanya?

“Korosho zimekaa wakati Tanzania ndio tulikuwa wazalishaji peke yetu, tumesubiri hadi Machi nchi nyingine zikaingia bado hatujauza. Unakuwa na liwizara la kupeperusha bendera barabarani,” alisema.

Rais Magufuli alisema pia licha ya wizara hiyo kuwa na vyombo mbalimbali, lakini vimeshindwa kuonesha uwajibikaji hasa katika kutafuta masoko.  

“Wizara ina vyombo vyote vya kufanya biashara, Tantrade (Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara) ipo pale… ilitakiwa niifagie (wizara) kutoka juu hadi chini,” alisema.

Alisema pia viwanda vingi vilivyobinafsishwa havifanyi kazi huku vingine vikibadilishwa matumizi, akitolea mfano kiwanda cha nguo Mbeya ambacho kinakusudiwa kubadilishwa kiwe cha kutengeneza pipi.

“Innocent (Waziri wa Viwanda) inawezekana wamekupongeza, lakini nilifikiri wakupe pole… mimi naangalia haya, nikiona hayaendi natengua.

“Jukumu langu ni kuteua ili kukidhi kiu ya Watanzania, na ninapotengua mahali si kwamba wewe nakuchukia, nakupenda tu. Watanzania walionichagua wanataka waone utekelezaji wa ilani ya uchaguzi,” alisema Rais Magufuli.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles