22.5 C
Dar es Salaam
Sunday, July 21, 2024

Contact us: [email protected]

JPM ASHTUKIA MCHEZO MCHAFU TRA

Na NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM


RAIS Dk. John Magufuli amebaini kuwapo mchezo mchafu Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na kuwaagiza Kamishna wa mamlaka hiyo, Charles Kichere na Wizara ya Fedha kusimamia suala hilo.

Akizungumza jana wakati wa kuweka jiwe la msingi ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa (Standard Gauge) kutoka Morogoro hadi Makutupora mkoani Dodoma, alisema kodi zimeonekana kero kwa wananchi na kusababisha wabuni mbinu za kukwepa kulipa.

“TRA muangalie kodi zenu mnazozitoza, inawezekana zingine ni kubwa mno kuliko miradi wanayoitekeleza wananchi.

“Badala ya kuwa motisha, inakuwa kero kwa walipakodi na badala yake wanabuni mbinu za kukwepa kulipa wakati wangeelimishwa vizuri wangeweza kulipa, hivyo mkajipange vizuri,” alisema Rais Magufuli.

Alisema pia kodi za majengo wananchi wanatozwa Sh 600,000 hadi milioni moja wakati alishawahi kupendekeza kuwe na kodi zinazolingana.

“Tuliwaambia mpige ‘flat rate’ ambayo itakuwa motisha kwa Watanzania wengi wawe wanalipia majengo yao, lakini kuna watu TRA si wazuri na saa zingine wanaipaka matope kwa kusema hii ndiyo dhana ya hapa kazi tu, kumbe wao ndio wanatafuta namna ya kuliibia taifa.

“Kamishna wa TRA, Naibu Waziri wa Fedha, Katibu Mkuu mkalisimamie hili ili kulipa kodi isiwe ni kero bali heshima… mwananchi aende kulipa kodi kwa heshima ya taifa lake,” alisema.

Pia aliwatahadharisha wafanyabiashara wanaotoa risiti tofauti na viwango halisi vya bei na wateja wanaokubali kuzipokea kuwa wanaiibia Serikali.

“Pamekuwa na mtindo mtu anapokwenda kununua bidhaa anapewa risiti ya bei ndogo badala ya risiti anayotakiwa kupewa. Mtoa risiti na mpokea risiti wote wanaiibia Serikali na kuchelewesha maendeleo, nawaomba Watanzania tuwe wazalendo.

“Tendelee kulipa kodi ili kutekeleza miradi ya maendeleo na kuboresha huduma mbalimbali za jamii,” alisema Rais Magufuli.

 

KUZALIANA

Akizungumzia idadi ya watu nchini, alisema licha ya kuongezeka, lakini hakutakuwa na madhara iwapo watashiriki katika kuleta maendeleo ya nchi.

“Tanzania tuna bahati kwa sababu ya ukubwa wa nchi yetu, hivi karibuni tuliambiwa tumefika milioni 55, wapo waliosema tunazaana mno, mimi nasema tuzaane zaidi.

“China wako bilioni 1.3 na ndiyo maana uchumi wake uko juu. Mkiwa wengi mnakuwa na sauti, tuko milioni 55, idadi ya watu wetu ni sauti tosha katika EAC, SADC.

“SADC wako zaidi ya milioni 400 na EAC zaidi ya milioni 165, kinachotakiwa tuchape kazi, suala si kuwa wengi bali namna gani Watanzania wanashiriki katika kuleta maendeleo ya nchi yao.

“Denmark wako milioni 5, lakini kwa sababu ya kuchapa kazi wamekuwa wakitoa misaada mpaka kwa nchi kama Tanzania yenye watu milioni 55.

“Hivyo tusiogope kuwa wengi, hata kama tungekuwa milioni moja, kama hatufanyi kazi tutalia tu njaa, vyuma vitatubana,” alisema.

 

AMANI

Kuhusu amani nchini, aliwataka Watanzania kuilinda na kuidumisha kwani ni muhimu kwa maendeleo ya nchi.

“Lazima tujue mahali tulikotoka, tulipo na tunakokwenda. Haijalishi kwamba haya yanafanyika wakati Magufuli rais, mimi ni wa kupita tu, lakini maendeleo ya Tanzania lazima yabaki.

“Alikuwepo Nyerere, Mwinyi, Mkapa, Kikwete walifanya yao wakaondoka. Na mimi nitafanya yangu nitaondoka, lakini Tanzania itaendelea kubaki,” alisema.

 Kwa habari zaidi jipatie nakala ya gazeti la MTANZANIA.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles