26.2 C
Dar es Salaam
Thursday, June 1, 2023

Contact us: [email protected]

YA UHURU NA RAILA, NCHI NI KUBWA KULIKO WATU

NASIKIA kuwa kuna viongozi wamefukuzwa kutoka kwenye ofisi za Serikali kwa sababu tu ni watu wa “Upinzani”na huwa sielewi maana ya neno hilo upinzani.

Wenzetu Marekani Husema Republican au Democrat- hawasemi Democrat thidi ya wapinzani au Republican dhidi ya Wapinzani. Hapa ni hilo ni shairi lisilo na mwisho. Nasikia tena kuna mtu mwingine amesema katu hatashirikiana na Chadema kwa sababu chama hicho hakijatajwa kwenye ilani ya chama chake.

Ninataka kusikia kwa masikio yangu kama alisema hivyo, maana hata Rais Magufuli sijawahi kumsikia akitamka maneno hayo.

Huwa namsikia akisema maendeleo hayajali chama. Hii sasa ni Lugha mpya kabisa! Lakini kwa sasa Tanzania imevamiwa na lugha ya undava –tough talk, kutoka kila kona na huku wananchi wasijue nini kiwe dira yao ya maendeleo. Tanzania imegawanyika kisaikolojia, kiitikadi, na baadhi yetu tunaosoma mtini za kisiasa- political discourse analysts, tunaona kuwa nchi inahitaji kuponyana.

Ee Roho wa Allah ashuke sasa, si ajabu mwezi huu!
Niliandika wiki mbili zilizopita au tatu zilizopita kuwa dhambi ya ubaguzi huwa tunakubali kuifanya mara moja kwa miaka mitano. Dhambi hii huhusisha watu kukaa katika makundi ya kisiasa, wenyewe wakiita vyama na kugombania kwenda Ikulu kwa kunadi sera zao na hatimaye kiongozi akipatikana kwa kura na baada ya hapo dhambi hiyo hufutwa na wote tunarudi tena kwenye kambi moja kama Taifa au chama na kuendelea na ujenzi wetu wa Taifa.

Tunajua ndani ya vyama na baina ya vyama makundi yanaweza kuendelea lakini huwa tunayapuuza na pengine kusuluhishana; mfano wakati wa Serikali ya Awamu ya Nne ambapo watu walialikana Ikulu au hata nje ya Ikulu kunywa chai pamoja na kujadiliana namna ya kuvunja makambi yanayojali watu badala ya Taifa.

Lakini safari hii uponyaji huu wa kunywa chai pamoja haupo na lugha ile ya undava ndio inaanza kuwa kauli mbiu na huku mwananchi hana uhakika kutokana na matukio yasiyoweza kuelezewa na mamlaka husika ila kwa ukimya au ngano ambazo hazijengi mashiko.

Tanzania ni kubwa kuliko mtu au chama au kikundi ndani ya chama kiwe nje ya utawala au ndani ya utawala. Na ndiyo ujumbe tunaoupata kutoka kwa majirani zetu, Raila na Uhuru (Rais wa Kenya), kama wanayoyafanya ni ya dhamiri yao na yana dhati ya kiroho. Yasije kuwa yale ya wasanii wanaosema niambie tu kama unanipenda hata kama nimekufuma una mpenzi mwingine ili roho yangu itulie. Lakini maneno aliyotamka Uhuru Kenyatta ndio ya msingi ya kusema Kenya kwanza mtu baadaye na sisi ifike mahali tuseme kuwa mtu atakuja baada ya Taifa na umoja wa kitaifa na sio kabla ya hapo.

Taifa haliishi kwa siasa tu! Ila siasa- kama mapambano ya kutaka kutawala- na ni moja tu ya ainisho, maana siasa inahusu uponyaji, upatanisho, kusameheana, kufikiria wanyonge watakaoumia mafahali wawili wakiumana pembe, kufikiri uchumi unapoporomoka kwa sababu kila mmoja anaishi kwa woga undava unapokuwa lugha za siasa wanaofanya siasa za kindava.

Siasa ni pamoja na kukubali undava utaiacha siasa na kuwaharibu wanaofanyia undava. Siasa itandelea kuwapo kuwakaribisha wachezaji wengine kama mandava watajiharibu. Ndivyo siasa iivyo! Tunaishi kwa uchumi, tunaishi kwa biashara, tunaishi kwa elimu, tunaishi kwa huduma za afya, tunaishi kwa barabara. Ni mazao ya siasa ambazo zinafikiria watu sio kutishiana nani ni mndava kuliko mwenzake.

Raila alionesha undava kwa kujiapisha na Uhuru alionesha undava kwa kuwafukuza Wakenya wenzake ili waende wakaishi nje ya nchi. Hakuna aliyefaidi kati yao. Waliokuwa tu wanaongeza uchungu kwa kutia chumvi katika kidonda cha ukabila na cha tofauti za kiitikadi. Natumaini kila mmoja alikiri kuwa alifanya kosa kwa kudhani undava ndiyo suluhisho, badala ya kuahirisha ile dhambi ya utengano wa muda wakati wa uchaguzi.

Kenya iliwahi kuvuja damu na hadi wakapelekana ICC, sielewi yalimalizikaje huko lakini sasa wameona kuwapatia amani Wakenya na kuruhusu uchumi ukue, wawekezaji wawe na uhakika na amani na fedha zao, wakae pamoja. Picha waliyopiga wakiongea na wananchi imepeleka ujumbe mkubwa kuwa kukaa pamoja na kuupuuza undava inawezekana.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
213,225FollowersFollow
568,000SubscribersSubscribe

Latest Articles