33.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

JPM afyeka mafao yake

Tanzania's President elect Magufuli addresses members of the ruling CCM at the party's sub-head office on Lumumba road in Dar es Salaam*Aridhia makamu wake, mawaziri, ma-RC, DC nao kukatwa kodi

*Harakati za wabunge kunusuru kiinua mgongo chao zakwama

Na Arodia Peter, Dodoma

RAIS Dk. John Magufuli ameunga mkono ukatwaji wa kodi kwa wabunge wote kwenye kiinua mgongo, huku na yeye akiridhia kukumbwa na hatua hiyo.

Pamoja naye pia amesema ni lazima viongozi wawe mfano kwa jamii, hivyo pia ameridhia kukatwa kodi kwa Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, majaji, mawaziri, wakuu wa mikoa na wilaya wote.

Hayo yalisemwa jana bungeni na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, alipokuwa akijibu hoja za wabunge, ambapo alisema kuwa siku alipowasilisha pendekezo hilo la kukatwa kiinua mgongo kwa wabunge, Rais Magufuli aliridhia mara moja na kusisitiza kwamba kulipa kodi ni wajibu wa Watanzania wote kama njia ya kujenga nchi.

“Mheshimiwa Spika, naomba niliarifu Bunge lako tukufu kwamba siku nilipowasilisha pendekezo hili kwa Rais Dk. John Magufuli, aliridhia mara moja na kusisitiza kwamba kulipa kodi ni wajibu wa Watanzania wote ili tujenge nchi yetu.

“Na kwa kuwa kiongozi lazima aongoze kwa mfano, alielekeza kuwa yeye ni mbunge wa Tanzania nzima na anapenda awe wa kwanza kukatwa kodi stahiki kwenye mafao yake ya kustaafu.

“Hivyo napenda kufafanua kwamba marekebisho niliyowasilisha mbele ya Bunge lako tukufu Juni 8, 2016 katika hotuba yangu ya Mapendekezo ya Serikali Kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha kwa mwaka 2016/17, maana yake ni kuwa kiinua mgongo cha viongozi wote wa kisiasa waliotajwa kusamehewa kodi chini ya Sheria ya Mafao ya Viongozi wa Kisiasa kitakatwa kodi,” alisema Dk. Mpango huku wabunge wakiwa hawashangilii.

Alisema kwa mujibu wa Sheria ya The Political Service Retirement Benefits Act 1995 kwa sasa kiinua mgongo cha rais kitakatwa kodi, pamoja na cha Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

Mbali na hao, alisema panga hilo la kodi pia litamwangukia Spika na Naibu Spika wa Bunge, mawaziri, manaibu waziri pamoja na wakuu wa mikoa na wilaya.

Dk. Mpango alisema mabadiliko hayo yanafanyika kwa mujibu wa kifungu 10(3) cha Sheria ya Kodi ya Mapato ambacho kimeweka sharti la kutotambua misamaha mingine yoyote ya kodi ya mapato ambayo haijatolewa na sheria hiyo.

Hatua ya kukatwa kwa kodi hiyo ilitokana na pendekezo la mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe (CCM), ambaye alisema kuwa suala la kodi kwenye kiinua mgongo kwa wabunge linaweza kuwachonganisha na wananchi.

Kutokana na hali hiyo, alipendekeza rais, makamu wa rais, waziri mkuu, majaji, wakuu wa mikoa na wilaya nao wakatwe kodi hiyo.

Dk. Mpango alisema kuwa kwa mujibu wa Sheria ya Kodi ya Mapato, Sura 332 kodi ya mapato hutozwa kwenye vyanzo vyote vya mapato.

“Kiinua mgongo ni chanzo kimojawapo cha mapato kinachotambuliwa na sheria na hutozwa kodi. Msamaha huu hauzingatii kanuni ya usawa ya utozwaji kodi, kwani watu wengine wote wanaopata malipo ya kiinua mgongo, iwe katika sekta binafsi au utumishi wa umma, hutozwa kodi katika mapato hayo. Kwahiyo, hatua hii imechukuliwa ili kujenga misingi ya usawa na haki katika ulipaji wa kodi,” alisema Dk. Mpango.

Alisema lengo la kufanya marekebisho hayo sasa ni kwa ajili ya kuweka utaratibu wa kisheria ambao utatumika kukokotoa stahili za mbunge endapo ukomo wa mbunge yeyote utatokea katika kipindi cha kuanzia Julai, 2016 na kuendelea.

Pamoja na hali hiyo, alisema mabadiliko haya yanafanyika sasa ili kuzingatia msingi wa utozaji kodi ambao unataka kodi iwe inatabirika.

Kuhusu pendekezo la wabunge kutaka nyongeza ya tozo ya Sh 50 kwa kila lita ya petroli na dizeli ili fedha hizo ziende kwenye Mfuko wa Maji, Waziri Mpango alisema halitekelezeki kwakuwa litaongeza mfumuko wa bei nchini.

“Napenda waheshimiwa wabunge mnielewe, Serikali haitaongeza kodi hiyo kwa sababu pendekezo hilo litasababisha kuongezeka kwa mfumuko wa bei na kushusha uzalishaji nchini, tunatambua umuhimu wa maji ndiyo maana bajeti ya mwaka huu imeongezwa kutoka bilioni 373/- za mwaka jana hadi kufikia bilioni 690/- mwaka huu,” alisema Dk. Mpango.

Aidha pendekezo la wabunge kutaka ongezeko la fedha Ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali, (CAG), Dk. Mpango alisema hakutakuwa na ongezeko lolote.

Katika bajeti ya mwaka huu Ofisi ya CAG imepangiwa Sh bilioni 44 badala ya Sh bilioni 72 za mwaka jana, na kati ya hizo zilitolewa Sh bilioni 32 na kusababisha kushindwa kufanyika ukaguzi katika maeneo 21 kati ya 27 yaliyopaswa kukaguliwa, yakiwamo halmashauri na kwenye mikataba ya madini.

Dk. Mpango alisema kuwa Serikali inatambua umuhimu na majukumu ya msingi ya Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi kama ilivyo kwa taasisi nyingine nyeti, ikiwemo vyombo vya ulinzi na usalama, mihimili mingine ya dola na uwezo wa kukabiliana na dharura.

“Hivyo, endapo kutajitokeza mahitaji ya lazima ambayo yatakwama kutekelezwa na Ofisi ya CAG kutokana na ufinyu wa bajeti, Serikali itahakikisha mahitaji hayo yanazingatiwa wakati wa mapitio ya utekelezaji wa bajeti kwa kipindi cha nusu mwaka,” alisema.

Akizungumzia ukomo wa bajeti ya matumizi mengineyo (OC) uliotengwa kwa mafungu mbalimbali, alisema  umezingatia uamuzi na mkakati wa Serikali wa kupunguza matumizi ya kawaida na kuelekeza fedha nyingi katika bajeti ya miradi ya maendeleo.

“Katika kufikia ukomo wa matumizi mengineyo kwa Serikali nzima (wizara, idara, taasisi za kiserikali, mikoa na halmashauri), uchambuzi wa kina ulifanyika kubaini mahitaji ya fedha ambayo si ya lazima kwa wakati huu na hivyo hayawezi kuathiri utendaji wa taasisi husika.

“Miongoni mwa mahitaji yaliyopunguzwa ni gharama za kumbi za mikutano, mafunzo na safari za nje zisizo za lazima, maadhimisho na sherehe, posho na kudhibiti matumizi ya magari kwa mafungu yote. Aidha Serikali iliangalia miradi ambayo inaweza kutekelezwa kwa awamu,” alisema .

Mapendekezo mengine ya wabunge ni pamoja na kuondoa kodi ya usajili wa bodaboda kutoka Sh 45,000 za sasa na kuwa 95,000 huku wakitaka magari kulipia kodi ya Sh 250,000 badala ya Sh 150,000.

Kuhusu matumizi makubwa ya sarafu ya dola ya Marekani nchini, Dk. Mpango alisema Serikali haiwezi kuingilia suala hilo kwa amri kwani inaweza kutia woga na kusababisha wawekezaji kukimbia uchumi.

 

MIAMALA YA SIMU

Waziri Dk. Mpango alisema ushuru wa bidhaa unaopendekezwa katika miamala ya fedha (Excise Duty on Money Transfer) hautakatwa kwenye fedha zinazotumwa au kupokewa, bali katika ada inayotozwa na benki au kampuni ya simu.

Alisema kwa sasa sheria inatamka kwamba ada hii itatozwa katika kutuma fedha tu, ambapo hata hivyo, baadhi ya kampuni za simu na benki zimekuwa zikitumia mwanya wa sheria hiyo kupunguza wigo wa kodi kwa kutoza ada wakati wa kupokea.

“Kwa mapendekezo haya, ushuru wa bidhaa utatozwa kwenye ada ya miamala ya uhawilishaji fedha ama wakati wa kutuma au kupokea fedha au vyote viwili kadiri itakavyotozwa.

“Mantiki yake ni kuwa ushuru huu utalipwa na benki au kampuni ya simu na si mtumaji au mpokeaji. Hata hivyo, Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Benki Kuu ya Tanzania (BoT), itawajibika kuhakikisha kwamba tozo hiyo inaendana na uhalisia wa huduma itolewayo na kufanya ukaguzi wa miamala ya makampuni ya simu kabla na baada ya tozo ili yasihamishie mzigo kwa mtumiaji wa mwisho,” alisema.

 

WAPITISHA BAJETI BILA UPINZANI

Bajeti ilipitishwa jana kwa jumla ya wabunge 252 wa CCM waliopiga kura za Ndiyo, ambao hawakuwepo bungeni ni 137.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles