26.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 18, 2024

Contact us: [email protected]

JPM aagiza uchunguzi ajali iliyoua 19 Mbeya

IBRAHIM YASSIN-SONGWE

RAIS Dk. John Magufuli amezitaka Mamlaka zinazohusika na usalama wa barabarani mkoani Songwe kuchunguza na kisha kuchukua hatua katika ajali ya gari la abiria iliyoua watu 19 likitokea Halmashauri ya Mji wa Tunduma wilayani Momba mkoani Songwe.

Rais Magufuli alitoa agizo hilo jana kupitia taarifa iliyotumwa na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu, ambapo mbali na kuzitaka mamlaka hizo kujipanga vizuri kukabiliana na matukio ya ajali za barabarani, pia alitoa  pole kwa ndugu, jamaa, marafiki na wote walioguswa na vifo vya watu hao.

AJALI ILIVYOTOKEA

Taarifa kutoka eneo la tukio na polisi zinaeleza kuwa 17 kati ya watu hao 19 waliofariki hapo hapo walikuwa ni abiria wa basi hilo lenye namba za usajili T 269 CJC.

Inaelezwa kuwa basi hilo liligongwa kwa nyuma na lori la mizigo lililokuwa limebeba shehena ya mahindi na kusababisha vifo hivyo.

Ajali hiyo ilitokea juzi saa 3:30 usiku katika Kijiji cha Senjele, wilayani Mbozi, mkoani hapa, ambapo abiria wote wa basi hilo walifariki dunia papo hapo, na abiria wawili waliokuwa kwenye lori walifariki muda mfupi baada ya kukimbizwa katika Hospitali teule ya Ifisi Mbeya Vijijini.

Juma Amily, ambaye alishuhudia tukio hilo, alisema akiwa pembezoni mwa barabara hiyo ghafla alisikia kishindo na aliposogea aliona watu wakiwa wamevunjika vibaya.

Alisema muda mfupi baadaye majirani na viongozi wa serikali walifika.

Mkuu wa Wilaya ya Mbozi, John Palingo, akiwa ameambatana na Mkuu wa Mkoa, walifika eneo la tukio  na kisha kushiriki katika zoezi la uokoaji, huku akisema kuwa tukio hilo ni la kwanza kutokea mwaka huu.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, George Kyando, alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kusema kuwa ilitokana na Lori lenye namba za usajili T 825 CNJ likiwa na tela lake namba T 388 CAA, lililokuwa likitoka nchini Kongo likiwa limebeba kichwa cha lori lingine kuelekea Jijini Dar es Saalam, kupata hitilafu kwenye mfumo wa breki.

Alisema lori hilo liligonga basi la abiria kwa nyuma, kabla ya kugonga lori lingine lenye namba za usajili T 371 BFX na tela lake lenye namba T 359 BGC likiwa na shehena ya mahindi ambalo lilikuwa likitokea mkoa wa Songwe kwenda mkoa wa Mbeya.

Alisema dereva wa lori lililosababisha ajali, Belege Mnubi, akiwa na mwanamke ambaye hata hivyo hakutambuliwa jina lake, walifariki dunia muda mfupi baada ya kufikishwa Hospitali teule ya Ifisi iliyopo Mbeya Vijijini kwa ajili ya matibabu baada ya hali zao kuwa mbaya.

“Dereva na yule mwanamke walipoteza maisha baada ya kufikishwa hospitali, hivyo kufanya idadi ya watu waliopoteza maisha katika ajali hiyo kufikia 19,” alifafanua Kyando.

Aidha, Kamanda Kyando alisema tayari maiti tisa zimeweza kutambuliwa na ndugu zao, baada ya kupata taarifa kupitia vyombo vya habari na kufika hospitalini.

Aliwataja marehemu tisa  waliotambuliwa kuwa ni dereva wa lori, Belege Mnubi (56), mkazi wa Dar es Salaam, Doris John (40), mkazi wa Iyunga, Sunday Mwakinyamile (44), mkazi wa Ilolo Mbeya na Andrew Medard (30), mkazi wa Mbalizi.

Wengine ni Georfrey Mwamakoba (30), Joseph Mbwana (34), Bakari Mwakala (23), Maneno Joseph (43), wote wakazi wa Jiji la Mbeya, pamoja na Joseph Mukirya ambaye ametambuliwa kama ni Mkazi wa Mkoa wa Tabora.

Mganga Mkuu wa Songwe, Dk. Kheri Kagya, amethibitisha kupokea miili 17 na kusema kuwa miili mingine ambayo ni dereva na mwanamke imehifadhiwa Hospitali ya Wilaya ya Mbeya Vijijini na kusema kuwa licha ya baadhi ya miili kutambuliwa, zoezi la utambuzi bado linaendelea.

Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Brigedia Nickodemas Mwangela, ambaye alishiriki zoezi la uokoaji, alisema miili ya baadhi ya watu hao ilikatika kutokana na ajali hiyo mbaya na kusema kuwa zoezi la utambuzi linaendelea.

ATOA POLE KWA KIGWANGALA

Wakati huo huo, Rais Magufuli ametoa mkono wa pole kwa familia ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla, ambaye amefiwa na mwanawe, Zul.

Rais Magufuli akiwa na Mkewe, Mama Janeth Magufuli, walifika nyumbani kwa familia hiyo Mikocheni, Jijini Dar es Salaam na kukutana na baadhi ya wanafamilia wakiongozwa na Mama wa Marehemu, Dk. Bayoum Kigwangalla, wakiwa katika maandalizi ya kusafirisha mwili wa marehemu kwenda Nzega, mkoani Tabora.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles