28.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 8, 2024

Contact us: [email protected]

JOHN MCCAIN: SHUJAA NA MUASI ALIYEACHA HISTORIA MAREKANI

JOSEPH HIZA NA MTANDAO             |             


AKITAJWA kuwa na moyo wa kijasiri, maadili, John McCain, anaelezwa kuwa mwanasiasa pekee anayeheshimika zaidi nchini Marekani mwenye ubavu wa kujibishana mfululizo na kumpa za uso mtu anayemhesabu kuwa mzandiki kupita wote duniani, Rais Donald Trump.

Neno shujaa, mpinzani na muwazi ndiyo yaliyotawala wakati vyombo vya habari na wanasiasa wakimwelezea Seneta huyo mkongwe zaidi Marekani aliyefariki Jumamosi iliyopita akiwa na umri wa miaka 81.

Maradhi ya saratani ya ubongo, yaliyogundulika wakati wa kiangazi mwaka jana, ndiyo yaliyokatisha uhai wa seneta huyo wa Jimbo la Arizona alilolishikilia kwa miongo mitatu.

Mwezi mmoja tu kabla ya Uchaguzi Mkuu wa Marekani mwaka 2008 katika moja ya matukio yasiyosahaulika yanayomtambulisha, mwanamke mmoja alisimana katika moja ya mikutano ya kampeni za urais wa Marekani.

Mwanamke huyo alimwambia McCain, aliyekuwa akigombea kupitia Chama chake cha Republican, wasiwasi wake mkubwa juu ya mpinzani wake katika kinyang’anyiro hicho cha kuelekea Ikulu ya Marekani, White House.

“Siwezi kumuamini (Barack) Obama. Nimesoma simulizi zinazomhusu, zikionesha si Mmarekani bali Mwarabu,” mwanamke huyo alisema akimzungumzia mgombea huyo wa Chama cha Democratic.

McCain alianza kutikisa kichwa chake na kabla hata mwanamke huyo hajamaliza swali lake, akachukua kipaza sauti, lugha ya mwili ikionesha wazi kutokubaliana wala kufurahishwa na kauli ya mwanamke huyo.

“Hapana, mama,” McCain alisema. “Obama ni mtu mzuri wa familia, raia mwema, ambaye mimi sikubaliani naye tu katika masuala ya kimsingi kisera na kisiasa. Hii ndiyo maana ya kampeni za kisiasa na si hii ya kukomalia dini na rangi ya mtu.”

Licha ya kauli yake ya kumtetea Obama kuitikiwa na zomea zomea kutoka sehemu ya wafuasi wake mkutanoni, McCain hakurudi nyuma bali ukawa mwanzo wa kuzidisha ukosoaji wa misimamo mingi ya chama chake hicho kwa kipindi chote kilichobakia cha maisha yake.

Mfungwa huyo wa zamani wa kivita nchini Vietnam, ni sababu kubwa ya kupungua kwa wahafidhina wenye misimamo mikali chamani mwake na kukifanya kujielekeza zaidi mrengo wa kulia.

Huyo ndiye McCain muwazi, mwadilifu na asiye na chembe za kibaguzi, aliye tayari kutofautiana na chama chake kiasi cha kuitwa muasi au mpinzani.

Alivuka ng’ambo kwenda kufanya kazi na wapinzani ila mradi tu wana mawazo sawa na anayoyaamini, anayoyasimamia na au kuyapigania ikiwamo kuunga mkono hadharani sera za Obama.

Ni tofauti na Donald Trump aliyepanda haraka kisiasa kwa misimamo ya kizalendo, kibaguzi na kauli gawanyishi, ikiwamo kampeni yake ya uongo kuwa Obama hakuwa raia wa Marekani na kuwa alifoji cheti chake cha kuzaliwa.

Trump akaenda kuwa rais akikumbatia siasa za mashambulizi, madongo na kauli tata zisizojali athari kwa taswira ya chama na taifa kiasi; McCain aliyelipenda taifa lake, hakuwa na hamu naye, chuki baina yao ikawa wazi kwa kila mtu.

Aliongoza kundi la wanachama maarufu wa Republican waliokuwa wakimshambulia vikali Trump na kuzidisha taswira ya mpinzani.

Tofauti za McCain na Trump zilizoshuhudia mikwaruzano ya mara kwa mara ziliashiria uwakilishi wa vizazi viwili tofauti katika siasa za Washington.

McCain aliwakilisha kizazi cha vigogo wa zamani wa siasa za Washington, simba wa Seneta, ambao waliendekeza heshima kwa pande zote na ambao waliamini heshima ni kila kitu.

Trump aliibua kizazi kipya, nyakati mpya za siasa zilizooza za Marekani, ambazo matusi, ubaguzi ni kawaida na neno samahani ni msamiati mgumu!.

John Sidney McCain III, amezaliwa katika kambi ya jeshi ya Coco Solo nchini Marekani, ambayo ilikuwa chini ya udhibiti wa Marekani, Agosti 29, 1936.

Ndiyo maana haikushangaza taaluma ya kijeshi kuwa ndani ya damu yake kwa sababu pia baba na babu yake wote walihudumu kama wanajeshi wakifikia nyadhifa za juu.

Alihitimu kutoka chuo cha jeshi la majini mwaka 1958 na alianza kazi ya urubani wa jeshi akiwa na umri wa miaka 22.

Akapelekwa vitani nchini Vietnam, ambako alinusurika kifo Julai 1967, wakati alipokuwa akijiandaa kwenda kufanya shambulio la anga, kombora liligonga matanki ya mafuta, hali iliyosababisha moto kwenye meli na watu 134 walipoteza maisha.

Miezi mitatu baadaye alitunguliwa kaskazini mwa Vietnam na hivyo akakamatwa na wapiganaji wa Vietnam, alikataa kuachiwa mapema.

Badala yake, alishikiliwa kama mfungwa wa kivita kwa zaidi ya miaka mitano, mahali alikokuwa akipigwa mara kwa mara na kuteswa hali iliyosababisha matatizo katika mikono yake.

Baada ya kurejea Marekani aliendelea kutumikia jeshi, hatimaye akawa mwambata wa jeshi la majini kwenye baraza la Seneti hadi alipostaafu mwaka 1981.

Na kama ilivyokuwa kwa baba na babu yake kabla yake, ambao wote walikuwa maadmiral wa jeshi wenye nyota nne kwa jina la John McCain, ametumia maisha yake yote katika utumishi wa nchi: Kwanza kama rubani wa ndege ya jeshi la majini, kisha kama seneta hadi alipofariki dunia.

Yeye pia angekuwa Admiral, iwapo kombora la kudungulia ndege la uliokuwa Muungano wa Kisovieti (USSR) halingekatisha kazi yake jeshini Oktoba 26, 1967.

Siku hiyo akiwa kwenye operesheni yake ya 23 katika anga ya Vietnam, ndege yake chapa A-4 Skyhawk ilishambuliwa wakati ikiwa katika anga ya Jiji la Hanoi.

McCain aliruka kwenye ndege hiyo kwa kutumia parachuti na kuangukia katika ziwa dogo katikati mwa mji, ambako nusura achomwe moto na kundi la watu waliokuwa na hasira. Mikono yake miwili na goti vilivunjwa vibaya.

Baba yake akiwa kamanda wa vikosi vyote vya Marekani katika kanda ya Pacific, McCain aliendelea kuwa mfungwa wa kivita kwa zaidi ya miaka mitano.

Aliachiwa mwaka 1973 baada ya makubaliano ya amani ya Paris, lakini madhara ya kimwili yaliyotokana na matibabu yasiyoridhisha ya makusudi ya viungo vyake vilivyovunjika  na mateso gerezani vilimgharimu kazi yake ya urubani.

“Kwa sababu fulani, haukuwa muda wangu wakati huo na ninaamini kwa sababu hiyo, nilikuwa nimepangiwa kufanya jambo lingine,” alisema katika mahojiano mwaka 1989.

Jambo hilo, lilidhihirika wazi, lingekuwa siasa. Baada ya kuhudumu miaka michache kama kiungo wa jeshi la majini wa Baraza la Seneti, McCain alihamia Arizona, jimbo la nyumbani kwa mke wake wa pili na kushinda kiti katika baraza la wawakilishi mwaka 1982.

Sifa zake zilikuwa haraha, haikuchukua muda akapanda ngazi kuingia Baraza la Seneti, ambalo ndilo chombo chenye nguvu zaidi kisiasa nchini Marekani.

Likageuka makazi yake ya pili kwa miaka 30 na kujipatia heshima kubwa.

Kuhusu taswira ya mpinzani ndani ya chama cha Republican, imetokana na kukaidi kwake misimamo ya chama kuhusu masuala kuanzia mageuzi ya ufadhili wa kampeni hadi kwenye uhamiaji.

Hakujali sana nidhamu ya chama, mtazamo uliochochewa na matukio ya nyuma ya uasi katika maisha yake, kama mwanafunzi mtukutu katika chuo cha jeshi la majini la Marekani, au mfungwa jeuri aliyekuwa akiwachokoza wafungaji wake nchini Vietnam.

“Kunusurika kifungo changu kuliimarisha kujiamini kwangu na kukataa kwangu kuachiwa mapema kulinifundisha kuamini katika maamuzi yangu,” McCain aliandika katika kitabu cha maisha yake mwaka 1999, “Faith of My Fathers.”

Ni McCain huyu mwenye matata, asiyedhibitika, mwenye kudharau mamlaka na wakati mwingine mwenye majigambo, aliyejitosa kwenye kinyang’anyiro cha urais mwaka 2000.

McCain alishindwa na George W. Bush katika kura ya uamuzi ya uteuzi wa mgombea urais wa Republican, lakini alijiimarisha na hatimaye kushinda kinyanganyiro kilichofuata cha kuwania urais Republican katika jaribio la kumrithi Bush aliyepoteza umaarufu mwaka 2008.

Baada ya chama hicho kumpitisha, akiwa anaikaribia Ikulu ya White House, alifanya uamuzi wenye utata mkubwa.

Wengi wa washirika wake hawakumsamehe kwa kumteua kama mgombea wake mwenza, Gavana wa Alaska asiye na uzoefu wowote Sarah Palin.

Palin hakuonekana kamwe kuendana na McCain, alionesha uzoefu mdogo, kazi yake kubwa wakati wa kampeni ilikuwa porojo na mashambulizi dhidi ya Obama na wengineo.

Palin akawa chimbuko la kuibuka kwa wagombea wa kariba ya Trump na haikuwa ajabu Gavana huyo wa zamani wa Alaska kumpitisha mfanyabiashara huyo bilionea wakati wa uchaguzi wa mwaka 2016.

Katika uchaguzi huo wa 2008, mgombea urais wa Chama cha Democrat, Barack Obama alishinda kwa urahisi

McCain, akiwa sasa ameshindwa mara mbili, aligeukia utani kuhusu namna alivyoanza kulala kama mtoto: “Lala masaa mawili, amka na kulia, lala masaa mawili, amka na kulala.”

Lakini licha ya kutokazia mashamulizi binafsi McCain hakuwa mtu wa vinyongo kwani watu wote waliomshinda kutimiza ndoto yake ya kuingia Ikulu, Bush na Obama kabla ya kifo chake aliwateua kuwa wasomaji wakuu wa kumbukumbu yake wakati wa mazishi yake.

Wakati akiwateua wapinzani wake hao wa zamani katika kinyanganyiro cha urais Mei mwaka huu kusoma kumbukumbu yake, McCain alimfungia vioo Trump, akimpiga marufuku kuhudhuria au kukaribia jeneza lake, badala yake akimtaka Makamu Rais Mike Pence.

Alikuwa na uwezo wa kuiburudisha hadhira yake. Mjini Washington, alikuwa akizungukwa na waandishi  wa habari katika kumbi za Bunge wakati mwingine akitumia nguvu na kukosa uvumilivu.

“Hilo ni swali la kijinga,” aliwahi kusikika akimwambia mwanahabari mmoja.

Lakini wakati mwingine majibu yake ya haraka yalikuwa yakigeuka kuwa unyenyekevu: “Sidhani mimi ni mtu mwenye akili sana,” alisema wakati mmoja. Wakati mwingine alikuwa akiripuka pia, hasa kuhusu mambo yenye umuhimu kwake: Vikosi vya jeshi, upekee wa Marekani na, katika miaka yake ya baadaye, kitisho kinachotoka kwa Rais wa Urusi Vladmir Putin, aliyemtaja kuwa ‘muuaji na jambazi.’

Wakati mwingine wenzake katika chama cha Republican walikuwa wakikejeli misimamo yake ya uingiliaji pasipo na kufikiri, wakibainisha kwamba hangeweza kusema ‘hapana’ kwa vita.

Wakati mmoja alitumia mdundo wa Beach Boys wakati akiimba kuhusu uwezekano wa ‘kuishambulia Iran kwa mabomu.’

Kwa lengo hilo, McCain aliendelea kushawishika kwamba maadili ya Marekani yanapaswa kuzingatiwa na kutetewa duniani kote.

Alikuwa akipanda ndege mara kwa mara kwenda Baghdad, Kabul, Taipei au Kiev, akipokelewa zaidi kama mkuu wa nchi kuliko Seneta.

Baada ya kuitwaa rasi ya Crimea, Urusi iliorodhesha jina lake kwenye orodha ya watu wabaya na kujibu vikwazo vilivyoongozwa na Marekani.

“Nadhani hii inamaanisha kuwa mapumziko yangu ya Siberia (Urusi) msimu wa machipuko yamefutwa,” alijibu alipoulizwa swali kuhusu kuwekewa vikwazo.

Kuhusu Urusi au Syria, sauti ya McCain ilifika mbali, lakini kiuhalisia Seneta huyo alikuwa jenerali asiye na majeshi.

Kuchaguliwa kwa Trump kulionekana kuvuruga mapambano na mawazo ya veterani huyo wa Republican, ambaye alikerwa na siasa za kizalendo na sera ya kujilinda ya mfanyabiashara huyo tajiri na kujikomba kwake kwa Putin na ‘kuua heshima ya ofisi ya rais.’

Lakini yote hayo hayakumfanya McCain kustaafu siasa kwa furaha.

Yumkini akimfikiria babu yake, aliyefariki siku chache tu baada ya kurejea nyumbani kufuatia kusalimu kwa Japan katika vita kuu vya pili vya dunia, McCain alitaka kusalia katika Seneti kwa kadiri awezavyo, hata wakati akikabiliwa na saratani kali ya ubongo.

Tangu Desemba 2017, hakuwa anahudhuria katika katika Baraza la Seneti wakati akipatiwa matibabu jimboni Arizona na aliwapokea kwenye shamba lake kubwa marafiki na wenzake waliokuja kumuaga mbali na vyombo vya habari.

Siku moja kabla ya kifo chake, familia yake ilitangaza kuwa alikuwa anasitisha matibabu.

McCain ameacha mke Cindy na watoto saba, watatu kati yao kutoka kwenye ndoa yake ya mwanzo. Pia bado yu hai mama yake Roberta McCain (106).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles