NA MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM
WASANII wa muziki wa kizazi kipya, Joh Makini na Abdulaziz Chende ‘Dogo Janja’, wanatarajiwa kutoa burudani katika mbio za Kilimanjaro Marathon 2017, Jumapili hii mjini Moshi.
Akizungumza jijini Moshi jana, Meneja wa Bia ya Kilimanjaro Premium Lager, Pamela Kikuli, aliwataka wakazi mkoani hapa kujitokeza kwa wingi katika mbio hizo ambazo ni kubwa Tanzania.
“Wasanii hawa wanakubalika Moshi, tuna uhakika mashabiki watajitokeza kwa wingi kuangalia mbio na kupata burudani,” alisema Pamela.
Upande wake Joh Makini alisema amejiandaa vizuri kukonga nyoyo za mashabiki wake na kuwataka wakazi wa Moshi kujitokeza kwa wingi kushuhudia burudani iliyoandaliwa.
Naye Dogo Janja alisema anafarijika kupata nafasi hiyo, kwani mkoa huo ni miongoni mwa mikoa yenye mwamko mkubwa wa mashabiki.
Usajili mjini Moshi ulianza kufanyika jana, huku wakazi mbalimbali wakiwa wamejitokeza kujiandikisha kushiriki mbio hizo.