Na GUSTAF HAULE-Kibaha
RAIS mstaafu, Jakaya Kikwete, amewataka wamiliki wa viwanda kuacha kuwakandamiza wakulima kwa kununua mananasi yaliyomo shambani kwa bei ya chini.
Kikwete ambaye pia ni mkulima wa zao hilo, alitoa kauli hiyo juzi katika shamba lake lililopo Kiwangwa wilayani Bagamoyo.
Alisema licha ya viwanda kusaidia kupatikana masoko ya ndani, vimekuwa havina uwiano wa gharama zinazolingana na maumivu anayoyapata mkulima.
Alisema wakati mwingine imekuwapo changamoto ya kushuka soko hali inayokuwa ikisababisha wakulima kupata hasara kwa matunda kuoza yakiwa mashambani .
Akitoa taarifa ya shamba lake la mananasi wakati msafara wa Mwenge wa Uhuru ulipotembelea shamba hilo, Kikwete alisema kilimo cha matunda kina tija endapo kitalimwa kisasa na kupata soko la uhakika.
“Wakati utafika watakosa matunda kutokana na gharama yao hailipi, wakulima wa matunda tutashindwa kukubali kuuza kwa bei ya chini ambayo hailipi,” alisema Kikwete.
Alimweleza kiongozi wa mbio hizo, Amour Hamad Amor kuwa mananasi huvunwa baada ya miezi 18 tangu kupandwa.
“Bei ya mauzo hutegemea wanunuzi na wachuuzi wadogo ambao hununua kwa ukubwa wa nanasi kutoka Sh 400 hadi Sh 800 linapovunwa shambani,” alisema.
Shamba la kiongozi huyo lina ukubwa wa ekari 200, kati ya hizo 64 zimelimwa na zipo hatua ya kupaliliwa.