Na ELIYA MBONEA -ARUSHA
KAMA si mbwa ambao walipiga kelele na kuanza kupambana na watu wasiojulikana, waliovamia nyumbani kwa Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari (Chadema) usiku wa kuamkia jana, huenda mwanasiasa huyo kijana leo hii asingekuwa hai.
Juzi saa 5:30 usiku, muda mfupi tu baada ya Nassari kurejea nyumbani kwake akitokea kwenye kongamano la vijana wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, watu hao wasiojulikana walivamia nyumbani kwake, katika Kijiji cha Nkwanenkori wilayani Arumeru.
Wakiwa katika nyumba hiyo, walimuua mbwa wake aliyekuwa akijaribu kuwazuia wasifanye kazi yao waliyokusudia na kisha kufyatua ovyo risasi zaidi ya 13.
SIMULIZI YA TUKIO
Akizungumza na MTANZANIA Jumapili lililofika nyumbani kwake jana baada ya kupata taarifa za kuvamiwa, Nassari kwa maneno yake mwenyewe alisema kama si mbwa huyo kupambana na watu hao nje, wangemtoa uhai akiwa ndani.
“Kawaida yangu kabla sijafika nyumbani huwa napiga simu kwa vijana
ninaoishi nao wanifungilie geti. Nilipoingia ndani nikiwa sebuleni kabla sijalala, nilisikia mbwa wanapambana nje.
“Ghafla nikasikia risasi zimeanza kulia, zilipigwa risasi zaidi ya 13, nililazimika kukimbia chumbani kuchukua bunduki yangu aina ya Riffle ili kujihami,” alisema Nassari ambaye nyumba yake licha ya kuzungukwa na miti ina uzio mrefu na imefungwa vifaa vya kiusalama (Security system).
Alisema baada ya kuchukua bunduki yake, alifungua mlango wa nyuma na kisha kwenda kujibanza pembeni ya ukuta na kuanza kufyatua risasi.
“Nilifungua mlango wa nyuma, sikujua walikuwa wanafyatua kutokea upande gani,
nilijivuta hadi pembeni ya ukuta nikajibanza, nikaanza kufyatua, nilifyatua hewani risasi kama sita wakati wao wakifyatua zaidi ya 13,” alisema.
Kwa mujibu wa maelezo yake baada ya kufyatua risasi, ghafla kimya kilitanda hali iliyoashiria watu hao wameondoka.
“Niliwafuata vijana wawili ninaoishi nao hapa nyumbani na tukaanza kuwaita mbwa kwa alama tunazozitumia, lakini hawakuonekana, baadaye tulimkuta mbwa mmoja kati ya wawili amekufa baada ya kupigwa risasi ya ubavuni upande wa kulia na kutokea kushoto,” alisema.
Inaelezwa kuwa mbwa mwingine ambaye alikimbia, alikuja kuonekana baadaye baada ya utulivu kurejea.
Nassari alisema baada ya hapo muda kama wa saa sita usiku alimtafuta kwa simu Mkuu wa Polisi Wilaya ya Arumeru, Jumanne Mkwama, lakini hakuweza kumpata kutokana na simu zote kutopatikana.
“Nilimwandikia ujumbe mfupi kumjulisha tukio lililonipata, baadaye nikawajulisha viongozi wangu wa chama usiku ule ule, wakanishauri nisiende polisi usiku ule badala yake niende asubuhi.
“Sikulala hapa kwa sababu mke wangu amesafiri, nilitafuta mahali pengine pa kulala. Nyuma ya ukuta walipotumia kuruka tumeokota risasi za moto tatu,” alisema.
Kuhusu waliohusika katika tukio hilo, Nassari alisema ni vigumu kwake kubashiri, lakini ukweli ni kwamba amekuwa akipokea vitisho vingi katika siku za hivi karibuni.
“Ni ngumu kusema nani anahusika na tukio hili. Lakini mimi ni mwanasiasa, hivi karibuni kumekuwa na vitisho vingi dhidi yangu, hapa nyumbani sina mali za kuibiwa.
“Mimi ni mwanasiasa, nimemaliza chuo nikapata bahati ya kuchaguliwa kuwa mbunge. Kwahiyo sijui, nadhani ni mambo ya kisiasa, mmeona wenyewe kilichotokea uchaguzi wa madiwani,” alisema Nassari.
Alisema huko nyuma pia aliwahi kulalamika kutishiwa maisha baada tu ya kuweka ushahidi wa viongozi wateule wa rais kujihusisha na rushwa kwa kununua wanasiasa wa upinzani.
“Kwenye kikao cha Kamati ya Utendaji ya Wilaya Chadema, kiongozi mmoja anasema alipewa taarifa na mmoja wa viongozi wa CCM Kata ya Maroroni, kwamba waliandaa jeneza la Nassari kwenye uchaguzi wa madiwani.
“Taarifa hizi nimezipata jana na leo nimevamiwa. Sijui, ngoja tuone polisi kama watapata au kusema wanachokichunguza. Mimi ni mwasiasa, kwenye siasa kuna marafiki na maadui, huwezi kujua,” alisema.
Nassari na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema), hivi karibuni walizua mjadala mkali ambao watu wengi wanasubiri kujua hatma yake, baada ya kuwatuhumu madiwani wao watano kununuliwa na ushahidi wa hilo kuufikisha Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).
Hadi sasa, Takururu haijawahi kueleza chochote ulipofikia uchunguzi juu ya ushahidi huo waliokabidhiwa na wabunge hao.
MASHUHUDA, MAJIRANI
MTANZANIA Jumapili lilizugumza na Hamis Peter (20) ambaye ni mmoja wa watu wanaoishi kwa Nassari na alikuwapo wakati wa tukio hilo.
Peter alisema alipigiwa simu na Nassari kufungua geti na alifanya hivyo na mbunge huyo kuingia ndani kwa wakati.
“Baada ya kuingia ndani tuliagana, sie tunalala nyumba nyingine ipo kwa chini, tukiwa ndani baada ya nusu saa tulianza kusikia milio ya risasi na hatukuweza kutoka kwa sababu hatukujua waliokuwa wakipiga walikuwa wapi,” alisema Peter.
Shuhuda mwingine, Ombeni Elisante, anayeishi jirani na Nassari, alikiri kusikia milio ya risasi usiku huo, lakini pia alisema hakuweza kutoka nje.
Kwa upande wake, Kaimu Katibu wa Chadema Mkoa wa Arusha, Elisa Mungure, akizungumza nyumbani kwa Nassari jana, alisema wahalifu hao hawakuwa wamepanga kwenda kuiba vitu.
“Uvamizi uliotokea hapa si wa kuiba gari wala vitu vya ndani, bali walifuata roho ya Nassari kwa sababu ya masuala ya kisiasa,” alisema Mungure.
POLISI WACHUNGUZA
Akizungumza na MTANZANIA Jumapili, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo, alikiri kupokea taarifa za tukio hilo.
“Taarifa hizo nimezipata, nimetuma timu ya kuchunguza. Lakini ni kweli kuna mbwa wake amepigwa risasi na kufa, tunaendelea na uchunguzi wa tukio hili,” alisema Kamanda Mkumbo ambaye hakutaka kuzungumza zaidi kwa kile alichosema kuwa tayari wapo kwenye uchunguzi.
MTANZANIA Jumapili lilishuhudia timu ya wataalamu wa Jeshi la Polisi yenye takribani watu saba ikifika nyumbani kwa Nassari saa 5:00 asubuhi wakiwa wameongozana na mbunge huyo na Mbunge wa Arusha Mjini, Lema.
Mara baada ya kuwasili nyumbani kwa Nassari, askari hao waliovalia kiraia, walianza kufanya uchunguzi wa eneo alipopigiwa mbwa risasi.
Baada ya kufuatilia damu ya mbwa, askari hao walizunguka nje ya ukuta ambako wahalifu hao waliutumia kupandia na kufanikiwa kuingia ndani na katika maeneo hayo yote walichukua vipimo vya vidole na kupiga picha.
Lema alionekana kufuatilia kila hatua iliyokuwa ikifanyika.
Askari hao pia walichukua maelezo kutoka kwa vijana wanaoishi na Nassari.
Mbali ya maelezo, walichukua pia risasi tatu zilizookotwa kwenye eneo la tukio.
MATUKIO YA KUVAMIWA
Tukio la Nassari kuvamiwa nyumbani kwake limekuja wakati mbunge mwingine wa Chadema, Tundu Lissu (Singida Mashariki), akielekea kutimiza miezi mitatu kitandani akiuguza majeraha yaliyotokana na kushambuliwa kwa risasi na watu ambao hadi sasa Jeshi la Polisi limeshindwa kuwabaini.
Lissu alivamiwa nyumbani kwake saa saba mchana wakati akijiandaa kushuka katika gari lake na kisha kumiminiwa risasi zaidi ya 30.
Watu hao ambao inaelezwa walikuwa katika gari aina ya Nissan Patrol lenye rangi nyeupe, walitokomea kusikojulikana baada ya kutekeleza kitendo hicho.
Matukio hayo pamoja na yale yenye mwelekeo unaofanana na huo, si ya kwanza kutokea nchini na mara zote Jeshi la Polisi limekuwa likisema linaendelea na uchunguzi na kwamba si ajabu kuchukua muda mfupi au mrefu kuukamilisha.