23 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

SHEIN: CCM INAFANYA MAGEUZI YA ITIKADI, SERA

NA MWANDISHI WETU – ZANZIBAR

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, Rais Dk. Ali Mohamed Shein, amesema chama hicho kina uzoefu mkubwa wa kufanya mageuzi ya kifikra, itikadi, sera na mabadiliko mengine ya kimaendeleo kwa kufuata matakwa ya wananchi bila ya kuathiri misingi imara iliyoachwa na waasisi wa taifa hili.

Kauli hiyo aliitoa mjini hapa jana katika Mkutano Mkuu wa CCM Mkoa wa Kusini Unguja, ambao pia ulichagua viongozi wa mkoa huo kichama.

Mkutano huo uliofanyika katika Ukumbi wa Hoteli ya Coconut, Marumbi, Wilaya ya Kati, Mkoa wa Kusini Unguja, ulihudhuriwa pia na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.

Dk. Shein ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar, alisema CCM si cha mtu mmoja kama ilivyo vyama vingine vya siasa vinavyoendelea kupoteza mwelekeo na kusambaratika kwa kukosa uzoefu wa historia kama ilivyo kwa chama hicho.

Alisema ni vyema kwa wajumbe wa mkutano huo wakatambua hivyo na wakahakikisha kwamba viongozi watakaowachagua wanaielewa itikadi ya chama hicho na sera zake na wapo tayari kuzilinda, kuzisimamia na kuzitekeleza kwa vitendo.

“Viongozi watakaochaguliwa watalazimika kuwa tayari kuwakemea na kupambana na wazembe, wababaishaji, wabinafsi na wote wenye tabia ya kufanya kazi kwa mazoea,” alisema.

Aliwataka viongozi watakaochaguliwa kuwa makini kama ilivyo kawaida kwa viongozi wa CCM katika uchaguzi wa viongozi na kukemea maovu.

“Chama chetu kinapendwa, kinawavutia wananchi na kina uwezo mkubwa na wa peke yake wa kurejesha na kujenga matumaini mapya kwa wanachama wake na wananchi wote, hivyo hapana shaka tuna nafasi nzuri ya kuendelea kushika dola kwa pande zote mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” alisema.

Pia alisema ushindi wa kishindo ambao CCM imeupata katika uchaguzi mdogo wa madiwani uliofanyika wiki iliyopita katika kata 43 zilizoko mikoa 19 ya Tanzania Bara, ni kiashiria kwamba chama hicho kilipitisha viongozi wenye sifa, uwezo, nia njema na waliokubalika kwa wananchi.

“Ushindi mkubwa uliopatikana hata katika maeneo ambayo wapinzani walidhani kwamba ni ngome zao, ni uthibitisho wa kuwa wananchi wanaendelea kukiamini na kuipenda CCM na maendeleo ya dhati ya nchi yamo ndani ya CCM,” alisema.

Naye, Samia, alitoa salamu za Rais Dk. John Magufuli na kusisitiza haja kwa wajumbe wa mkutano huo kuwachagua viongozi watakaokiimarisha zaidi chama hicho ili kiendelee kupata ushindi katika uchaguzi ujao.

Awali, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dk. Juma Abdalla Mabodi, alielezea mchakato wa uchaguzi ulivyoanza toka ngazi ya shina na alisema chama kimekuwa imara na viongozi waliochaguliwa na watakaochaguliwa katika mkutano huo ni weledi na watakipeleka chama hicho katika ushindi mkubwa uchaguzi wa mwaka 2020.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles