24.8 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

KIPYENGA CHAPULIZWA MAJIMBO YA NYALANDU, GAMA, NANGOLE

Na MWANDISHI WETU – Dar es Salaam

TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetangaza kuwa uchaguzi mdogo katika majimbo matatu ya Singida Kaskazini, Longido na Songea Mjini na kata sita za Tanzania Bara, utafanyika Januari 13, mwakani.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari Dar es Salaam jana, Makamu Mwenyekiti wa NEC, Jaji mstaafu Hamid Mahmoud Hamid, alisema uchaguzi wa majimbo hayo ameutangaza baada ya kupokea barua kutoka kwa Spika wa Bunge, Job Ndugai, kuhusu kuwapo nafasi zilizo wazi.

Alisema Jimbo la Singida Kaskazini liko wazi baada ya aliyekuwa mbunge wake, Lazaro Nyalandu, kuvuliwa uanachama wa CCM na hivyo kukosa sifa.

Jaji Hamid alisema kuwa NEC ilipokea barua kutoka kwa Spika wa Bunge, ambaye kwa kuzingatia kifungu cha 37(3) cha sheria ya Taifa ya Uchaguzi, sura ya 343, aliitaarifu tume uwepo wa nafasi wazi ya Jimbo la Uchaguzi la Singida Kaskazini mkoani Singida kuanzia Oktoba 30, mwaka huu.

Alisema kwa upande wa Jimbo la Songea Mjini, Ndugai aliitaarifu NEC kuwapo nafasi wazi baada ya kifo cha aliyekuwa mbunge wake, Leonidas Gama.

Pia alisema walipokea hati ya Mahakama Kuu, Kanda ya Arusha ikithibitisha kuwa Jimbo la Longido liko wazi baada ya kufutwa matokeo ya uchaguzi yaliyompa ushindi Onesmo ole Nangole.

Akizungumzia kuhusu uchaguzi wa kata sita zilizoko Tanzania Bara, alisema Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Selemani Jafo, akitumia masharti ya kifungu cha 13(1) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, sura ya 292, aliitaarifu NEC juu ya kuwapo nafasi zilizo wazi za madiwani.

Jaji Hamid alizitaja kata zinazohusika katika uchaguzi huo kuwa ni Kimandolu (Halmashauri ya Jiji la Arusha), Kihesa (Halmashauri ya Manispaa ya Iringa), Bukumbi (Halmashauri ya Wilaya ya Uyui), Kurui (Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe), Keza (Halmashauri ya Wilaya ya Ngara) na Kwagunda (Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe).

Alisema utoaji wa fomu za uteuzi katika majimbo hayo na kata hizo utakuwa Desemba 12 hadi 18, huku katika Jimbo la Songea Mjini ukiwa ni Desemba 14 hadi 20.

“Uteuzi wa wagombea katika majimbo ya Singida Kaskazini na Longido na kata za Keza, Kimandolu, Kwagunda, Bukumbi, Kurui na Kihesa, utafanyika Desemba 18, mwaka huu na uteuzi wa wagombea katika Jimbo la Songea Mjini utafanyika  Desemba 20, mwaka huu,” alisema.

Jaji Hamid alisema kampeni za uchaguzi huo katika majimbo ya Singida Kaskazini na Longido na kata zote sita, zitaanza Desemba 19, na kumalizika Januari 12, mwakani.

Katika Jimbo la Songea Mjini, alisema kampeni zitaanza Desemba 21, na kumalizika Januari 12, mwakani.

Alisema majimbo yote na kata zote sita uchaguzi wake utafanyika Januari 13, mwakani na alivikumbusha vyama vya siasa na wadau wote wa uchaguzi kuzingatia sheria, kanuni, taratibu, miongozo na maelekezo yote wakati wa kipindi cha uchaguzi huo mdogo.

Wiki iliyopita, ulifanyika uchaguzi mdogo katika kata 43 na CCM ilivigaragaza vyama vya upinzani kwa kushinda kata 42.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles