24.2 C
Dar es Salaam
Monday, May 27, 2024

Contact us: [email protected]

HISIA ZAKO ZISIKUONGOZE VIBAYA!

NA JOSEPH SHALUWA

UNAWEZA kuwa na hisia nzuri au mbaya, unaweza kuhisi kumpenda mtu, kumchukia au kuhisia amekufanyia kitu kibaya! Vyovyote inavyokuwa, ila zote ni hisia.

Katika mapenzi, unaweza kuhisi kumpenda sana mtu, ukajitahidi kuonyesha kila aina ya unavyompenda, lakini ama akuonyeshe kukupenda huku moyoni akiwa hana mapenzi na wewe au akukatae kabisa!

Lakini kubwa ambalo nalizungumzia leo, ni pale unapokuwa na mpenzi wako, ukahisi anakusaliti, haonyeshi mapenzi ya kweli au yupo kati kwa kati, yaani haeleweki! Hali hii inapotokea inaweza kukuchanganya na kukukosesha amani moyoni mwako ukiwa hufahamu kama uliye naye anakupenda au anakulaghai.

Hizo tunaziita hisia tata! Sasa unafanya nini baada ya kuwa na hisia hizo? Unaachana na mpenzi wako moja kwa moja au unazungumza naye? Na kama unazungumza naye, unamwambiaje? Hapa panaweza kuibuka maswali mengi sana kichwani mwako.

Kimsingi linapokuja suala la hisia kwamba mwandani wako, inawezekana hakupendi basi ni lazima uwe makini sana na ikiwezekana utumie kila njia ili uweze kuujua ukweli kuliko kusumbuliwa na hisia tu moyoni mwako.

Vipengele vifuatavyo vitakusaidia kuchunguza kama mpenzi wako anakupenda kwa mapenzi ya dhati au anapumzika kwa muda tu! Jipe wiki moja ya kugundua hilo – yes siku saba. Twende tukaone.

ONYESHA KUMPENDA

Hii ni hatua ya kwanza kabisa, katika kudhibitisha hisia zako. Unahitaji kujua kama anakupenda, kwa maana hiyo anza wewe kuonyesha unavyompenda! Inaweza kukusaidia, maana kama hakupendi, kuonyesha kwako kumpenda itakuwa kero kwake.

Kuwa kiongozi siku yake nzima, mfanyie manjonjo yote unayoyajua. Lengo hapo ni kumuweka sawa! Kwa kufanya hivyo, hata kama alikuwa na mpango wa kukutana na patina mwingine, nafsi humsuta, maana kila baada ya muda mfupi, simu yake huingiza sms kutoka kwako.

Meseji ambazo bila shaka zitakuwa na ujumbe wa mapenzi, kutokana na hilo, sio rahisi kuingiwa na hisia za kufanya kitu kibaya, vinginevyo atakuwa hakupendi!

Lazima utambue kitu kimoja muhimu katika hili, unapaswa kufanya haya yote, bila kujali kuwa anaonyesha kukupenda au hapana! Jitahidi kumpigia simu angalau mara tano au zaidi kwa siku na kumtumia sms kumi au zaidi kwa siku, bila kusahau kuwa unapaswa kumtumia waraka pepe mara moja au zaidi kwa siku!

Ninachomaanisha hapa  ni kumuweka karibuni. Zoezi hilo hufanyika kwa siku tatu tu!

MTEGE

Baada ya kuona mambo ya msingi ya kuzingatia katika siku tatu za mwanzo, sasa tugeukie katika siku tatu zingine. Kumbuka kuwa katika siku tatu hizo, utakuwa umesaliwa na siku moja ya mwisho!

Katika muda huu wa siku tatu, unapaswa kumwekea mitego! Hapa namaanisha mitego ya kimapenzi. Kumbuka kuwa kwa siku tatu za mwanzo umeshamsogeza karibu yako, hafurukuti kwa lolote, umemfanya aishi unavyotaka wewe, ni kama hawezi kufanya kitu chochote kabla hujampa maelekezo, sasa mtege!

Usifanye kitu chochote kwa nia ya kumwonyesha mapenzi, bali kaa kimya! Katika siku hizi tatu, hutakiwi kumwandikia sms, waraka pepe wala kumpigia simu, acha yeye afanye akutumie. Kimsingi ni kwamba hupaswi kufanya mawasiliano ya aina yoyote na yeye.

Kumbuka kuwa umeshamfanya aishi unavyotaka, sasa atakapoona anakosa text sms, whatsapp au kwenye mtandao wowote wa kijamii kutoka kwako, ni hapo sasa atakapoamua kukutafuta.

Hata akikutumia sms usijibu! Akikuandikia waraka pepe hivyo hivyo, ila akipiga simu pokea lakini epuka neno dear, sweet, mpenzi na majina mengine yatakayoonesha lugha ya mapenzi.

Ni jambo litakalomshangaza sana na kama  akihitaji mkutane pamoja kubali.

JE, HISIA ZAKO ZINA UKWELI?

Hapa sasa ni wakati wako wa kuangalia kama hisia zako zilikuwa sawa au vinginevyo.  Baada ya kuchunguza hisia hizo kwa siku sita zilizopita, sasa unatakiwa kuhakiki hisia zako.

Hapa  unatakiwa kuangalia kama kuna ukweli wowote juu ya penzi lako kwa huyo anayeutesa moyo wako. Kwa mambo uliyomfanyia katika siku tatu za mwanzo, lazima atahisi kuna matatizo katika siku tatu zinazofuata.

Kama anakupenda, atakutafuta na wakati mwingine atahitaji mkutane kwa ajili ya mazungumzo faragha, hapo sasa ndipo atakapokueleza ukweli wa penzi lake, lakini kama hakupendi, hatashtuka na atakuacha, kwa sababu sms, waraka pepe na simu zako zilikuwa zinachukiza!

Jiulize, kama ulikuwa unamkera, kuna sababu gani ya kuwa na mtu ambaye hana mapenzi ya dhati kwako? Hapo ni mwanzo wa utumwa ambao mwisho wake ni mbaya.

Lengo ni kuangalia kama hisia zako zilikuwa zikikutuma sawa, baada ya kupata jibu ni wakati wako wa kuamua kunyoa au kusuka!

Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Saikolojia ya Uhusiano. Ameandikia vitabu vingi vikiwemo True Love, Let’s Talk About Love na Maisha ya Ndoa. Kwa sasa anaandaa kitabu chake kipya cha SIRI ZA NDOA YENYE FURAHA kitakachotoka hivi karibuni.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles