26.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 20, 2024

Contact us: [email protected]

JEAN-CLAUDE ‘BABY DOC’ DUVALIER: Rais mdogo kuwahi kutokea duniani

JOSEPH HIZA NA MASHIRIKA

NI mmoja wa madikteta hatari kabisa wa karne ya 20, akiwa ameutumikia urais wa Haiti kuanzia mwaka 1971 hadi 1986 kufuatia kifo cha baba yake, aliyeitawala nchi hiyo kwa mkono wa chuma.

Lakini pia ameweka rekodi ambayo hadi sasa haijavunjwa ya kuwa rais mdogo kabisa kuwahi kutokea duniani; aliingia madarakani akiwa na umri wa miaka 19 tu.

Anayezungumzwa hapa si mwingine zaidi ya Jean-Claude “Baby Doc” Duvalier, dikteta asiyesahaulika katika taifa hilo masikini Amerika ya Kusini.

Alifariki dunia mwaka 2014 kwa shambulio la moyo akiwa na umri wa miaka 63 wakati kesi kadhaa za uchafu na unyama aliotenda wakati wa utawala wake zikiwa hazijakamilika.

Akiwa ameikimbia nchi mwaka 1986, Jean-Claude Duva­lier alirudi Haiti Januari 16, 2010, akitumia uwapo wa ombwe la uongozi na janga la kibinadamu lililotokana na tetemeko kubwa la ardhi lililoua watu 316,000 na wengine milioni kukosa makazi.

Lakini haikuchukua muda akaanza kuandamwa na polisi ili ashitakiwe kwa uhalifu wa kifedha na kisiasa.

Januari 18, 2011, alikamatwa na kushitakiwa kwa mashitaka ya rushwa, wizi na matumizi mabaya ya fedha wakati wa utawala wake wa miaka 15.

Aliachiwa lakini kwa masharti ikiwamo kuwa wakati wowote kuitikia wito wa kumwita mahakamani.

Baadaye ikaja hatua ya jaji wa Haiti kutoa uamuzi kuwa Baby Doc atakabiliwa na mashitaka ya rushwa, si mauaji, kutoweka kwa wapinzani, mateso na ukiukaji mwingine wa haki za binadamu alioufanya wakati wa utawala wake, iliwaudhi wengi.

Uamuzi huo ulitolewa kwa kile kilichodaiwa kuwa muda umepita kumshitaki kwa mashitaka aina hiyo.

“Bila uamuzi huu kubatilishwa na rufaa, itakuwa uthibitisho mwingine kwa watu wa Haiti kuwa mfumo wa sheria daima uko upande wa matajiri na watu wenye nguvu na ushawishi na hauwezi hata kuadhibu kwa uhalifu mbaya,” alisema Reed Brody wa Shirika la Haki za Binadamu (HRW).

“Kwa Jean-Claude Duvalier kurudi Haiti bila kushitakiwa ni kofi kwa maelfu ya watu waliouawa na kuteswa wakati wa utawala wake,”alisema.

Hatua hiyo pia inatoa mwanya kwa wale wanaotenda uhalifu wa aina hizo fursa za kuikimbia nchi wakisubiri muda upite ndiyo warudi wakijua sheria itakuwa imepoteza meno dhidi yao.

Pamoja na kudai kuunga mkono mageuzi na kuheshimu haki za binadamu, utawala wa Jean-Claude Duvalier uliendekeza ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu na rushwa kushamiri kama ulivyokuwa wakati wa utawala wa baba yake:

Wakati Duvalier akiwa bado hajaeleza sababu za kurudi kwake nchini humo, ilionekana alikuwa akitarajia kunufaika na ombwe la kisiasa lililokuwapo kipindi hicho, akisema amekuja na kile alichokiita dhamira yake ya kusaidia kupata serikali imara yenye misingi ya utulivu na utawala wa sheria. 

Baby Doc akiwa na mkewe Veronique Roy aliporudi Haiti baada ya kuwa ukimbizini

Wakati Duvalier alipowasili Haiti, wafuasi wake 2,000 walijitokeza kumpokea kwenye uwanja wa ndege wa Port-au-Prince.

Lakini serikali ya wakati huo chini ya Rais Rene Preval hakumruhusu kujaribu kutumia kipindi hicho ambacho Haiti ilikuwa katika mgogoro wa kisiasa kufuatia kushindikana kupatikana mshindi katika duru ya pili kupumua kwa raha.

Mashirika ya haki za binadamu mara kwa mara yameripoti uhalifu huo tangu miaka ya 1960 hadi 1980 na ripoti hizo zingeweza kutumika kwa kesi zinazomkabili.

Kwa mara nyingine pia, hakuna maelezo ya kutosha kuthibitisha hilo, lakini imekadiriwa kwamba kati ya Wahaiti 20,000 na 30,000 waliuawa na majeshi ya serikali au kikosi maalumu cha miavuli cha Tontons Macoutes au ‘Majitu ya Kutisha’ chini ya Papa Doc na baadaye chini ya Baby Doc.

Jean-Claude Duvalier na marehemu baba yake, Francois, maarufu kama ‘Papa Doc’, walituhumiwa kupora dola hadi milioni 300 wakati wakiwa madarakani, japokuwa hakuna uthibitisho rasmi kuhusu hilo. 

Fedha hizo zinasemekana kufujwa kutoka kampuni zinazomilikiwa na serikali pamoja na makusanyo ya kodi. 

Alizaliwa mwaka 1951, mjini Port-au-Prince na kulelewa katika mazingira pweke.

Harusi yake iligharimu pesa za walipa kodi sh bilioni sita mwaka 1980

Alihudhuria katika vyuo vya kati vya Bird na Saint-Louis de Gonzague kabla ya kusomea sheria katika Chuo Kikuu cha Haiti, chini ya usimamizi wa maprofesa kadhaa.

Baby Doc aliiongoza nchi baada ya kifo cha baba yake François ‘Papa Doc’, kuanzia mwaka 1971 hadi 1986, wakati alipong’olewa na majeshi ya serikali kufuatia nguvu ya umma na akakimbilia uhamishoni nchini Ufaransa.

Duvalier bado ana baadhi ya wafuasi lakini Wahaiti wengi ni wadogo mno kumkumbuka.

Haiti bado inahaha kuimarisha utawala wa demokrasia baada ya miongo mitatu ya tawala dhalimu za kurithishana za kizazi hicho cha Duvalier.

Baba yake Papa Doc kwa mara ya kwanza aliingia madarakani mwaka 1957, wakati alipodai kushinda uchaguzi huru na wa haki.

Awali alikuwa mtu maarufu, lakini akaanza kuwa muimla na katili, akiithibiti nchi kwa mkono wa chuma kwa msaada wa Tontons Macoutes, ambaye hakuona taabu kuondoa roho ya mtu aliyeleta upinzani wowote.

Mwaka 1964 Papa Doc alijitangaza mwenyewe kuwa rais wa maisha.

Utawala wake ukazidi ukatili na ilikuwa katika miaka ya 1960 wasomi wengi wa Haiti walipokimbilia Marekani, Canada na Ufaransa na kuwa mwanzo ulioshuhudia Wahaiti zaidi ya milioni moja kati ya milioni 11 wakiishi ugenini.

Kufikia mapema miaka ya 1970 afya ya Papa Doc ikaanza kuporomoka na akaitisha Bunge la Taifa, alilolitangazia kuwa mwanae Jean Claude atachukua nafasi yake na pia urais wa maisha.

Mara baada ya kifo, Duvalier akawa rais katika umri wa miaka 19 na kumfanya kuwa rais mdogo kuliko wote duniani.

Duvalier alifanya majaribio ya kuleta mageuzi nchini humo lakini ilishindikana kutokana na baadaye kuamua kufuata mkumbo wa aina ya utawala wa baba yake, pengine kutokana na mama yake, Simone Ovide Duvalier kuwa na sauti katika maamuzi ya nchi.

Ikumbukwe awali, Jean-Claude Duvalier alipinga mpangilio huo wa kurithishana uliomfanya kuwa kiongozi wa Haiti, alitaka urais uende kwa dada yake mkubwa Marie-Denise Duvalier, ili yeye aendelee na starehe zake ikiwamo kuendekeza mabibi.

Lakini mwishowe, ikaonekana akabidhi masuala ya utawala kwa mama yake huyo na kamati iliyoongozwa na Luckner Cambronne, aliyekuwa waziri wa mambo ya ndani wa baba yake, huku yeye akihusika zaidi na matukio ya ufunguzi wa sherehe, na kuendelea kujirusha.

Kwa kukabidhi sehemu kubwa ya mamlaka kwa wasaidizi walioonja na kuzoea aina ya utawala katili wa baba yake, kulisababisha maelfu ya Wahaiti kuendelea kuuawa na kuteswa na mamia kwa maelfu wengine kukimbilia uhamishoni. 

Aliendelea staili ya kifedhuli ya kuishi ‘maisha ya peponi’ ikiwamo kuamuru harusi yake na Michèle Bennett Pasquet kugharimiwa na fedha za walipa kodi dola milioni tatu sawa na zaidi Sh bilioni sita mwaka 1980.

Na alitengeneza mamilioni mengine ya dola kwa kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya na kuuza sehemu za viungo vya mwili kutoka kwa Wahaiti waliokufa huku umasikini miongoni mwa watu wake ukizidi kuongezeka na kulifanya kuwa taifa masikini kabisa barani Amerika.

Mwishowe akabainika hana ujuzi wala uwezo wowote wa kuiondoa Haiti dhidi ya matatizo yake makubwa ya umasikini wa kutupwa, ukosefu wa uwekezaji na ajira.

Matatizo hayo ndiyo yaliyoibua nguvu ya umma iliyoligusa hadi jeshi la nchi lililoamua kushirikiana na Wahaiti kumng’oa mnamo Februari 1986, katika mapinduzi yasiyo na umwagaji damu.

Hivyo Baby Doc akaenda kuishi ugenini kusini mwa Ufaransa.

Awali aliishi maisha ya kifahari kabla ya kuishia katika umasikini baada ya kupoteza sehemu kubwa ya utajiri wake kutokana na talaka chungu kutoka kwa mkewe Michele mwaka 1993.

Aidha dola milioni sita alizokuwa nazo katika akaunti za Uswisi zilitaifishwa tangu mwaka 1986 pamoja na kuwa Februari 2010 mahakama iliamuru arejeshewe baadhi ya mali zake, lakini Serikali ya Uswisi imeendelea kuzuia.

Katika miaka ya karibuni Duvalier amekuwa akitegemea msaada wa fedha kutoka kwa wafuasi wake akiishi katika nyumba ndogo mjini Paris.

Na kipindi akiwa uhamishoni, mara kadhaa alifanya majaribio ya kurudi nyumbani hususani mwaka 2004 alipotangaza kutaka kurejea ili awanie urais lakini bila mafanikio.

Uwapo wake nchini humo, awali ulizua hofu ya kusababisha machafuko yatakayozidi kuidhoofisha nchi hii. Hata hivyo wakati kesi dhidi yake zikianza kuunguruma  alifariki dunia Oktiba 4, 2014 kwa shambulio la moyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles