NA KULWA MZEE – DAR ES SALAAM
UPANDE wa Jamhuri umedai kwamba jalada halisi la kesi ya mauaji inayomkabili mke wa bilionea Erasto Msuya, Miriam Mrita na mwenzake bado liko kwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), linafanyiwa kazi.
Hayo yalidaiwa jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Patrick Mwita, wakati kesi hiyo ilipokuwa inatajwa.
“Mheshimiwa Hakimu jalada halisi la kesi bado liko kwa Mkurugenzi wa Mashtaka analifanyia kazi, naomba mahakama iahirishe kesi hii hadi tarehe nyingine kwa kutajwa,” alidai Mwita.
Hakimu Simba alikubali kuahirisha kesi hiyo hadi Julai 23, mwaka huu kwa kutajwa na washtakiwa walirudishwa mahabusu kwa kuwa shtaka hilo halina dhamana kwa mujibu wa sheria.
Washtakiwa katika kesi hiyo ni mke wa marehemu bilionea Msuya, Miriam na mfanyabiashara Revocatus Muyela, ambao wanadaiwa kwa makusudi walimuua dada wa marehemu bilionea Msuya, Aneth Msuya.
Inadaiwa washtakiwa hao kwa pamoja walitenda kosa hilo la mauaji Mei 25,2016 maeneo ya Kibada Kigamboni, Dar es Salaam.