Na Mary Gwera, Dar es Salaam
KAIMU Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma ameutaka uongozi mpya wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS) kuusoma na kuuelewa mpango mkakati wa miaka mitano wa Mahakama ya Tanzania ili umoja huo uweze kuchangia katika kuutekeleza.
Aliyasema hayo jana alipotembelewa na uongozi wa TLS ulioongozwa na Rais wa chama hicho, Tundu Lissu.
Alisema ni vema kuusoma Mpango Mkakati huo kufahamu ni wapi mahakama inatoka na wapi inapotaka kuelekea hususan katika suala zima la maboresho ya huduma ya utoaji haki nchini.
Mpango Mkakati wa Mahakama ya Tanzania (2015/2016-2019/2010) umegawanyika katika nguzo kuu tatu ambazo ni utawala bora, uwajibikaji na usimamizi wa rasilimali.
Nyingine ni upatikanaji na utoaji haki kwa wakati na kurejesha imani ya jamii na ushirikishwaji wa wadau na umejikita katika kuboresha huduma za utoaji haki kwa ujumla.
Naye Rais wa TLS, Tundu Lissu pamoja na mambo mengine alieleza baadhi ya changamoto zinazowakabili mawakili nchini .
Alisema changamoto hizo ni pamoja na baadhi ya mahakama kutokuwa na ofisi kwa ajili ya mawakili, taratibu za usajili wa mawakili, na nyingine.
Akijibu, Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Ilvin Mugeta alisema Mahakama Kuu inaendelea kufanyia kazi changamoto zote zinazowakabili mawakili.
Mugeta alisema kingine kinachoangaliwa ni kuona uwezekano wa taratibu za malipo kufanyika kwa elektroniki.