27.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, July 24, 2024

Contact us: [email protected]

Jaji Kiongozi atoa waraka msongamano mahabusi magerezani

NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM

SIKU chache baada ya Rais Dk. John Magufuli kutembelea Gereza la Butimba, Mwanza, Mahakama Kuu ya Tanzania imetoa waraka kwa majaji na mahakimu, ikiwataka kuhakikisha kesi zinazofikishwa mahakamani zinakidhi matakwa ya kisheria kuepuka msongamano wa mahabusi.

Hivi karibuni, Rais Magufuli alitembelea gereza hilo na kuzungumza na wafungwa na mahabusi ambako alibaini changamoto lukuki huku suala la kubambikiwa kesi likiongoza kulalamikiwa na wengi.

Waraka huo namba nne wa 2019, umetolewa na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu, Dk. Eliezer Feleshi, kuhusu matakwa ya kuzingatia sheria katika ufunguaji na usikilizaji wa mashauri ya jinai mahakama kuu, mahakama za mahakimu wakazi na mahakama za mwanzo ili kuepukana na msongamano wa mahabusi usio wa lazima.

Dk. Feleshi, alisema waraka huo umelenga kuwakumbusha majaji na mahakimu wajibu unaoendana na viapo vyao na kwamba watafuatilia utekelezaji wake.

“Hakikisheni kesi zinazofikishwa mahakamani zinakidhi matakwa ya kusajiliwa kisheria na zinaposajiliwa hakikisheni mienendo hiyo inaendeshwa kwa kuzingatia matakwa ya sheria ambayo baadhi yametajwa hapo juu.

“Hakikisheni kesi zinasikilizwa na kutolewa hukumu/uamuzi katika muda uliowekwa na sheria na kwa kuzingatia malengo ya mahakama,” alisema Dk. Feleshi.

Kulingana na waraka huo, maelekezo mengine ni kutoa hukumu ndani ya siku 90 kuanzia siku jaji/hakimu alipokamilisha usikilizaji wa kesi husika na kupewa kipaumbele kwa adhabu mbadala ya kifungo cha jela kwa kufuata sheria.

Pia majaji na mahakimu wameelekezwa kuhakikisha vikao vya kusukuma kesi vinafanyika kadiri ya waraka wa Jaji Mkuu Namba 2/1987 kama ulivyorekebishwa mwaka 2003 na 2011 na wachukue hatua zinazostahili kutekeleza maazimio yake.

“Hakikisheni mahakama inashiriki kikamilifu kwenye vikao vya Jukwaa la Haki – Jinai ngazi zote na hakikisheni mwongozo wa ukaguzi unafuatwa kama ulivyo ikiwa ni pamoja na kuwafichua watumishi wa mahakama watakaotuhumiwa kwa vitendo vya rushwa.

“Sambamba na hatua hiyo, vipo vikao vya Jukwaa la Haki – Jinai na vile vya kusukuma kesi ngazi za wilaya, mkoa na taifa ambavyo ni nyenzo za kuziwezesha mamlaka zinazohusika na utoaji wa haki – jinai kutatua changamoto zinazojitokeza katika ngazi mbalimbali katika nchi yetu,” alisema.

Dk. Feleshi alisema pia endapo jaji au hakimu atajiridhisha kuwepo kwa vitendo vya hila vinavyohujumu mwenendo wa kesi iliyo mbele yake, mamlaka – asili ya kuondosha mashtaka na kumwachia huru mshtakiwa itabidi yachukue mkondo wake.

Kwa upande wa wapelelezi na waendesha mashtaka, wamekumbushwa kutenda haki kwa kuzingatia Tangazo la Serikali namba 296 la 2012 linalotoa mwongozo kwa kesi nyingi isipokuwa zile zinazohusisha makosa makubwa ya kukamilisha upelelezi kabla ya kufunguliwa kwa kesi mahakamani.

“Yapo maelekezo ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Novemba 3, 2008 ambayo kupitia kipengele cha nne yanaitaka mamlaka husika kumwajibisha mwendesha mashtaka au mpelelezi ambaye kwa hila atasababisha haki kutotendeka,” alisema Dk. Feleshi.

UZINGATIAJI VIFUNGU VYA SHERIA

Dk. Feleshi alisema Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai na sheria nyingine zinavyo vifungu vya sheria ambavyo kama vitazingatiwa magereza hayatalemewa na mahabusi.

Alisema sheria hizo zina vifungu vinavyohusika na wajibu wa kutoa taarifa ya kutendeka kwa jinai au taarifa ya mpango wa kutendeka jinai.

Hivyo waraka huo unasisitiza uzingatiaji wa vifungu vya sheria katika uandikishaji wa maelezo ya mlalamikaji na haki ya mtuhumiwa/mshtakiwa kupata maelezo ya mlalamikaji pamoja na hati ya mashtaka pale kesi inapofunguliwa mahakamani.

Uandikishaji wa maelezo ya mashahidi mbalimbali wa mashtaka na yale ya washtakiwa, utaratibu wa kutolewa dhamana polisi kwa makosa yanayodhaminika pale ambapo polisi hawajakamilisha upelelezi.

Utaratibu wa kutolewa kwa dhamana mahakamani kwa makosa yanayodhaminika kwa kufuata vigezo vya kisheria baada ya mtuhumiwa kufikishwa mahakamani.

Utaratibu wa kuiomba mahakama isitoe dhamana kwa masilahi ya umma kwa kufuata misingi ya sheria na utaratibu wa kuwaweka wahalifu chini ya uangalizi wa polisi au mahakama bila kuwafungulia mashtaka na kuwafanya wakae mahabusu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles