24.6 C
Dar es Salaam
Saturday, September 7, 2024

Contact us: [email protected]

Waziri Mkuu alipongeza Kanisa la TAG

MWANDISHI WETU-ARUSHA

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, amelipongeza Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG) kwa kuthamini na kutambua kazi zinazofanywa na Serikali ya awamu ya tano.

Alitoa pongezi hizo jana wakati akizungumza na maelfu ya waumini wa TAG katika maadhimisho ya miaka 80 ya kanisa hilo hapa nchini yaliyofanyika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, jijini Arusha.

“Baba Askofu Mtokambali umenifurahisha kwa takwimu ulizozitaja hapa za miradi mikubwa ambayo inatekelezwa na Serikali hii. Kuna wengine hawapendi kusikia mambo kama haya, hongera sana,” alisema.

Majaliwa ambaye alikuwa mgeni rasmi kwa niaba ya Rais Dk. John Magufuli, alisema ameguswa na jinsi kanisa hilo linavyomtambua Rais na wasaidizi wake na kuthamini juhudi za Serikali.

“Serikali hii imedhamiria kuwatumikia Watanzania wote bila kujali dini zenu, rangi wala itikadi za kisiasa. Napenda kuwahakikishia kuwa Serikali ya awamu ya tano itaendelea kumtegemea Mungu pasipo shaka yoyote.

Pia amewapongeza viongozi wa kanisa hilo kwa mafanikio yaliyopatikana katika kipindi chote cha miaka 80.

“Pia nikupongeze Baba Askofu kwa kuchangia mifuko 1,000 ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa shule za sekondari hapa Arusha. Natambua kwamba ulishachangia mifuko mingine 500, asante sana,” alisema.

Alilishukuru kanisa hilo kwa kuendesha maombi maalumu kwa taifa yaliyoongozwa na Mchungaji Titus Mkama.

“Niliguswa sana wakati maombi ya taifa yalipokuwa yakiendelea. Mchungaji aligusia masuala ya muhimu kwa taifa hili,” alisema Majaliwa.

Awali akimkaribisha Majaliwa kuzungumza na maelfu ya washirika waliohudhuria maadhimisho hayo, Askofu Mkuu wa TAG, Dk. Barnabas Mtokambali, alisema anamshukuru Rais Magufuli kwa kulipenda na kulijali kanisa hilo.

Alimpongeza Rais Magufuli kwa miradi mikubwa ya maendeleo anayoisimamia kama vile umeme wa Stiegler’s Gorge, reli ya SGR, ununuzi wa ndege, ujenzi wa hospitali mpya 67 za wilaya, ujenzi wa vituo vya afya 370 na ununuzi wa dawa za hospitali.

“Nina umri wa kutosha, lakini katika miaka yangu yote hii, sijawahi kuona hospitali 67 zikijengwa kwa pamoja. Tena, mwaka huu wa fedha mmetenga hela kwa ajili ya ujenzi wa hospitali nyingine 27. Hongera sana kwa ujasiri huo,” alisema Dk. Mtokambali.

Maadhimisho ya miaka 80 ya TAG yameenda sambamba na hitimisho la miaka 10 ya mpango mkakati wa mavuno.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles