23.5 C
Dar es Salaam
Monday, June 24, 2024

Contact us: [email protected]

Bashe ndani, January nje

*Ni baada ya JPM kufanya mabadiliko madogo Baraza la Mawaziri

*Simbachawene naye arudishwa tena baada miaka miwili

ELIZABETH HOMBO-DAR ES SALAAM

RAIS Dk. John Magufuli ametengua uteuzi wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba na nafasi hiyo kuchukuliwa na Mbunge wa Kibakwe, George Simbachawene.

Pia Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe, ameteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Kilimo nafasi ambayo awali ilikuwa ikishikiliwa na Innocent Bashungwa ambaye hivi karibuni aliteuliwa kuwa Waziri wa Viwanda na Biashara.

Vilevile Rais Magufuli amemteua Balozi Martin Lumbanga kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA).

Taarifa ya Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Gerson Msigwa jana, ilieleza kuwa uteuzi wa viongozi hao umeanza rasmi jana.

Muda mfupi baada ya taarifa hiyo kusambaa katika mitandao ya kijamii, January aliandika katika ukurasa wake wa Twitter akisema amepokea taarifa hiyo huku akiahidi kutoa kauli yake siku zijazo. 

Huku akiambatanisha picha yake akiwa na Rais Mstaafu wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi, January ambaye pia ni Mbunge wa Bumbuli aliandika; “Kwa kweli nimeyapokea mabadiliko yaliyofanywa kwa moyo mweupe kabisa kabisa. Nitasema zaidi siku zijazo.”

Katibu wake, Hozza Mandia, alitoa taarifa akisema; “Ndugu zangu, nimekuwa nikipigiwa simu kutoka maeneo mbalimbali jimboni na nje ya jimbo letu juu ya taarifa iliyotolewa na vyombo vya habari kuhusu kutenguliwa nafasi ya uwaziri wa January Makamba.

“Taarifa hiyo ni sahihi. Ni utaratibu wa kawaida kwa nafasi zozote za uteuzi inapojitokeza, lazima tukubali. Sababu za kutenguliwa hazina athari kwa wananchi wa Bumbuli.

“Ni muda muafaka mheshimiwa kurudi jimboni kuwatumikia wananchi. Pia nimeongea na January muda si mrefu, kubwa tumezungumzia mipango na ratiba zetu za kazi jimboni na nimezungumza naye akiwa na furaha kupongeza maamuzi ya mheshimiwa Rais.”

KAULI YA BASHE

Bashe naye aliandika katika ukurasa wake wa Twitter akimshukuru Rais Magufuli kwa kumwamini na kumteua kuwa Naibu Waziri wa Kilimo.

“Ndugu zangu awali nimshukuru Allah kwa yote, namshukuru kwa dhati Mheshimiwa Rais kwa imani yake, ni jukumu zito nimelipokea, kwa uwezo wa Allah tutavuka, ni ‘sector’ iliyoajiri Watanzania wengi na changamoto nyingi, nawashukuru Watanzania, wananchi wa Nzega na kwa dhati chama changu,” aliandika Bashe.

Zaidi Bashe aliahidi kuwa atakwenda kutoa mawazo mapya ndani ya wizara hiyo ya kilimo.

“Hii ndiyo sekta iliyoajiri Watanzania wengi, inaendesha uchumi wa nchi, inachangia asilimia 28 ya GDP na asilimia 70 ya ajira, lakini ina changamoto nyingi, ninaamini katika ushirikiano tutafanikiwa,” alisema Bashe.

SIMBACHAWENE

Naye Simbachawene, kabla ya uteuzi wa jana alikuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) nafasi ambayo alijiuzulu Septemba 7, mwaka juzi baada ya jina lake kuonekana katika ripoti zilizotolewa na Kamati ya Bunge iliyofanya uchunguzi kuhusu madini ya Tanzanite.

Alichukua uamuzi huo ili kuilinda heshima ya Serikali na nchi kwa ujumla.

Katika mkutano wake na wanahabari waka huo, alisema ameamua kujiuzulu kutokana na agizo la Rais Magufuli.

Ripoti hizo zilionesha kwamba Simbachawene ni kati ya mawaziri waliotajwa kusaini mikataba ya madini iliyosababisha nchi kupata hasara ya mamilioni ya fedha.

Kutokana na ripoti hizo, Rais Magufuli alimtaka kila aliyetajwa ajiuzulu hadi pale uchunguzi utakapokamilika.

ZITTO ATOA NENO

Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo), naye aliandika katika ukurasa wake wa Instagram akimkaribisha mbunge mwenzake January kukaribia tena ‘Backbench’ (nafasi za nyuma ndani bungeni) kuendelea na kazi ya ubunge.

Katika andiko lake, Zitto alimwelezea baadhi ya sifa za mbunge huyo wa Bumbuli akisema ni miongoni mwa mawaziri bora.

“Umekuwa mmoja wa mawaziri bora kabisa ambao umeonyesha tofauti ya kutawala na kuongoza. Namna ulivyoongoza marufuku ya mifuko ya plastiki ilionyesha falsafa yako ya uongozi ni tofauti sana na falsafa ya Serikali yenu ya CCM.

“Tuna kesho nyingi, tupambane kuijenga Tanzania inayojali watu wake na ya kidemokrasia,” alisema Zitto katika andiko lake.

CHANZO CHA UTEUZI

Uteuzi huo umekuja siku chache baada ya makatibu wakuu wawili wastaafu wa CCM, Yusuf Makamba na Abdulrahaman Kinana kuandika barua kwa Baraza la Wazee wa chama hicho, wakitaka chama kichukue hatua dhidi ya mtu anayewachafua huku akijipambanua kuwa mwanaharakati huru anayepambana na wanaomhujumu Rais Magufuli.

Akijibu barua hiyo siku chache baadaye, Katibu wa baraza hilo, Pius Msekwa, alisema wao hufanya kazi kwa njia ya vikao rasmi, hivyo katibu peke yake hana mamlaka ya kutoa uamuzi wowote.

Msekwa ambaye alipata kuwa Spika wa Bunge, alisema kwa mujibu wa Ibara ya 127 (3)ya katiba ya CCM toleo la 2012, kazi ya baraza hilo ni kutoa ushauri kwa chama na kwa Serikali zinazoongozwa na chama hicho.

Hata hivyo hali hiyo iliibua mjadala huku makundi ya watu wakidai kuna mkakati maalumu wa kumdhalilisha Rais Magufuli.

Mjadala huo ulikwenda mbali zaidi ambapo baadhi ya wabunge akiwamo Bashe, walidai kuwa mwasisi wa vitendo vya udhalilishaji ndani ya chama ni Kinana wakati akiwa kiongozi wa chama hicho kwa zaidi ya miaka 40 ya utumishi wake.

Mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Msukuma, aliwataka viongozi hao wastaafu wanyamaze kimya kwani wao ndio waasisi wa vitendo hivyo, lakini sasa wameibuka kwa kuwa wameguswa na kuhisi maumivu.

Naye Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde, alisema kwamba anakwenda nchini China kwa ziara ya kibunge ila akirudi Kinana atamtambua kama ataendelea na mtindo wake huo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles