BEIJING, CHINA
MASOKO makubwa ya hisa ya barani Ulaya yametetereka baada ya Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Fedha (IMF), Christine Lagarde kuingilia kati mzozo wa kibiashara baina ya Marekani na China.
Lagarde ametahadharisha kwamba vizingiti vya kibiashara vitahujumu ustawi wa uchumi wa Dunia.
Masoko ya hisa ya London, Frankfurt na Paris yalipanda na kushuka yakiwepo matumaini kuwa vita vya kibiashara baina ya Marekani na China vitaepushwa.
Akihutubia kwenye kongamano nchini hapa jana Lagarde amesema ustawi wa uchumi wa dunia unaimarika lakini wakati huo huo unatishiwa na vita vya kibiashara.
Ameeleza ni kosa kuzingatia nakisi za biashara kuwa ni ishara ya biashara isiyokuwa ya haki kama ambavyo Rais Trump amekuwa anadai mara kwa mara, hali iliyosababisha mzozo na China.
Katika kile kinachoonekana kuwa onyo la kificho kwa Rais Donald Trump wa Marekani, ambaye anavutana na China masuala ya biashara, Lagarde amesema nchi zinapaswa kuweka biashara zao wazi zaidi, kwa kufanya mageuzi ya ndani badala ya kuweka vizingiti.
Lagarde amesema serikali zinapaswa kuendesha sera za kujiweka mbali na vita vya kibiashara.
Ametahadharisha mfumo wa sheria na wa wajibu sasa umo katika hatari ya kusambaratika.
Hata hivyo, Rais wa China Xi Jinping ameituliza dunia baada ya kutoa kauli ya maridhiano na kuahidi kuiweka wazi zaidi milango ya kiuchumi ya nchi yake.
Jinping amesema China itapunguza cha ushuru unaotozwa magari na pia itachukua hatua ili kulinda haki miliki.
Kauli ya Jinping imepunguza wasiwasi juu ya kufumuka vita vya kibiashara vinayvoweza kuvuruga uchumi wa dunia wakati ambapo uchumi huo unarejea katika hali ya kawaida baada ya mgogoro mkubwa wa mabenki wa hivi karibuni.