Na TUNU NASSOR-DAR ES SALAAM
MANISPAA ya Ilala imeanza ukaguzi wa shule zote za msingi na sekondari kuona kama zimefanikiwa kuweka mazingira salama kabla ya kufunguliwa Juni 29.
Hatua hiyo imekuja baada ya Serikali kutoa maelekezo ya shule kuandaa mazingira salama kwa wanafunzi kujikinga na ugonjwa wa Covid-19.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Ofisa Afya wa manispaa hiyo, Reginald Mlay alisema lengo la ukaguzi huo ni kujiridhisha kama shule zimetimiza maelekezo yaliyotolewa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto.
“Tunaanza ukaguzi leo (jana) kwa shule zote za awali, msingi na sekondari kujiridhisha kama wameandaa mazingira wezeshi kwa wanafunzi kujikinga na ugonjwa wa Covid-19,” alisema Mlay.
Alisema wameandaa vikosi vitakavyotembelea shule zote na kufanya tathmini ya afya na baadaye kutoa taarifa kwa shule zilizokidhi vigezo.
Machi 17, mwaka huu Serikali ililazimika kuzifunga shule zote na vyuo vikuu kufuatia kuwapo kwa mlipuko wa ugonjwa wa Covid-19.
Hata hivyo, Mei 21 Rais Dk. John Magufuli alitangaza kufungua vyuo na kidato cha sita Juni Mosi na Juni 16 alitangaza kufungua shule zote Juni 29.