24.2 C
Dar es Salaam
Monday, September 27, 2021

Daktari: Wanaokaa kwenye joto wapo hatarini kupata mawe ya figo

Na AVELINE KITOMARY-DAR ES SALAAM

DAKTARI bingwa wa mfumo wa njia ya mkojo katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili-Mloganzila, Dk. Jacob Jica, amesema watu wanaokaa  katika mazingira ya joto wako hatarini kupata tatizo la mawe kwenye figo na ameitaka jamii kujenga utamaduni wa kunywa maji kila wakati ili kuepukana na tatizo hilo.

Dk. Jica pia amesema kuwa hata ulaji wa nyama nyekundu kwa wingi unaweza kusababisha tatizo hilo.

Akizungumza na MTANZANIA jana Dar es Salaam,  alisema tatizo la mawe kwenye figo linatokana na kuwepo kwa baadhi ya madini kwa wingi kwenye mkojo.

“Mfano madini yaliyopo kwenye mkojo ni  aina ya calcium oxalate na citric acid,  haya yanaweza kusababisha tatizo hilo  na wakati mwingine inatokana na kutengenezwa kwa kiwango  kidogo cha mkojo  katika figo, hasa wale ambao unywaji wao wa maji sio wa kutosha.

“Vilevile maambukizi ya bakteria katika mfumo wa mkojo yanaweza kusababisha  kupata ugonjwa wa mawe kwenye mfumo wa mkojo,” alisema Dk. Jica.

Alisema tatizo hilo kwa kiasi kikubwa huwaathiri zaidi  wanaume wa kuanzia umri wa miaka 20  huku asilimia kubwa wakianzia miaka 40 hadi 70.

“Njia nzuri ya kuzuia tatizo hilo ni kunywa maji kwa wingi kwani mtu anapopata mkojo vizuri  inasaidia sana, lakini pia tiba ya kisasa ipo,” alibainisha Dk. Jica.

Alisema dalili za tatizo la mawe ya figo inategemea na sehemu jiwe lilipo na ukubwa wake.

“Mtu anaweza kuona dalili kama kukojoa damu, hii inatokea kama jiwe ni kubwa, kupata maumivu wakati wa kukojoa  na wakati mwingine kukojoa usaha,” alisema Dk. Jica.

Takwimu za Hospitali ya Taifa ya Muhimbili katika kipindi cha mwaka 2019 zinaonyesha kuwa jumla ya wagonjwa 1,035 wenye mawe kwenye figo walionwa katika kliniki za wagonjwa wa nje na kati yao wapya ni 425, wakati waliolazwa kutokana na tatizo hilo ni 114.

Wagonjwa waliopewa rufaa kwenda kutibiwa nje ya nchi  kwa  kipindi cha mwaka 2010 hadi 2017 walikuwa ni  23.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
158,310FollowersFollow
519,000SubscribersSubscribe

Latest Articles