23.9 C
Dar es Salaam
Wednesday, July 24, 2024

Contact us: [email protected]

…Ikulu yapata hati ya chafu 

ikuluNA BAKARI KIMWANGA, DODOMA

RIPOTI ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), imezidi kuibua namna upigaji ‘dili’ ulivyofanyika kwa fedha za umma katika taasisi na idara nyeti, zikiwamo Bunge na Ofisi ya Rais Ikulu.

Katika vitabu 11 vya taarifa ya CAG, imebainika kuwa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutokana na makisio ya juu, zaidi ya mahitaji lilinunua samani za Sh milioni 94.344 wakati wa maandalizi ya Bunge Maalumu la Katiba ambazo sasa hazitumiki.

Hayo yalibainika juzi, baada ya CAG Profesa Mussa Assad, kukabidhi vitabu vya ukaguzi.

“Wakati wa maandalizi ya Bunge Maalumu la Katiba, samani zilizonunuliwa zilikuwa zaidi ya mahitaji, hivyo kusababisha samani zenye thamani ya Sh milioni 94.344 zimekosa matumizi, sasa zimehifadhiwa ghalani,” alisema Profesa Assad.

 

OFISI YA RAIS IKULU

Ripoti ya CAG pia imefichua namna ambavyo Ofisi ya Rais Ikulu, ilivyopata hati isiyoridhisha katika fungu 20, huku Bunge ikitajwa kwenye fungu 40.

Kwa mujibu wa utaratibu, taarifa hizo kwa undani hutolewa baada ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), itapokutana na kuanza uchambuzi wa kina.

Ripoti hiyo, pia inaonyesha bodi ya mishahara nayo imepata hati ya aina hiyo.

Licha ya ofisi hizo, Ofisi ya Rais – Baraza la Mawaziri nayo imepata hati isiyoridhisha pamoja na ofisi binafsi ya Makamu wa Rais, ofisi binafsi ya Waziri Mkuu na ofisi ya Rais Utumishi.

Mbali na hilo, pia CAG alisema ofisi ya Makamu wa Rais nayo imepata hati isiyoridhisha kutokana na kushindwa kufutilia miradi yenye kipaumbele.

 

SHULE YA SHERIA

Ripoti hiyo ambayo ukaguzi wake unaishia Juni 30, 2015, pia inaeleza namna Shule Kuu ya Sheria Tanzania ilivyoingia mkataba wa Sh milioni 213.561, ikijumuisha Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) na Kampuni ya Invention Technology Limited kwa ajili ya ununuzi wa vifaa na ufungaji kiungo cha kuwezesha kufanya mikutano kwa kutumia nyenzo ya runinga.

Hata hivyo, vifaa hivyo vilivyofungwa havijaanza kufanya kazi kwa sababu hakukuwa na makubaliano kati ya Shule Kuu ya Sheria na mahakama ili kuwawezesha wanachuo kufuatilia mienendo ya kesi kama ilivyokusudiwa.

“Ninashauri Shule Kuu ya Sheria ifuatilie mkataba huo ili kuhakikisha malengo yaliyokusudiwa yanafikiwa kulingana na thamani ya fedha.

“Kitendo cha kushindwa kuweka kiungo husika na kuwezesha matumizi ya vifaa vilivyonunuliwa, kunaashiria kutofikiwa kwa thamani ya fedha kama ilivyokusudiwa,” ilieleza taarifa hiyo.

 

JICHO APRM

Pia CAG alisema Mpango wa Kujitathimini kwa Nchi za Afrika (APRM), ulishindwa kuwasilisha Sh 89,286,386 Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Katika fedha hizo, Sh 61,734,761 zilikuwa kwa ajili ya mwaka wa fedha 2013/14 na Sh 27,551,625 kwa mwaka wa fedha 2014/15.

“Katika mwaka wa fedha 2014/15, APRM walipokea Sh 681,221,236 kama ruzuku ya Serikali. Tunakumbuka APRM ilianzishwa Mei 26, 2004 na Serikali kwa kuridhiwa na Bunge, hadi wakati wa ukaguzi Desemba Mosi, 2015 sekreterieti ilikuwa inafanya kazi bila kutangazwa katika gazeti la Serikali, hivyo kukosa hadhi ya kisheria,” ilieleza taarifa ya CAG.

 

YALIYOJITOKEZA

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, sura ya 10 ilieleza wakati wa ukaguzi ilibainika kuwa wizara 17, balozi mbili na sekreterieti za mikoa 11 zilifanya malipo ya Sh bilioni 11.314 ambayo yalikuwa na nyaraka pungufu kinyume cha kanuni 86 (1) ya kanuni za fedha ya mwaka 2001, pia na kanuni 95 (4) na 18 (f) ya kanuni za fedha ya mwaka 2001.

“Nyaraka za viambatanisho zikikosekana inakuwa vigumu kuthibitisha pasipo shaka uhalali wa malipo hayo, hivyo kufanya mawanda ya ukaguzi kuwa finyu,” alisema.

Juzi, Profesa Assad baada ya kusoma ripoti hiyo aliwakabidhi wenyeviti wa kamati za kudumu za Bunge; Hesabu za Serikali (PAC) na ile ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC).

Akisema ofisi yake imekagua taasisi za Serikali Kuu 199, Mamlaka ya Serikali za Mitaa 164 na mashirika ya umma 102, kati ya 186.

Profesa Assad alisema kwa upande wa miradi ya maendeleo, ametoa ripoti 799 na kufanya jumla ya ukaguzi wa fedha.

Akisoma muhtasari wa ripoti kwa zaidi ya saa mbili, CAG Assad alisema halmashauri zilizopata hati safi ni 47, hati zenye shaka 113, hati isiyoridhisha tatu na hati mbaya moja.

Kwa upande wa Serikali Kuu, wizara zilizopata hati safi ni 180, hati yenye shaka 18, isiyoridhisha moja na hakuna hati mbaya.

Huku kwa upande wa mashirika ya umma yaliyopata hati safi ni 99, yenye shaka matatu na  hakuna iliyopata hati isiyoridhisha wala hati mbaya.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles