NA SUSAN UHINGA
Takukuru Mkoa wa Tanga imeitaja Idara ya Serikali za mitaa kuwa ndio iliyokithiri kwa vitendo vya rushwa ikifuatiwa na idara ya Mahakama.
Akisoma taarifa ya utendaji kazi wa Takukuru mkoani Tanga kwa mwaka wa fedha 2017/2018, Meneja wa Takukuru Christopher Mariba, amesema taasisi hiyo imeongoza kwa asilimia 25 sawa na vitendo 136Â huku Idara ya Mahakama ikiwa na vitendo 29 vya makosa ya rushwa.
Meneja huyo amezitaja idara nyingine zilizojihusisha na vitendo vya rushwa kwa taasisi ya umma kuwa ni misitu ,uhamiaji, afya, polisi, ardhi, vyama vya siasa, elimu, biashara , vyama vya ushirika pamoja na bima.
Aidha amesema katika uendeshaji wa mashitaka, Takukuru Mkoani hapa imeendesha Jumla ya mashauri 27 huku mashauri 4 yameshamalizika kwa kutolewa hukumu ambapo shauri moja ilishinda .
Aliongeza kuwa taasisi hiyo imeweza kuokoa shilingi milioni 34.78 zilizotokana na hatua zilizochukuliwa dhidi ya malipo ambayo yamefanyika kinyume na sheria.
Taasisi hiyo inaendelea na jitihada za kutoa elimu kwa kushirikisha jamii katika mapambano dhidi ya Rushwa ambapo kwa mwaka wa fedha 2017/2018 imeweza kutoa jumla ya semina 127 kwa makundi mbalimbali wakiwemo watumishi wa Idara ya Afya na Elimu.
Katika uchunguzi uliofanywa na taasisi ya hiyo mkoani Tanga, ilipokea Jumla ya taarifa 366 za vitendo vya rushwa.