24.1 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

WAANDISHI TUMIENI KALAMU ZENU KUELIMISHA AFYA YA UZAZI

NA VERONICA ROMWALD – NAIROBI

Waandishi wa habari wameshauriwa kutumia vema kalamu zao kuelimisha jamii kuhusu masuala ya afya ya uzazi ili kuunga mkono juhudi za Serikali katika nchi zao za kupambana na matatizo ya uzazi.

Rai hiyo ilitolewa hivi karibuni mjini Nairobi na Waziri wa Afya wa Uganda, Sarah Opendi alipozungumza katika hafla ya kuwatunuku tuzo ya uandishi wa habari za afya ya uzazi zilizotolewa na Taasisi isiyo ya Kiserikali inayojihusisha na masuala ya kijamii, kiuchumi na maendeleo, Merck More Than A Mother.

Pamoja na hilo, Opendi alisema kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), takribani asilimia 25 ya wana ndoa duniani wanakabiliwa na matatizo ya uzazi yanayopelekea kukosa watoto maishani (utasa).

“WHO linaeleza asilimia kubwa ya wanaokabiliwa na matatizo ya uzazi ni waishio katika nchi zinazoendelea, Uganda ikiwamo, ni changamoto kubwa lakini tunaendelea kufanya juhudi kukabiliana nayo,” alisema.

Aliwataka pia kutumia vema mitandao ya kijamii kufikisha ujumbe sahihi kuhusu masuala ya uzazi na kutoa taarifa zitakazowajenga na si kuwabomoa.

Naye, Naibu Waziri wa Afya, Kenya, Dk. Rashid Aman alisisitiza kuwa kuwa ikiwa jamii itapewa elimu sahihi itasaidia kukabili changamoto hiyo kwani asilimia 80 ya matatizo yanaweza kuzuilika.

“Ndoa nyingi zinavunjika kwa kukosa watoto, watu wanakumbana na unyanyasaji huko kwenye jamii, tunapaswa kupaza sauti kuzisaidia jamii zetu,” alisema.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo, Dk. Rasha Kelej aliongeza kuwa matatizo hayo huwakumba watu wa jinsi zote hata hivyo katika jamii nyingi wanawake pekee ndiyo hunyooshewa kidole.

“Kuna visababishi vingi vinavyoweza kuchangia hali hiyo kutokea, ikiwamo magonjwa ya ngono, utoaji mimba ovyo, sababu kama hizi zinaweza kuepukwa kwa kuelimisha jamii,” alisisitiza.

Akizungumza na MTANZANIA, Mashaka Mgeta ambaye ni mwandishi pekee kutoka Tanzania (Gazeti la Jambo Leo) aliye miongoni mwa washindi katika tuzo hizo, alisema waandishi wa habari wanapaswa kuwekeza zaidi katika masuala yanayohusu afya ya uzazi.

Alisema hatua hiyo itaiwezesha jamii kupata taarifa sahihi zitakazosaidia jamii kukabiliana na changamoto za afya ya uzazi na ambazo zimekuwa chanzo cha matatizo kadhaa ya kiafya na kijamii.

“Ingawa vyombo vya habari vinashiriki katika kuandika na kutangaza masuala ya afya ya uzazi, lakini ipo haja ya kuongeza ubunifu na weledi vitakavyoyafanya masuala hayo kuwa moja ya ajenda za kuchochea mabadiliko katika sekta hizo nchini,” alisema Mgeta.

Mgeta ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari za Afya (THJ), alisema katika kuchangia ukuzaji uelewa, chama hicho kinaandaa mpango wa mafunzo kwa waandishi wa habari kuhusu namna bora zaidi ya kuandika na kutangaza habari za afya ya uzazi.

Pamoja na Mashaka waandishi wengine waliotunukiwa tuzo hizo ni kutoka nchini Kenya, Uganda, Afrika Kusini, Mozambique, Cameroon na Botswana

Hafla hiyo ilihudhuriwa na waandishi wapatao 200 kutoka nchi 17 zilizopo barani Afrika na mwandishi wa Habari za Afya wa Gazeti la MTANZANIA, Veronica Romwald alitunukiwa cheti cha heshima kwa kuwasilisha kazi yake kushindanishwa katika shindano hilo.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Merck, Dk. Kejel, mashindano hayo kwa mwaka 2018 yamezinduliwa na kwamba wakati wowote kuanzia sasa watatangaza ‘link’ ambayo waandishi wataitumia kuwasilisha kazi zao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles