24.4 C
Dar es Salaam
Thursday, October 31, 2024

Contact us: [email protected]

HUU NDIO MWISHO WA BARCELONA?

ADAM MKWEPU NA MITANDAO


MFANO  wa nyota wa Barcelona, Lionel Messi kuanguka kifudifudi kwenye Uwanja wa Nou Camp katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Juventus usiku wa Jumatano iliyopita, ulionekana kueleza zama za mwisho za Barcelona na hali yao ya sasa.

Barcelona haikuwahi kuwa katika hali hii kabla ya kocha wa sasa, Luis Enrique achukue timu hiyo miaka mitatu iliyopita na tayari ametangaza kuondoka baada ya msimu kumalizika huku akiacha timu hiyo ikipita katika wakati mgumu.

Maswali mengi kutoka kwa mashabiki ni kuhusu nani anastahili lawama na kitu gani kilichoiangusha hadi kufika hapo ilipo huku wengine wakitaka kufahamu namna ambavyo watamaliza matatizo yao.

Lakini swali la msingi ni wapi walikosea hadi wakafika katika hatua hiyo au sera ya klabu ilipindishwa na kusababisha kuanguka kwao.

Neno moja ni kwamba, mbali na kumsajili beki wa kati, Samuel Umtiti, Barcelona haijawahi kumsajili nyota wa kiwango cha juu kama ilivyokuwa kwa Luis Suarez mwaka 2014.

Kwani klabu hiyo ilitumia pauni milioni 30 kupata saini ya Arda Turan, baada ya kupata taarifa kwamba nyota huyo alikuwa na mpango wa kutimka katika timu yake ya zamani ya Atletico Madrid.

Barcelona pia ilitumia pauni milioni 30 kwa Andre Gomes, mchezaji ambaye alikuwa katika wakati mgumu katika timu yake ya zamani ya Valencia msimu uliopita.

Mabingwa hao tena wapo katika mpango wa mwisho wa kuinasa saini ya Paco Alcacer kwa pauni milioni 30 wakiendelea kutafuta kuziba pengo la Dani Alves kwa muda mrefu na safari hii wanataka kuwapa Sevilla pauni milioni 15 kuipata huduma ya Aleix Vidal.

Wachezaji wengine ni Lucas Digne na Denis Suarez, hata hivyo licha ya kutumia fedha nyingi kwa ajili ya kukijenga kikosi hicho, bado kikosi chao hakijawa na ubora unaotakiwa.

Kutokana na hali hiyo, labda anayetakiwa kulaumiwa kwa sasa ni Mkurugenzi wa benchi la ufundi la klabu hiyo, Robert Fernandez, si kocha Enrique kama wengine wanavyodhani.

Enrique aliomba kumsainisha Turan na kusisitiza angemtumia kama kiungo wa kati lakini klabu hiyo ikaona mchezaji sahihi katika nafasi hiyo kwa sasa ni Alcacer.

Hata hivyo, ili Barcelona waweze kuwa na matumaini ya ubingwa wa La Liga msimu huu lazima washinde katika mchezo wa Clasico dhidi ya Real Madrid, kwani kwa sasa wamebakiwa na michezo saba ya ligi hiyo.

Kama Barcelona watashindwa kuwafunga Madrid wataondoa matumaini yao ya kunyakuwa ubingwa huo msimu huu.

Mashabiki wa timu hiyo wataendelea kumkumbuka Enrique kwa mafanikio yake ya kushinda makombe matatu katika msimu wa kwanza.

Jambo jingine watakaloweza kumkumbuka ni aina ya uchezaji wa timu hiyo ambayo kwa sasa inaonekana kuwa timu ya kawaida tofauti na zamani ilipokuwa chini ya kocha Pep Guardiola.

 

Kutokana na kitendo chake cha kuondoka katika timu hiyo mwishoni mwa msimu, tayari makocha watatu wapo katika orodha ya viongozi wa Barcelona akiwamo kocha wa Sevilla, Jorge Sampaoli, Carlos Unzue ambaye ni msaidizi wa Enrique  na Ernesto Valvede ambaye tayari ameaga katika klabu yake ya Athletic Bilbao kuwa ataondoka msimu ujao.

Valvede aliwahi kucheza Barcelona  nafasi ya ushambuliaji kwa miaka miwili  mwaka 1998 hadi 2000 na alishinda mataji mawili, Kombe la Mfalme na Kombe la Ligi ya Mabingwa likifahamika wakati huo kabla ya kujiunga na Bilbao kwa miaka sita.

Mashabiki wengi wa Barcelona wanaamini kuwa Valvede atawasaidia kama akiwa kocha wa timu hiyo, hata hivyo kocha huyo alikuwa chaguo la pili wakati klabu hiyo ilipomteua Tata Martino aliyefariki mwaka 2014.

Barcelona kwa sasa inahitaji wachezaji muhimu wa eneo la beki wa kulia na kushoto pamoja na kiungo wa uhakika.

Hadi sasa bado wanasuasua kwa nyota wa Arsenal, Hector Bellerin, hata hivyo wanafahamu namna ya kumaliza suala hilo kwa kuwa inawezekana kwa Arsenal kumwachia mchezaji huyo.

Chaguo lingine lipo kwa kiungo Marco Verratti lakini Paris Saint Germain (PSG) hawana mpango wa kumuuza nyota huyo na inaonekana kuwa ngumu kwao.

Kiungo wa Liverpool ndilo chaguo lililobakia baada ya dili la Verratti kuonekana kuwa gumu na usajili wa Coutinho haitakuwa kazi rahisi kuipata saini ya kiungo huyo tegemeo Liverpool.

Lakini Barcelona wanataka kumuunganisha na Neymar Jr na nyota wa zamani wa Liverpool, Luiz Suarez, hata hivyo kocha wa timu hiyo, Jurgen Klopp, atakuwa tayari kumtafuta mchezaji mbadala endapo watamuuza.

Tatizo lililopo kwa Coutinho ni kiungo anayependa sana kushambulia, anaweza kuwa mbadala wa Andrea  Iniesta lakini hawatakuwa na haja ya kiungo wa kukaba mtu na mtu (box to box).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles