28.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

SIMBA, YANGA WANATUVURUGIA SOKA LETU

Na ADAM MKWEPU-DAR ES SALAAM


NANI kasema lazima bingwa wa Ligi Kuu awe timu ya Simba au Yanga labda  ndio viwango vya soka letu vitaongezeka kimataifa? Huko ni kujidanganya.

Hakuna klabu mbovu hapa nchini kama Simba na Yanga na hilo ndilo linalochangia viwango vya soka letu kuporomoka kila kukicha.

Kitu pekee walichofanikiwa ni kuwa na mashabiki wengi kutokana na kuanzishwa zamani kwa malengo tufauti lakini walitumia mpira kuwaunganisha.

Wingi wa mashabiki hao ndiyo sababu ya klabu hizo kuwa na ushawishi mkubwa hadi kuitisha Serikali pindi linapokuja suala la kuingilia masilahi ya klabu hizo.

Morali ni muhimu sana kwa klabu  yoyote ndio maana hufikia hatua shabiki kuitwa ni mchezaji wa 12, hilo wamefanikiwa kiasi cha kila kinachofanywa na klabu hizo wanachama wao hudhani kina ukweli, kumbe ni uongo na kutafuta pa kujifichia.

Simba na Yanga ndizo klabu zinazofanya nyingine zisionekane hata kama zinafanya vizuri ilhali hazina nguvu basi zitaishia ‘matopeni’.

Klabu hizo mbili zina ushawishi mkubwa katika soka letu kiasi ambacho kuna wakati zinajihusisha na hila za kulishawishi Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), liamini kuwa bila ya wao  soka la nchi hii litapotea. Kumbe si kweli.

TFF inafikia hatua kuchukua wachezaji wengi wa timu ya Taifa kutoka Simba na Yanga kutokana na majina yao kuwa makubwa lakini kiuwezo bado wachezaji wa Mbao FC na Ndanda FC wanaweza kuwa vizuri zaidi.

Kufanya kwetu vibaya kimataifa kunachangiwa na mambo mengi ikiwemo kuchanganya soka na siasa ambazo zinafanywa kwa kuwanufaisha baadhi ya watu wachache ndani ya nchi hii.

Mfano mzuri ni hili la pointi tatu za Kagera Sugar ambazo Simba zinawafanya kuhamasishana suala la kuandamana hadi kwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Harrison Mwakyembe, wakidai kutotendewa haki.

Kwa mujibu wa Katiba ya TFF, Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji, ina mamlaka ya kutafsiri sheria na kanuni za mpira wa miguu nchini kama ilivyoainishwa kwenye katiba na sehemu ya utangulizi ya kanuni za Ligi Kuu.

Kamati hiyo ilikutana wiki iliyopita katika Hoteli ya Protea iliyoko Oysterbay jijini Dar es Salaam, kutokana na ombi la timu ya Kagera Sugar ambayo imeomba kupitiwa upya uamuzi uliofanywa na Kamati ya Saa 72.

Kamati hiyo kwa mujibu wa kanuni, ilitoa matokeo mapya ya mchezo kati ya timu hiyo na Simba uliofanyika Aprili 2, mwaka huu Uwanja wa Kaitaba mkoani Kagera.

Simba ambayo ni sehemu ya wanaolalamika walitakiwa kutulia hadi wapate majibu si kutumia nguvu ya mashabiki wao kutafuta huruma kutoka katika mamlaka fulani.

Ni upuuzi kujenga taswira ya kuonewa kila msimu wakati mpira una utaratibu wake ndani ya uwanja kwani lazima kuwa bingwa hata kama hauna uwezo wa kufanya hivyo.

Kwa haya yanayoendelea ni wazi kabisa soka letu limeingia katika mtego wa wanasiasa na kama hatujaliangalia na kulitetea litaendelea kupotea kabisa katika uso wa wamamichezo.

Kwani kinachofanywa na Simba leo ndicho kitakachofanywa na Yanga huko tuendako maana hizi klabu zipo kama mapacha, leo atafanya huyu kesho yule.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles