KUONGEZEKA kwa mvutano kutoka kwa mashabiki wa timu ya Manchester united na Manchester City, kumedaiwa kuongeza hofu ya usalama katika mchezo wao unaotarajiwa kuchezwa Jumamosi uwanja wa Old Trafford, England.
Kwa mujibu wa mtandao wa Daily mail, mchezo huo unatarajiwa kuwa chini ya ulinzi mkali wa kihistoria kila kona ya mji wa Manchester.
Uwanja huo unatarajia kuwa na polisi takribani 400 watakaoanza doria saa 12:30 usiku wakiwa katika ulinzi mkali kabla ya mchezo huo wenye upinzani mkali.
Manchester United wanatarajia kukutana na ushindani mkali tangu msimu uliopita katika mchezo dhidi ya Bournemouth ambao uliahirishwa kutokana na madai ya kuwapo kwa bomu katika uwanja wa Old Trafford.
Wafanyakazi wa uwanja huo kwa sasa wapo katika presha kubwa ya usalama kutokana na walinzi wa uwanja huo kufanya operesheni ya ukaguzi kila wakati, hasa baada ya tukio dhidi ya Bournemouth kutokea.
Mtandao wa Daily mail unadai kwamba wataalamu wa matukio ya kigaidi wapo kila kona ya uwanja huo.
Moja ya lengo la kuwapo kwao ni kuzuia kutokea tena tukio la kutishia usalama tangu lilipotokea katika mchezo dhidi ya Bournemouth.
Hata hivyo, upande wa Jeshi la Polisi wa mji huo, walithibitisha kusimamia kwa umakini usalama katika mchezo huo.
“Hadi sasa hakuna taarifa yoyote mbaya inayotishia usalama katika mchezo huo,” kilisema chanzo kimoja cha Polisi.
Kuwapo kwa hali ya kutoelewana baina ya mashabiki wa timu hizo katika maeneo mbalimbali ambayo ni maarufu kwa starehe katika jiji hilo, pia kumeongeza presha ya usalama ya mchezo huo.
Kocha wa Manchester United, Jose Mourinho na Kocha wa Manchester City, Pep Guardiola, wamedaiwa kuwa katika upinzani mkubwa zaidi ya miaka 20 iliyopita tangu wakiwa pamoja katika klabu ya Barcelona.
Mkuu wa kitengo cha usalama katika jiji la Manchester, Dean Howard, alisema mchezo huo utakuwa ukifuatiliwa na kila mpenzi na shabiki wa soka duniani.
“Tuna ujuzi wa kutosha katika matukio ya aina yoyote hivyo tupo karibu na mashabiki pamoja na wapenzi wa soka wa timu zote ili kubaini kuwapo kwa kitendo cha kutokuwa na usalama,” alisema Howard.