MOSCOW, Urusi
HAKUNA utakavyoweza kuziepuka taarifa za fainali za Kombe la Dunia, ikizingatiwa kuwa ni kipindi kisichozidi wiki tatu ndicho kilichobaki kabla ya michuano hiyo kuanza.
Ukiacha mataifa makubwa kama Ujermani na Brazil ambayo yamekuwa yakipewa nafasi ya kutoana jasho katika kuufukuzia ubingwa kutokana na ubora wa vikosi vyao, Afrika ambayo haijawahi kutinga nusu fainali, Â itakuwa na wawakilishi wake watano.
Makala haya hayatazigusia Nigeria, Tunisia, Senegal wala Morocco na badala yake itajikita Kundi A ambalo mashabiki wa soka barani humu watakuwa wanalifuatilia kwa kuwa lina Misri.
Ikumbukwe kuwa Mafarao walio chini ya kocha wa kimataifa wa Argentina, Hector Cuper, shabiki mkubwa wa mfumo wa 5-3-2, watakwenda Urusi ikiwa ni miaka 28 imepita tangu waliposhiriki fainali za Kombe la Dunia.
Kuelekea mikimiki ya mashindano hayo yatakayofanyika kwa mwezi mmoja, mashabiki wa Misri wanajivunia makali aliyonayo staa wao anayekipiga Ligi Kuu England.
Huyo ni Mohamed Salah ambaye tangu kuanza kwa msimu huu uliomalizika siku chache zilizopita, amekuwa moto wa kuotea mbali katika kuzipasia nyavu za wapinzani wanaokutana na Liverpool.
Salah alikuwa mwiba mchungu pia kwa timu zilizokutana na Misri katika mbio za kuiwania tiketi ya kwenda Urusi. Mechi zake sita za kufuzu, zilimshuhuduia akipachika mabao matano.
Katika mabao yake hayo, lipo alilopachika kwa penalti ya dakika za majeruhi wakati Misri ikiwatandika Congo mabao 2-1, matokeo yaliyowawezesha kupata nafasi ya kwenda Kombe la Dunia.
Akiwa Liver, Salah amekuwa aking’ara kwa kutokana na pasi za mabao ‘asisti’ za Roberto Firmino na Sadio Mane lakini kazi hiyo nchini Urusi itafanywa na kiungo wa Arsenal, Mohamed Elneny na winga wa Stoke City, Ramadan Sobhi.
Kwa upande mwingine, mashabiki wa soka nchini Misri wanajivunia aina ya wapinzani wao katika Kund A- Uruguay, Saudi Arabia na Urusi, ambao hawaonekani kuwa wa kutisha hata waweze kuwazuia kutinga 16 bora.
Huku timu mbili katika kila kundi zikiwa na uhakika wa kusonga mbele, ni wazi Misri wanaweza kwenda Uruguay ambayo inatarajiwa kuwa na mastaa kama Edinson Cavani na Luis Suarez.
Licha ya kwamba ndiyo wenyeji, Urusi si tishio na baadhi ya wachambuzi wa soka barani Ulaya wameitabiria kufuata nyayo za Afrika Kusini ambayo mwaka 2010 iliweka rekodi ya kuwa timu ya kwanza kuandaa fainali za Kombe la Dunia na kuishia hatua ya makundi.
Hizo itakuwa ni fainali za nne kwa Uruguay na ni mabingwa wa mwaka 1930 (michuano ya kwanza) na 1950.
Lakini pia, vijana hao wa Amerika Kusini walikuwa wa moto wakati wa mechi za kufuzu Kombe la Dunia mwaka 2010, kwani walishika nafasi ya pili nyuma ya Brazil waliomaliza mechi za kufuzu wakiwa kileleni.
Hata hivyo, rekodi hazioneshi kuwa Misri watashindwa kuchukua pointi tatu katika mchezo watakaokutana nao hapo Juni 15. Katika mechi tatu zilizopita, Misri amefungwa moja na zilizobaki zilimalizika kwa matokeo ya kutofungana.
Wamisri wana rekodi nzuri hata kwa wenyeji Urusi kwani michezo mitatu waliyowahi kukutana nao, walishinda mmoja, wakafungwa mmoja na mwingine ukaamuliwa kwa sare.
Ukiitaja Saudi Arabia, unaizungumzia timu ambayo imeambulia ushindi wa mechi moja kati ya nne dhidi ya Misri, huku ikichezea vichapo sita.
Ni kwa mazingira hayo, safari ya Waarabu hao wa Kaskazini mwa Bara la Afrika kwenda hatua ya mtoano (16 bora) inaweza kuonekana wazi hata kabla ya kuanza kwa fainali hizo zitakazomalizika Julai 15.