21.5 C
Dar es Salaam
Tuesday, July 23, 2024

Contact us: [email protected]

Hivi ndivyo Dk. Magufuli anavyoingoza Tanzania

NapeBILA ya shaka masuala magumu yanaanza kuikabili Serikali  ya Dk. John Pombe Magufuli  juu ya suala la utawala bora na nia ya kuiongoza nchi mbali zaidi katika njia hiyo. Shaka hiyo sasa iko dhahiri kwa kila mtu kuona, isipokuwa wale ambao sio tu wameziba macho lakini pia masikio yao.

Utawala bora ulianza kuwa suala gumu kwa Serikali ya Magufuli pale alipoanza kutaka kuifanya Serikali kama yake (personalization) kwa kupigia chapuo kwa kauli mbiu ya “Serikali ya Magufuli” na pia kwa kauli mbiu ya “ Tanzania ya Magufuli” na zikawa ni dalili mbaya lakini wengi hawakuliona hilo.

Kwangu mimi hilo niliona ni kitu ambacho kilianza kujenga himaya ya mamlaka ya Rais ambayo hayawezi kuhojiwa kwa sababu Serikali na Tanzania zote “ni zake.” Si lazima iwe hiyo ni moja kwa moja lakini kwa hisia mtu aweza kutaka kudhani hivyo.

Kutokana na hilo basi uongozi wa Magufuli ukaja na dhana ya kutumbua majipu ambapo hakuna anayekataa hilo maana majibu yakibaki mwilini ni sumu kwa Watanzania wote, lakini naona ya utumbuaji imezua masuala mengi kuliko majibu.

Lakini imekuwa sisi ambao tunahoji utumbuaji ambao una athari za kisheria ( legal implications) na ambao unafanywa papo kwa papo mara nyingi haungefaa katika nchi ambayo inatambaa katika utawala  bora, lakini anayepinga hilo huonekana kuwa ni mpinga Serikali, ilhali sote ni wananchi na hii ni nchi yetu na tunakosoa kwa ajili ya kusonga mbele.

Kwa kuwa hilo limekuwa likiendelea na Serikali imefanikiwa vitu viwili basi mengine makubwa zaidi yamekuwa yakitokea. Kwanza Serikali imefanikiwa kunyamazisha wakosoaji wake ambao ni wa ndani na hasa pale tamko la Rais liliposema “wanarekodiwa” lakini pia kupata watu wengi wanaofuata mkumbo wa kushangilia kila jambo la Serikali hata kama athari yake ya kesho ni ya kwao, lakini kwa leo Magufuli ndio shujaa wao.

Sasa inaelekea nguvu za Serikali zimehamishiwa katika Bunge la Jamhuri ya Muungano ambapo hivi sasa linakutana katika kikao kirefu cha kujadili na kupitisha Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2016/2017, ikiwa ni bajeti ya mwanzo kwa kipindi cha miaka mitano ya Magufuli.

Ilianza kikao cha pili cha Bunge la 11 pale tamko la Serikali lilipowasilishwa na Waziri Nape Nnauye kuwa vikao vya Bunge havitarushwa moja kwa moja ili wananchi wavione na waone wabunge wao wakiwa kazini. Sokomomoko ikazuka bungeni na kusababisha hata askari kuingizwa ndani ya Bunge na wabunge kusulubiwa.

Wabunge waliokutana na kipigo na wengine kufunguliwa mashtaka ndani ya Bunge chini ya Kamati ya Maadili ni wale wa upinzani.  Inashangaza wabunge wa CCM hawakuhusika kabisa na kuonekana kama wanaunga mkono hatua hiyo ya Serikali na hivyo kama kusema kuwa hawana haja ya kuonekana na wananchi wao na kuwa uamuzi huo wa Serikali ni sahihi.

Lakini sote tunajua kuna wabunge kadhaa wa CCM katika hili wanafuata mkumbo na maelekezo ya chama chao ambacho ndicho kinachoendesha Serikali na ni ambacho kinafanya makusudi kuwaziba koo wapinzani ili wasionekane na wala kusikika na wananchi.

Mfumo wa sasa wa kutoa habari unakwaza kabisa uhuru wa kukusanya na kusambaza habari na baadaye kuwafikia wananchi kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania, lakini wabunge wa CCM ambao wamo kadhaa wenye elimu ya kutosha wanakubali kuliunga mkono hili na badala yake kulalamikia pembeni kuwa ni uamuzi wa chama chao na hawawezi kwenda kinyume nao.

Hivi sasa hali imekuwa mbaya bungeni maana kamera yoyote ya kuchukua filamu hairuhusiwi ndani ya Bunge na badala yake waandishi kugaiwa vipande vya filamu vilivyochukuliwa na wafanyakazi wa Bunge na kwa hivyo hakuna hakika ya kupata wakitakacho.

Kwa kukosa kuonyeshwa moja kwa moja badala yake Televisheni ya Taifa hurusha sehemu ya yale yaliyotokea asubuhi na jioni katika Bunge lakini hapana shaka TBC haina muda wa kuonyesha kila kitu na katika hali hiyo hakuna uhakika iwapo wapinzani watapewa nafasi katika vipindi hivyo vinavyokuwa vimehaririwa.

Baya zaidi ni kuwa ukiwa ndani ya eneo la Bunge pahala pekee ambapo matangazo ya vikao yanaonekana  ndani ya ukumbi wa Bunge lenyewe jambo ambalo halina mantiki yoyote. Badala yake televisheni zote zilizopo sehemu mbali mbali za Bunge zimefungwa kuonyesha yanayopita ukumbini na hivyo hata mbunge awapo mgahawani au sehemu nyingine eneo la Bunge au hata wafanyakazi hawawezi kuona kinachotokea bungeni.

Kwa maana hiyo inawawia vigumu wafanyakazi na watafiti wa upinzani kujua kinachoendelea, ilhali wafanyakazi na watafiti wa kiwizara huruhusiwa kuingia ndani ya ukumbi na kuweza kutoa ushauri kwa waziri wa wizara yao. Hali imefika kiasi hicho.

Watanzania wanatakiwa kujua kuwa Bunge na mkutano wa hadhara ni wa Watanzania wote. Ila kwa sababu wote hawawezi kuhudhuria ndipo kuna wawakilishi wao ambao watataka kuwaona wanavyofanya kazi waliyowatuma na kama yupo anayezuia haki yao hiyo wajue ni Serikali ya Dk John Pombe Magufuli.

Ikifika hapa ndipo mtu unajiuliza hivi kweli kuna nia safi katika hili? Kinaepushwa nini, kinafichwa nini jamani?  Hivi ndivyo Serikali ya Magufuli ilivyokusudia kuiongoza Tanzania ambayo ilikuwa imesonga mbele katika suala la uhuru wa habari na sasa irudi nyuma?

Kitu gani kinaipa nguvu Serikali hii katika hili?  Inafaa umma unyanyuke na useme kuwa hili linaturudisha nyuma kama Taifa, linatuaibisha kama taifa na linatudumaza kama Taifa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles