26.7 C
Dar es Salaam
Monday, March 4, 2024

Contact us: [email protected]

Bado tunauhitaji Muungano huu?

nyerere-karume-b03MIAKA kadhaa nyuma nikiwa shule ya msingi nilikuwa napenda sana yale maswali niliyokuwa naulizwa kwenye somo la Maarifa ya Jamii, katika mtihani wake nilikuwa sikosi swali lililokuwa likiuliza Tanganyika na Zanzibar ziliungana mwaka gani, kama lilikuwa ni swali ambalo lina majibu ya kuchagua hakika nilikuwa siwezi kukosa maana niliitafuta ilipo Aprili 26,  maswali mengine kama Rais wa Kwanza wa Tanzania aliitwa nani?

Basi ningelitafuta jina la Julius Kambarage Nyerere, ni viongozi gani walioiunganisha Tanganyika na Zanzibar? Basi ningelitafuta jina la Mwalimu Nyerere na Abeid Amani Karume, Bendera ya Tanzania ina rangi ngapi? Kila rangi inawakilisha nini? Hivyo hivyo hadi nilipoanza kidato cha kwanza kwenye somo la Uraia (CIVICS) nilikuwa napenda sana maswali yenye mfanano huo.

Jamhuri Ya Muungano wa Tanzania inaundwa na muunganiko wa nchi mbili ambazo ni Tanganyika almaarufu Tanzania Bara kwa sasa na Zanzibar almaarufu Tanzania Visiwani ambayo inaundwa na visiwa vikuu viwili vya Unguja na Pemba, yenyewe ilifanya Mapinduzi tarehe Januari 12, 1964 huku Tanganyika ikipata uhuru wake Disemba 9,1961. Tanganyika ilipata Uhuru baada ya kuwa chini ya usimamizi wa Taifa la Uingereza baada ya Taifa hilo kushinda Vita Kuu ya Pili ya Dunia huku Zanzibar ilifanya Mapinduzi yake na kufanikiwa kuuondoa utawala wa Sultan kutoka Oman.

Ikifika siku ya maadhimisho ya miaka kadhaa ya Muungano nilikuwa nafurahia sana maana nilikuwa najua lazima kutakuwa na gwaride pale Uwanja wa Uhuru zamani Taifa, nilikuwa najua nitafurahia kuona wanajeshi wanavyopiga kwata maana nilikuwa naihusudu kazi hiyo sijui zile ndoto ziliishia wapi,  pili nilikuwa najua nitafurahia nikiona watoto wanavyocheza halaiki na kwangu mimi Muungano ndio ulikuwa unaishia pale maana mimi nimezaliwa nikaikuta Tanzania ikiwa na miaka zaidi ya ishirini lakini kadri siku zinavyokwenda nikaanza kuiona na kuifahamu maana halisi ya Muungano.

Washukuriwe viongozi ambao walitumia muda wao na nguvu kuhakikisha walifanya mataifa haya mawili kuwa Taifa moja kubwa, mpaka leo hii tunatimiza miaka 52 ya Muungano ama kwa hakika si jambo dogo japo kuna viashiria ambavyo naweza kusema zisipochukuliwa hatua za dhati huko mbele historia inaweza kubadilika na tukaanza kusema kuwa kulikuwa na Taifa linaitwa Tanzania.

Mpaka hivi sasa Muungano huu umeshakuwa chini ya marais watano ambao kwa nyakati tofauti wameweza kuliongoza Taifa hili wakianza na Mwalimu Julius. K. Nyerere, Alhaj Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa, Jakaya Kikwete na Dk. John Magufuli, ila pamoja na mabadiliko ya marais wote hao ukiniambia nimeweza kuona jambo gani la kitofauti limefanyika nitakujibu kwa kifupi kuwa sioni? Lakini pia kuna swali ambalo ukiniuliza jibu lake nitakalokupatia nafikiri jibu lake linaweza kuwa uchochezi, swali lenyewe ni hili.

Je, Zanzibar ni nchi? Hili swali nimewahi kushuhudia Waziri Mkuu mstaafu akizomewa bungeni baada ya kujibu kuwa Zanzibar si nchi. Hapa unaweza kujiuliza nini tatizo? Na baada ya muda ndipo nikaanza kulisikia neno ambalo mpaka sasa linasumbua kichwa changu nalo ni ‘Kero za Muungano’ hili nimewahi kulisikia tangu kwenye hotuba za Mwalimu Nyerere mpaka leo hii bado nalisikia. Sasa swali ambalo najiuliza, Je, kuna faida zozote za huu Muungano? Je, kuna hasara pia ambazo zinatokana na huu Muungano? Tukiuvunja Muungano tunapata nini na kuendelea kuwa na Muungano tunafaidika na nini?

Watu wengi niliowahi kuwasikia wakizungumzia sababu kuu ya viongozi hao kuleta Muungano ni nini? Wengi hujibu kuwa sababu kuu ni mambo ya Kiusalama kuwa Mwalimu Nyerere alihofia kuwa eneo la upande wa bahari haliwezi kuwa salama hivyo ni vyema kuungana na Wazanzibar ili kuweka hali ya usalama inayoeleweka katika eneo hilo. Lakini ukiachana na sababu hiyo Muungano huu bado nafikiri una umuhimu mkubwa sana, na zifuatazo ni sababu kadhaa za kwa nini tunauhitaji Muungano.

Moja, upatikanaji wa rasilimali watu, katika nchi yoyote idadi ya watu ni jambo la msingi katika kuimarisha uchumi maana ili uchumi uwepo ni lazima watu wafanye uzalishaji lakini pia baada ya kufanya uzalishaji inahitaji upate watu ambao watakuwa kama soko hivyo suala la kuungana lilikuwa na faida zaidi ya zile za kiusalama maana ni rahisi kwa watu wa visiwani kupata rasilimali watu huku Bara na hata masoko pia kwa vile ambavyo havizalishwi huku Bara na vivyo hivyo kwa vile ambavyo vinazalishwa huku Bara na kuuzwa visiwani, mfano mzuri ni hivi sasa ambapo Mchaga anaweza kwenda kuuza nafaka kule Visiwani na hata Mpemba anapoweza kuja kutengeneza na kuuza tambi huku Bara.

Pili, ongezeko la vyanzo vya mapato, kama kuna nchi imebarikiwa kuwa na vyanzo vya mapato basi Tanzania ni nchi moja kati ya nyingi, japokuwa tuna tatizo kwenye kusimamia vyanzo hivyo lakini bado hii ni faida, tuna maeneo ya utalii kama mbuga, milima, bahari, tuna bandari na miji ya kihistoria pia kama Bagamoyo ukiacha Zanzibar yenyewe kama Taifa lakini kama tukitengana ina maana Mzanzibar hatakuwa hahusiki na rasilimali zilizo Bara vivyo hivyo kwa upande wa pili. Kama isingekuwa udhaifu kwenye usimamiaji wa hivi vitu yawezekana hii hoja ingekuwa imeifanya nchi hii kuwa nchi tajiri ssna katika bara hili kama si ulimwenguni kote.

Tatu, uwepo wa soko la uhakika, kama kuna jambo ambalo hivi sasa linasumbua nchi zilizoendelea basi soko la uhakika, kuna nchi zina teknolojia nzuri lakini hazina soko la uhakika na hata kama kuna soko nikiwa na maana uwepo wa namba kubwa ya watu bado wanapata changamoto kubwa kufanya kazi na watu wa mataifa mengine ila kwetu sisi tumefanikiwa kuunganisha mataifa mawili maana yake ni kuwa hamna vikwazo kwenye ufanyaji wa biashara kwenye nchi hizi mbili.

Nne, maingiliano yasiyo na vikwazo, leo hii mtu wa Bara kwenda Zanzibar ni kama kutoka Morogoro kwenda Dodoma, mwananchi hawezi kupata matatizo akitoka upande mmoja wa Jamhuri kwenda upande mwingine. Haya maingiliano yana faida nyingi sana kwa sababu katika maingiliano haya kuna wataalamu wanatoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine, kuna wawekezaji wanatoka upande mmoja kwenda upande mwingine kitu ambacho kama kusingekuwa na Muungano wangehesabika kama wawekezaji wa kigeni lakini hivi sasa haiko hivyo, kuna wanafunzi wa Elimu ya Juu wanatoka visiwani kuja Bara na wapo ambao wanatoka Bara kwenda visiwani na wengine huanzisha maisha huko huko.

Hizo ni baadhi ya faida ambazo zinaweza kupatikana na nyingine zimeshapatikana kutokana na uwepo wa Muungano ila Muungano huu pia una hasara nyingi, nasema hasara nyingi kwa sababu hizo ndizo zinazoonekana wazi, nimezungumzia faida lakini kwenye faida ili tunufaike kuna hatua za muhimu sana kuchukua ili kufikia malengo lakini kwenye hasara hizi zimeanza kuonekana na hasara zenyewe ni kama hizi

Mosi, muingiliano wa Katiba kati ya ile Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ile ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar. Katiba ya Jamhuri ya Muungano inasema kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano ndiye Amiri Jeshi wa Watu wa Jamhuri lakini pia Katiba ya Serikali ya Mapinduzi inazungumzia Rais atakuw andiye Mkuu wa Vikosi vya SMZ, nafikiri hapa unaweza kuona huo mkanganyo, yaAni haiwezekani Taifa Moja liwe na mamiri Jeshi wakuu wawili, ukiangalia kwa jicho moja unaweza kusema hakuna tatizo ila kutokuwa na tatizo hakukufanyi usikague na kuangalia kama kuna tatizo litaweza kutokea.

Leo hii Rais wa Jamhuri akienda Zanzibar kwenye sherehe za kiserikali kama Mapinduzi anakwenda kama mgeni mwalikwa hii inakuwaje? Leo hii tunaona kama hili si jambo la hatari kwa sababu marais wa pande zote mbili wanatoka chama kimoja lakini Je, tumeshawahi kuwaza siku marais wa pande hzi watakapokuwa wanatoka vyama tofauti halafu wakakwaruzana? Tutakuwa salama kweli? Undugu wetu utaendelea kuwapo?

Pili, Muungano umeleta unyonyaji, leo hii kuna mambo ya Muungano na mambo yasiyo ya Muungano, mambo yasiyo ya Muungano ina maana ni mambo ya Zanzibar peke yake na mambo ya Muungano maana yake ni mambo ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hivyo hii ina maana kuna mambo Zanzibar kama Zanzibar inajadili peke yake lakini kwenye mambo ya Jamhuri pia Zanzibar inachangia. Kabla ya Muungano kulikuwa na rasilimali ambazo ziko Bara tu haziko visiwani vivyo hivyo na upande wa pili lakini kwa bahati mbaya hakuna sehemu ambayo mambo ya Bara yanajadiliwa peke yake  hii ina maana Zanzibar wakiwa kwenye Baraza la Wawakilishi wanajadili masuala ya Zanzibar kwa kutumia rasilimali ambazo ni za Zanzibar tu lakini pia wanakuja Bara kujadili mambo ya Muungano ambayo sehemu kubwa ni mambo ya Bara ambayo yamevishwa sura ya mambo ya Muungano sasa huu kwa namna moja au nyingine ni unyonyaji na si Bara tu inayonyanyasika hata Zanzibar pia, mara nyingi wamekuwa wakitamani kutambulika kama Taifa ili waweze kupata baadhi ya misaada lakini haipo hivyo maana huko nje Zanzibar haifahamiki kama Taifa bali inatambulika kama sehemu ya Jamhuri hali inayosababisha Wazanzibar wengi kujiona kama kisiwa kinachotawaliwa na upande mwingine.

Tatu, Muungano huu unaleta viashiria vya ubaguzi, ukienda pale Zanzibar wana bendera yao, wana wimbo wao wa Taifa, wana Rais wao na pia wana Katiba yao lakini pia hiyo kama haitoshi katika Taifa hili moja kuna Watanzania na Wazanzibar, swali la kujiuliza Je, Mtanzania ni nani na Mzanzibar ni nani?  Hivi iliwezekana vipi Watanganyika wakaondoka halafu Wazanzibar wakabaki? Upi ulikuwa msingi wa Muungano? Nnachofahamu ni kuwa tukiamua kuwa wamoja basi tunatafuta wote na kutumia wote sasa hili la kusema hiki changu hiki cha wote limeanzia wapi? Wapo watakaosema au wanaoona kama nawaandama watu wa upande mmoja la hasha, haya ni matokeo ya wakubwa kutokuliangalia suala hili kwa umakini maana nafikiri haukuwa msingi wao kwenye uanzilishi wa jambo hili.

NnE, Muungano huu unaweza kusababisha viashiria vya uvunjifu wa amani, tumeshuhudia mara kadhaa vikundi fulani vikianzishwa ili kudai madai sulani ambapo wengine walikwenda mbali mpaka kuanzisha kampeni za kutaka Muungano ufe. Tumeona watu wakifunguliwa mashtaka, tumeona nyumba za ibada zikichomwa, tumeshuhudia matukio mengine mengi ambayo mengi ambayo msingi wake ni Muungano hivyo ni kazi kwa viongozi kulitazama hili vyema.

Nimejaribu kuangazia upande wa faida na hasara wa suala hili la Muungano lakini sisi kama Taifa tuna kazi kubwa ya kama ni kweli bado tuna nia ya dhati kuliendeleza Taifa hili, jambo lolote lililo imara linahitaji kuwa na msingi imara, ya Mwalimu Nyerere na Mzee Karume yalishapita na walishatangulia mbele za haki sasa tuna kazi ya kutengeneza Taifa litakalokwenda sawa na changamoto za kizazi chetu, watu wa Visiwani wanahitaji Zanzibar yenye mamlaka kamili lakini pia hata watu wa Bara nao imebidi waamke na kudai Tanganyika yao lakini haya yote ni matokeo ya kushindwa kutengeneza Taifa moja ambalo litakuwa na bendera moja, Katiba moja na hata Rais mmoja.

Kama tulisoma kuwa Tanzania ni muunganiko wa Tanganyika na Zanzibar iweje bado sehemu ya Jamhuri iko pembeni tena?  Wakati wa mchakato wa Katiba Mpya suala la Serikali tatu lilikuwa haliepukiki maana kila mtu kaanza kuvutia kwake mashaka yangu ni kuwa kila mtu akiwa na lwake nafikiri hapo mbele hatutaona umuhimu kutembeleana na kutumia sawa hivi tulivyonavyo kwa sababu kila mtu atakuwa na chake.

Ukinirudisha siku kadhaa nyuma kwenye mchakato wa Katiba ningekwambia mimi ni muumini wa Serikali moja nikiwa na maana Tanganyika na Zanzibar zibaki kwenye historia halafu sote tuwe Watanzania kama ni kweli tunautaka Muungano kutoka moyoni mwetu vinginevyo ni vyema tungefuata ushauri wa Mzee Karume kuwa Muungano ni kama koti ikifika kipindi tukiona linatubana tunavua, nafikiri ni busara zaidi tukirudi chini tukajadili na kuhakikisha misingi ya nchi zote inazingatiwa ili kutengeneza Taifa moja lenye umoja usio na manung’uniko ambao utasababisha mmoja kuona ni heri akabaki mwenyewe.

Miaka 52 ya Muungano bado ninauhitaji Muungano lakini si kwa muundo huu, nauhitaji muundo bora zaidi ambao utatufanya tuendelee kutamani kubaki kwenye Muungano zaidi ya kuwaza kutoka.

Nawasilisha.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
584,000SubscribersSubscribe

Latest Articles