WIKI chache zilizopita ilipotangazwa kwamba Mkuu wa Mkoa wa Sinyanga, Anne Kilango Malecela, ameondolewa kwenye nafasi yake kutokana na kutokuwa mkweli, kuna swali niliulizwa na mmoja wa watu walio karibu nami. Niliulizwa maoni yangu kuhusu hatua hiyo ya Rais, kwanza nikiwa kama mwanamke na pili, nikiwa Mtanzania wa kawaida.
La kwanza lilikuwa rahisi sana kujibu. Mimi si muumini hata kidogo wa “wanawake wakiwezeshwa wanaweza.” Siamini kwamba wanawake wanatakiwa kuwezeshwa. Ninachokiamini ni kwamba wanawake wanatakiwa kupewa fursa sawa kama wanaume. Wapate kazi kutokana na elimu yao na uwezo wao na si kutokana na jinsia yao. Wapandishwe vyeo kutokana na uongozi wao thabiti na si jinsia yao. Watumbuliwe kutokana na makosa waliyoyatenda na si kusitiriwa eti kwa kuwa tu ni wanawake.
Swali la pili, hata hivyo, lilikuwa linahitaji ufafanuzi zaidi. Nazungumziaje kutumbuliwa kwa Kilango Malecela kutoka katika nafasi yake ya ukuu wa mkoa, takribani wiki tatu na nusu tu tangu ateuliwe.
Nilichokijibu ni kwamba siku Rais anawaapisha wakuu wa Mikoa, alitoa ‘assignment’ hadharani. Alisema kwamba anawapa ‘grace period’ ya wiki moja, kwamba wawe wamewasaka watumishi hewa kwenye mikoa yao. Kauli ya Rais ilikuwa ni amri na ilitakiwa kuwa kazi ya kwanza kabisa kufanywa na wakuu wa mikoa.
Siku tuliyotangaziwa idadi ya watumishi hewa kutoka kila mkoa, tulitangaziwa pia kwamba Mkoa wa Shinyanga haukuwa na mtumishi hewa hata mmoja, kutokana na mikakati mizuri iliyowekwa na Mkuu wa Mkoa aliyepita.
Tunajua kwamba Mkuu wa Mkoa hakwenda yeye mwenyewe moja kwa moja kwenye mifumo ya takwimu na fedha kubaini kama watumishi hewa wapo ama hawapo. Ni dhahiri kwamba mkuu wa mkoa analetewa orodha hiyo na wasaidizi wake, akiwamo Katibu Tawala wa Mkoa. Ni dhahiri pia kwamba orodha hiyo inatoka katika halmashauri mbalimbali zilizopo katika mkoa husika na hivyo wakuu wa wilaya nao wanahusika. Lakini pamoja na hayo, mkuu wa mkoa ni lazima ajiridhishe kwamba taarifa iliyoletwa kwake ni sahihi na kama ana shaka nayo, aombe muda ili kufanya uchunguzi zaidi.
Niseme tu ukweli kwamba ilipotangazwa kuwa Shinyanga hakuna mtumishi hewa hata mmoja, mimi mwenyewe nilipata shaka. Nilijiuliza kama hilo kweli linawezekana. Kila mtu anajua kwamba Tanzania ilikuwa imefika mahali pabaya sana, huku wengi wa wafanyao kazi serikalini wakiwa wamekosa uadilifu, na wakati wote wakiwaza kuchuma tu hela kupitia migongo ya watu wengine. Hili la mtumishi hewa lilikuwa ni jipu ambalo kila mtu analijua na limeshawahi hata kusemwa na watu wengi, wakiwamo mawaziri waliopita, lakini hatukusikia hatua zozote zikichukuliwa.
Jibu langu lilikuwa hivi: Kwakuwa Rais alitangaza hadharani kazi ya kwanza kabisa ya wakuu wa mikoa waliyotakiwa kuifanya ndani ya wiki moja na kwa kuwa kila mwananchi aliisikia amri ile na kwa kuwa utendaji kazi wa Magufuli umeshajulikana kwamba ni wa kasi kweli kweli ili kuleta mabadiliko chanya Tanzania, basi Anne Kilango Malecela alitakiwa kuwa makini zaidi kwenye kazi yake.
Kama ‘Assignment’ ya kwanza tu anaruhusu wasaidizi wake wamdanganye na yeye akadanganyika, basi ni dhahiri kwamba kasi hii ya Magufuli itamshinda. Alitakiwa kuondolewa katika nafasi yake na huenda akatafutiwa nafasi ambayo ataweza kuimudu, kwani hiyo ya ukuu wa mkoa tayari imekuwa kubwa sana kuliko uwezo wake.
Sasa wiki iliyopita tena, Rais Magufuli amemtumbua hadharani Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Wilson Kabwe. Kutumbuliwa huku kumetokana na madai mazito dhidi ya Kabwe yaliyotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda. Halikumpa shida Rais. Aliuliza hadharani wakati wa ufunguzi wa daraja la Kigamboni kama atumbue jipu pale pale, na watu wakaitikia “tumbua” naye hakuikawiza.
sasa wapo watu ambao wameibuka kwa jina la ‘haki za binadamu’ wakidai kwamba staili ya utumbuaji ya Rais Magufuli ni ya udhalilishaji na haizingatii misingi ya haki za binadamu. Wengine wanadai kwamba anachokifanya ni udikteta na pia anatafuta sifa.
Wakati kila mtu akitoa maoni yake kutokana na hii staili ya Rais ambayo watu hawajazoea kuiona, kuna swali lilinijia kichwani: Kwani, hii tumbua tumbua ya Rais Magufuli inamkwaza nani hasa? Inawakwaza wanaotumbuliwa? Wanaotuhumiwa? Ndugu na jamaa zao? Wanaoibiwa? Ni nani hasa anayekwazika na kupiga kelele kwamba haki za binadamu zinakiukwa na kwamba Rais amekuwa dikteta?
Naomba niwakumbushe kitu kimoja. Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana ulikuwa ni uchaguzi mgumu sana kwa Chama Cha Mapinduzi. Wengi wa walioshabikia upinzani, hawakushabikia kutokana na kumpenda sana mgombea kwa tiketi ya Chadema; la hasha! Walishabikia kutokana na kuchoshwa kuongozwa na Serikali ya CCM. Kilichowachosha ni ulaji uliokuwa ukiendelea, kulindana kulikokuwa kukiendelea, kunyanyasa wananchi kulikokuwa kunaendelea na wizi wa wazi kabisa uliokuwa ukiendelea.
Tangu Rais Magufuli aingie madarakani, wale waliokuwa wakishabikia upinzani, ndio ambao hivi sasa wanamshabikia Rais Magufuli; unadhani ni kwa sababu gani? Wanamshabikia kwa sababu ameonyesha mwelekeo wa kuyafanya yale waliyokuwa wakiyataka siku zote: Haki sawa kwa raia wote, kila mtu kula kwa jasho lake halali, mijizi kukamatwa na kufunguliwa mashitaka; naam! Na majipu kutumbuliwa.
kwamba wakati Rais anazindua Bunge, alisema wazi kuwa atatumbua majipu. Alisema wazi kwamba atayatumbua bila kuona huruma na majipu hayo yatauma. Sasa kama kuna mtu alitarajia kwamba jipu likikamuliwa anayekamuliwa atajisikia raha kama anakula wali maharage, basi huyo mtu ni wa ajabu sana.
Lakini turudi tena kwenye swali langu. Anayeumia hasa kutokana na majipu hayo kutumbuliwa namna yanavyotumbuliwa, ni nani? Ni mwananchi wa kawaida ambaye miaka nenda rudi amekuwa akilalamikia udhalimu uliokuwapo ambao tuliahidiwa maisha bora kwa kila Mtanzania lakini yakabaki kwa wateuliwa wachache? Ni mwanakijiji ambaye anafuatwa kila siku kulipa kodi lakini akienda hospitali hata Panadol hakuna? Ni mama muuza soko ambaye analazimishwa kulipia mapato kila siku lakini pale sokoni hata usafi wa vyoo ni tatizo? Ni mzazi ambaye kila kukicha analazimishwa kuchangia maabara wakati mtoto wake hajawahi kukalia dawati tangu aanze shule?
Kama si hao wanaolalamika, basi nakubaliana na Rais. Watu wanataka wateuliwe hadharani, basi na kutumbuliwa iwe hadharani. Wakiwatumikia wananchi ipasavyo, kamwe hawataishi kwa hofu kama waliyonayo hivi sasa.