22.9 C
Dar es Salaam
Sunday, June 23, 2024

Contact us: [email protected]

CAG azidi kuanika madudu     

cag-mussa*Afichua wajanja walivyohamisha hisa za Pride

*Benki ya Exim yachota bilioni 10/- Ngorongoro

Na Bakari Kimwanga, Dodoma

MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad, amezidi kufichua madudu ndani ya Serikali na mashirika yake, huku akihoji utata wa namna Taasisi ya mikopo ya Pride Tanzania ilivyomilikishwa kwa watu binafsi.

Pamoja na hali hiyo, pia amebaini namna wafanyakazi wa Benki ya Exim walivyoshiriki kufanya ufisadi katika Mamlaka ya Hifadhi Ngorongoro kwa kukwapua dola za Marekani 2,890.

Hayo ameyabainisha katika taarifa ya ukaguzi wa hesabu za Serikali na mashirika ya umma iliyoishia Juni 30, mwaka 2015.

Profesa Assad alisema kuwa hadi sasa haijaelezwa wazi namna hisa za Pride zilivyopelekwa katika umiliki wa watu binafsi.

Kutokana na hali hiyo, amemtaka Msajili wa Hazina kuhakikisha anafuatilia kwa karibu juu ya umiliki wa kisheria wa hisa hizo zilizokuwa zinamilikiwa na Serikali na baadaye kuhamishwa kwa watu binafsi.

“Taasisi ya Pride Tanzania ilianzishwa Mei 5, mwaka 1993 chini ya sheria ya makampuni kwa dhamana. Madhumuni ya kuanzishwa kwa chombo hiki ni kutoa mikopo midogo midogo kwa wajasiriamali.

“Taarifa ya Msajili Hazina iliyoonyesha uwekezaji wa Serikali katika kampuni hii, kufikia Juni 30, 2008 ilionyesha hisa zote za Pride zinamilikiwa na Serikali,” alisema CAG Assad katika taarifa yake ya ukaguzi.

Hata hivyo, kwa mujibu wa taarifa ya Msajili wa Hazina inayoishia Juni 30, 2012, Pride iliondolewa katika orodha ya mashirika ya umma, lakini uhalali wa hatua hiyo hakuweza  kubainika.

CAG Assad alisema kwa mujibu wa kifungu cha 31 cha sheria ya ukaguzi wa mashirika ya umma namba 11 ya mwaka 2008,  kila shirika la umma linatakiwa kupeleka hesabu kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kukaguliwa katika fedha.

“Hata hivyo, hesabu za Pride Tanzania hazijawahi kuwasilishwa kwenye ofisi ya CAG kama inavyotakiwa na sheria.

“Pamoja na majibu ya Serikali kuwa kampuni hii imeacha kupata fedha za Serikali kutoka Serikali ya Kifalme ya Norway na Tanzania mwaka 2005, bado haijawekwa wazi jinsi hisa za kampuni hii zilivyohamishwa kwenda kwa wamiliki binafsi.

“Hivyo basi, ninaendelea kusisitiza kuwa Msajili wa Hazina anapaswa kufuatilia kwa karibu juu ya umiliki wa kisheria wa hisa za Pride Tanzania zilizokuwa zinamilikiwa na Serilali na baadaye kuhamishiwa kwa wamilii binafsi,” alisema CAG.

 

BENKI YA EXIM NA WIZI

Kuhusu Benki ya Exim ambayo inadaiwa na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kiasi cha dola za Marekani 741,910 ambazo ni sawa na Sh bilioni 1.6152, alisema madeni hayo yalitokana na udanganyifu uliofanywa na wafanyakazi wa benki hiyo kwa mwaka wa fedha 2012/13.

Profesa Assad alisema katika ripoti yake kuwa baadae benki hiyo ilikubali kulipa kiasi cha dola za Marekani 333,960 tu pamoja na riba ya asilimia 2.5 ambayo ni sawa na dola za Marekani 8,349.

Alisema pamoja na kufanyika kwa malipo hayo, bado lilibaki salio la dola za Marekani 404,950, ambapo kiasi hicho hakikuweza kuthibitishwa na timu ya uchunguzi wa Benki ya Exim.

“Hadi kufikia Desemba 17 mwaka 2015, Benki ya Exim iliweza kulipa Mamlaka kiasi cha dola za Marekani 331,070 badala ya dola za Marekani 330,960 ambazo benki ilikubali kulipa, hivyo dola za Marekani 2,890 hazikulipwa.

“Deni hilo ambalo halikulipwa linatia mashaka, hivyo tunaishauri menejimenti ya Mamlaka kuhakikisha inaweka nguvu za kutosha kuhakikisha kiasi cha fedha kilichobaki kinakusanywa kutoka Benki ya Exim na ikishindikana hatua za kisheria zichukuliwe,” alisema CAG.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya CAG sura ya 10, wakati wa ukaguzi alibaini kwamba wizara 17, balozi mbili na sekreterieti za mikoa 11 zilifanya malipo ya Sh bilioni 11.314, ambayo yalikuwa na nyaraka pungufu kinyume cha kanuni 86 (1) ya kanuni za fedha ya mwaka 2001, pia na kanuni 95 (4) na 18 (f) ya kanuni za fedha ya mwaka 2001.

“Nyaraka za viambatanisho zikikosekana inakuwa vigumu kuthibitisha pasipo shaka uhalali wa malipo hayo, hivyo kufanya mawanda ya ukaguzi kuwa finyu,” alisema.

Ripoti hiyo aliyoikabidhi kwa wenyeviti wa kamati za kudumu za Bunge za Hesabu za Serikali (PAC) pamoja na ile ya Hesabu ya Serikali za Mitaa (LAAC), imezimulika kwa kuzikagua taasisi za Serikali Kuu 199, Mamlaka ya Serikali za Mitaa 164 na mashirika ya umma 102 kati ya 186.

Profesa Assad alisema kwamba kwa upande wa miradi ya maendeleo ametoa ripoti 799 na kufanya jumla ya ukaguzi wa fedha.

Akisoma muhtasari wa ripoti kwa zaidi ya saa mbili, CAG Assad alisema halmashauri zilizopata hati safi ni 47, hati zenye shaka 113, hati isiyoridhisha tatu na hati mbaya moja.

Kwa upande wa Serikali Kuu, wizara zilizopata hati safi ni 180, hati yenye shaka 18, hati isiyoridhisha moja na hakuna hati mbaya na kwa mashirika ya umma yaliyopata hati safi ni 99, hati yenye shaka matatu na hakuna iliyopata hati isiyoridhisha wala hati mbaya.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles