33.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Meya: Tunahakiki miradi ya jiji Dar

MEYA-ISAYA-MWITANA CHRISTINA GAULUHANGA, DAR ES SALAAM

HALMASHAURI ya Jiji la Dar es Salaam, imeunda kamati maalumu kwa ajili ya kuchunguza mali zake, baada ya kubaini uwepo wa mbinu chafu zinazosababisha ukusanyaji wa mapato katika jiji hilo kushuka.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita alisema uamuzi huo umetolewa na Baraza la Madiwani, baada ya kubaini harufu ya ufisadi katika miradi mbalimbali ya jiji hilo.

Alisema jiji hilo lina miradi mingi lakini cha kushangaza kwa mwaka limekuwa likikusanya Sh bilioni 11.7 tu ambazo haziendani na vyanzo vya mapato vilivyopo.

“ Tumeamua kukusanya fedha nyingi kutoka vyanzo vyetu vya ndani …tumejipangia kufikia makusanyo ya Sh  bilioni 20 katika bajeti yetu ya mwaka huu,”alisema Mwita.

Alisema wamebaini wana mali nyingi, lakini hazifuatiliwi kwa ukaribu ambapo gharama zinazolipwa na kukusanywa haziendani na uhalisia.

Akitolea mfano, alisema jiji hilo  halinufaiki na miradi kama ile ya Soko la Kariakoo ambalo lina biashara kubwa, ambapo kwa muda mrefu kuna madai linaendeshwa kwa hasara.

“ Hali hii hatukubaliani nayo…tunaangalia mazingira ya Soko la Kariakoo jinsi yalivyo kibiashara, eti mtu anasema linaendeshwa kwa hasara hatukubaliani kabisa, tunatumia timu yetu kufanya tathimini,”alisema Mwita.

Alisema mfano, mwingine ni fremu zilizopo Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa ambapo wapangaji wanatozwa Sh 30,000 kwa mwezi kiwango ambacho ni kidogo mno.

“Haiwezekani fremu zikalipiwa kiasi hiki Kariakoo, wakati wapangaji wengine katika maeneo hayo wanalipia fremu ndogo zaidi ya hizo hadi Sh 300,000 kwa mwezi…hapa kuna wajanja wengi wananufaika

“Kwa mfano kuna ukumbi wa  DDC Kariakoo, Temeke, Mlimani City , Kondoa- Kinondoni, ajabu ni kwamba eti tunaambulia Sh milioni 50 tu kwa mwaka kwa sehemu zote hizo, ”alisema Mwita.

Kuhusu Kituo cha Mabasi cha Ubungo, Mwita alisema kuna vibanda vingi vya biashara, lakini mapato yanayopatikana hayaendani na biashara zilizopo.

Alisema kamati iliyoundwa itatoa taarifa yake Jumanne kuhusu miradi yote inayomilikiwa na jiji na aina ya biashara zilizopo, ili kubaini kiwango cha upotevu wa fedha.

“Tunafanya hivyo kwa uzalendo mkubwa ili watu wajue tunachokipoteza na kama waliojichukulia kinyemela waanze kurejesha mali zetu,”alisema Mwita.

Alisema wanasubiri  taarifa za kamati ndogo ya ufuatiliaji kwa kuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ameonyesha njia kuwa UDA ni mali ya jiji.

“ Tunaanza kufuatilia kwa karibu mchakato mzima wa hisa za UDA ili tujiridhishe na turejeshewe mali yetu kwa kuwa sisi kama jiji hatukuingia mkataba na hao waliopo,”alisema Mwita.

Kubenea

Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea (Chadema), alisema ripoti iliyotolewa na CAG inaonesha wazi kuwa jiji hilo halikuuza hisa kwa Kampuni ya Simon Group Ltd.

Alisema Mkurugenzi Mtendaji wa SGL, aliingiza Sh bilioni 5 kwenye akaunti ya jiji  kwa ajili ya kununua hisa, hivyo fedha hizo wamezizuia hadi hapo watakapojiridhisha kuhusu mchakato huo.

“Katika hili tunamuagiza mwenzetu Kisena aje tufanye naye mazungumzo lakini fedha zake tunazizuia kwa sababu ametumia jina letu kibiashara kwa muda mrefu wakati hatuna makubaliano naye.

“Tumejiandaa vya kutosha katika hili kama hataki makubaliano na sisi aende mahakamani nasi tutakutana huko tutatumia wanasheria wa aina mbalimbali,” alisema Kubenea.

Alisema wamepitia nyaraka za manunuzi ya hisa za UDA na kubaini mapungufu mengi ambapo wataalamu wengi waliopitia nyaraka hizo walisema utaratibu haukufuatwa.

Mdee

Kwa upande wake Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (Chadema), alisema kitendo cha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), George Simbachawene kumkabidhi mradi wa Machinga Complex, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ni ukiukwaji wa sheria.

Alisema waziri huyo hakupaswa kuivunja Bodi ya Machinga Complex kwa kuwa ipo chini ya jiji na ndiyo lenya  mamlaka na masuala yote.

“Soko la Machinga ni mali ya jiji kwa asilimia 100…hivyo kitendo alichokifanya Waziri Simbachawene si sahihi kwa kuwa uozo uliopo umesababisha deni la Sh bilioni 36 ya ujenzi wa jengo hilo tunazodaiwa na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF),”alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles