25.5 C
Dar es Salaam
Saturday, May 18, 2024

Contact us: [email protected]

Wabunge ‘mabubu’ bungeni kubanwa

Naibu Spika wa BungeNA BAKARI KIMWANGA, DODOMA

KUFUATIA wabunge wa Kambi ya Upinzani Bungeni kutangaza kutochangia bajeti za wizara mbalimbali, Ofisi ya Bunge inatafakari kubadili kanuni ili kuwabana wabunge wasiochangia bungeni.

Kauli hiyo ilitolewa jana bungeni mjini hapa na Naibu Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson, alipokuwa akijibu mwongozo wa Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe (CCM), juu ya hatua ya wapinzani kuendelea kulipwa posho na mshahara, huku wakiwa hawachangii mjadala wa hotuba za bajeti unaoendelea.

Dk. Tulia alisema lazima wabunge wote wawe wazalendo kwa nchi kwa kuhakikisha wanashiriki kikamilifu katika kuchangia bajeti iliyowasilishwa bungeni kwani ndiyo kazi waliyotumwa na wananchi kwa mujibu wa sheria.

“Tabia ya kuhudhuria bungeni kwa ajili ya kulipwa posho bila ya kuitolea jasho inabidi iachwe. Nadhani ipo haja ya siku zijazo kurekebisha sheria tulizonazo kukabiliana na hali ya namna hii, ili kuweka utaratibu mahsusi utakaowezesha kila mbunge kulipwa posho, baada ya kutekeleza majukumu yake ipasavyo na si kuandika kuhudhuria katika mkutano na vikao pekee,” alisema Dk. Tulia.

Alisema kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, Ibara ya 73 imeainisha masharti ya kazi za wabunge ambapo ni pamoja na kulipwa mshahara kwa kila mwezi.

“Masharti hayo yametoa ufafanuzi kuwa mbunge anapohudhuria vikao vya Bunge na kamati zake atalipwa posho ya vikao kwa kiwango kitakachowekwa na Serikali kwa kuzingatia sheria ya fedha za umma na kanuni zake na masharti ya kanuni za Bunge kuhusu vikao.

“Malipo ya mshahara kwa mbunge ni suala la kikatiba na sheria, hulipwa kutokana na kazi yake ya ubunge kama ilivyotajwa katika ibara ya 73 ya Katiba,” alisema.

Dk. Tulia alisema malipo ya posho kwa mbunge yameanzishwa kwa mujibu wa Katiba na pia yamewekwa katika sheria ya uendeshaji Bunge, sura ya 115 chini ya kifungu cha 19.

Alisema utaratibu unaotakiwa kuzingatiwa umefafanuliwa kwenye waraka wa Rais wenye masharti ya kazi ya mbunge yaliyoanza kutumika Oktoba 25, mwaka 2010 na marekebisho yake ya Juni mwaka 2012, ambayo kwa pamoja yanaeleza kwamba mbunge anapohudhuria vikao vya Bunge na kamati zake atalipwa posho ya vikao kwa kiwango kitakachowekwa kwa kuzingatia sheria ya fedha, kanuni zake na masharti ya kanuni za Bunge kuhusu vikao.

Dk. Tulia alisema malipo ya posho kwa wabunge yanatokana na mahudhurio yao bungeni na si kuchangia kama ambavyo wengi wangependa itokee.

“Kimsingi kuhudhuria bungeni pekee si njia inayopendeza kwa kuwa mbunge anapofika bungeni anatarajiwa atekeleze majukumu yake ya kikatiba kama yalivyoainishwa katika Ibara ya 63.

“Tabia hii haikubaliki na haistahili kuendelea. Badala ya mbunge kutekeleza wajibu wake kwa mujibu wa Katiba, anahudhuria bungeni ili tu alipwe posho,” alisema Dk. Tulia.

Alisema Bunge lina jukumu zito la kujadili utekelezaji wa kila wizara na wabunge wote wanao wajibu wa kuchangia makadirio ya matumizi ya Serikali kwa mujibu wa kanuni za kudumu za Bunge toleo la Januari mwaka 2016.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles