22.5 C
Dar es Salaam
Saturday, June 22, 2024

Contact us: [email protected]

Mwongozo utendaji kazi wa mawaziri waiva

Kassim MajaliwaNa Mwandishi Wetu, Dodoma

SERIKALI imekamilisha mwongozo wa majukumu ya mawaziri (instrument) na kwamba muda wowote itatangaza katika gazeti lake, Bunge limeelezwa.

Kauli hiyo ilitolewa bungeni jana na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, wakati akijibu hoja za wabunge waliochangia hotuba ya bajeti ya ofisi yake ya makadirio ya fedha kwa mwaka 2016/17.

Majaliwa alisema kwa mamlaka aliyonayo Rais alianza kuunda Baraza la Mawaziri na baadaye makatibu wakuu ambao ndio watendaji wakuu wa Serikali.

“Ili kuwe na uwezo wa kutengeneza hiyo instrument, ikikamilishwa lazima itangazwe kwenye gazeti la Serikali, nataka niwape faraja kwamba tayari instrument hizi zimeshakamilika na zimesainiwa Aprili 20, mwaka huu, muda wowote Rais atakapoamua atatangaza.

“Mawaziri walioko wanafanya kazi kwa mujibu wa maelekezo ya rais na watendaji wanafanya kazi kwa mujibu wa instrument hii,” alisema.

Kauli hiyo ya Serikali imekuja siku chache baada ya Kiongozi wa Kambi ya Upinzani bungeni, Freeman Mbowe, kugoma kuwasilisha maoni ya kambi hiyo akitoa hoja tatu zilizosababisha kuchukua uamuzi huo.

Miongoni mwa hoja hizo ni pamoja na kupinga hatua ya Serikali ya Rais Dk. John Magufuli kufanya kazi bila ya kuwa na mwogozo wowote wenye msingi halali wa kisheria katika wizara zake.

Hoja nyingine ni uvunjaji wa Katiba na sheria za nchi kuhusu bajeti na Serikali kupoka madaraka na uhuru wa mhimili wa Bunge.

Mbowe alilieleza Bunge kuwa kambi yake haitakuwa tayari kuendelea kushiriki uvunjaji wa Katiba, sheria na haki za msingi za wananchi na kwamba wanatafakari kwa kina hatua za kufuata.

Alisema kutokana na kukosekana kwa mwongozo halali wa kisheria katika wizara mbalimbali, inaonyesha Rais Magufuli hajaiunda kihalali serikali yake.

Akifafanua hilo Mbowe alisema kiongozi huyo wa nchi ameshindwa kutekeleza sheria ya utekelezaji wa majukumu ya mawaziri ya mwaka 1980, ambayo inaweka masharti ya kutengeneza mwongozo wa muundo na utekelezaji wa majukumu ya Serikali yake.

Alisema sheria hiyo inamtaka Rais kila anapounda Baraza la Mawaziri kuchapisha katika gazeti la Serikali kueleza jinsi Serikali yake itakavyotekeleza majukumu yake, jambo ambalo halijafanyika na badala yake Serikali imekuwa ikifanya kazi kwa kauli za Rais na mawaziri bila kufuata mwongozo wowote.

“Sheria ya Utekelezaji wa Majukumu ya Mawaziri ya mwaka 1980, kifungu cha 5(1) kinaweka masharti kwa Rais kutengeneza mwongozo wa muundo na utekelezaji wa majukumu ya Serikali yake.

“Mpaka sasa mwongozo wa utendaji wa Serikali kwa kila wizara (Instrument) unaotumika ni ule uliochapishwa kwenye gazeti la Serikali namba 494A la tarehe 17/12/2010,” alisema Mbowe.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles