Je, tulijua tulichokiomba?

MAGUFULLINI mtoto gani ambaye atamuomba Baba yake mkate akampa jiwe? Hili ni andiko ambalo lipo ndani ya Biblia na hunijia mara nyingi pale ninaposikia malalamiko kuwa mkuu wa kaya ni dikteta, kila ninapokumbuka kuwa siku si nyingi tulikuwa tukilalamika juu ya mkuu wa kaya tuliyekuwa naye kuchelewa kufanya uamuzi na tukaomba mkuu ajaye awe dikteta ili aweze kuinyoosha kaya ambayo ilionekana kukosa kiongozi wa juu imara na mwenye uamuzi wenye tija kwenye kaya yetu.

Ya Mungu mengi na siku hazigandi, mkuu wa maya mpya akapatikana na akaanza kufanyia kazi matatizo yanayosumbua kaya yake ila cha kushangaza ni kuwa wananchi wale wale wanalalamika kuwa mkuu wa kaya anakosea kwenye kutatua matatizo yetu, njia zake hazifai.

Hivi tulifahamu maana ya dikteta? Tulijua matokeo ya kuwa na mkuu dikteta tena katika kaya kama hii yetu ambayo mtu mwenye cheo kidogo anaweza kusigina Katiba na asiwepo mtu wa kumuwajibisha.

Mkuu wa kaya aliyepita tulisema ni dhaifu anachelewa kufanya uamuzi kaja mpya yeye anawahi kufanya uamuzi tunasema hapana anapenda sifa, wengine wanaenda mbali zaidi na kudai anachofanya ni udhalilishaji lakini pia wanasahau kuwa wabadhirifu hao ndio wanaosababisha udhalilishaji kwenye sehemu nyingi.

Kinamama wanajifungulia chini Je, ule si udhalilishaji? Walimu hawalipwi stahiki zao ila kuna watu wanalipa watu wengine mishahara hewa Je, huo si udhalilishaji kwa walimu? Walimu wanakesha wakifunga ubuyu na maandazi ili kwenda kuwauzia wanafunzi madarasani badala ya kufundisha Je, huo sio unyanyasaji? Au unyanyasaji ni kwa walionacho tu ila kwa siye makapuku kukosa haki zetu kwa sababu ya ubadhirifu wa mali za umma si unyanyasaji?

Mtumishi wa umma anaiibia kaya pesa zinazozidi milioni kwa siku halafu bado tunasema ameonewa, mtu kama huyu tulitaka afanyiwe nini? Mtu anapewa kazi ya kukusanya mapato ya kaya yeye anakusanya milioni moja na laki sita halafu anaipatia kaya laki moja na kubaki na mulioni moja na laki halafu bado mnataka achekewe? Mbona binadamu hatuna shukrani?

Mimi nilifikiri tungeanzisha kampeni ya kuhimiza mtu huyo afunguliwe mashtaka maana kusemwa hadharani hakutoshi kumbe ndio kwanza tumeanzisha kampeni ya kumtetea, kampeni ya kumwambia mkuu aache uonevu, yaani kaya inapatiwa milioni moja na laki mbili kwa mpangaji mmoja kwa mwaka pale kituo kikuu cha mabasi halafu kampuni binafsi ya ukusanyaji wa mapato inapata milioni kama kumi na nane kwa mwaka kwa mpangaji mmoja halafu tunataka aandikiwe barua kimyakimya, tunataka asitiriwe mbona yeye wakati anafanya ubadhirifu hakuwa na stara? Tumeusahau ule msemo wa mwosha huoshwa? Au ile kila mtemi ana mtemi wake?

Mtu unapewa kazi ya kufuatilia watumishi hewa unadai hakuna mtumishi hewa halafu inabainika kuna watumishi hewa lukuki mnataka mtu huyu afanyejwe? Leo hii tunasema mkuu huyu anawahi kufanya uamuzi lakini ni sisi wananchi ambao huwa tunapiga kelele tukisikia tume inafanya uchunguzi, ni sisi wananchi ambao huwa tukiwa na kesi zetu zinachukua muda mrefu mahakamani tunalalamika tunapoambiwa uchunguzi unaendelea na mara nyingine kesi zingine huwa na ushahidi wa wazi kabisa lakini uamuzi huchelewa.

Wakati niko shule niliwahi kuambiwa kuwa ukiwa kiongozi kuna muda unatakiwa utumie aina zote za uongozi, uwe kiongozi usiyetabirika maana kuna uamuzi inabidi uvae sura ya kidikteta na kuna uamuzi unatakiwa uvae sura ya kidemokrasia na hiki ndicho ninachokiona kwa mkuu huyu wa kaya japo pia nakubali kuwa si mara zote uamuzi aufanyao anaufanya sawa, ila kwa kaya hii ilipofika bado tunahitaji kiongozi wa aina hii ili tunyooshane kwanza maana Waswahili wanasema bora wakikuogopa maana wakikupenda watakuchukia na hili naliona wazi kwenye mifano ya wakuu hawa wawili ambapo mkuu aliyepita tulimpenda sana mwanzoni matokeo yake mwishoni tukamchukia sasa ni bora huyu tunayemuogopa maana hata tukimchukia tutasema tulimchukia kwa sababu alifanya mambo ya msingi kuliko yule tuliyemchukia kwa sababu alishindwa kufanya uamuzi yenye tija.

Nafikiri kama wananchi tunachotakiwa kufanya ni kuangalia kama uamuzi unaofanyika unaleta tija? Kama hauna tija tujaribu kupaza sauti zetu kwa hoja nzito ambazo zitamshawishi kuonesha kuwa hapa kuna makosa na sio kusubiri kukosoa tu pasipo na hoja.

Uongozi ni jalala, ukiwa kiongozi unatakiwa ukubaliane na hali zote maana kuna muda unaweza ukaambiwa jambo fulani halifai halafu ukalifanyia kazi ila bado ukaambiwa halikutakiwa kufanywa vile ulitakiwa ufanye hivi nani kitu ambacho ni kigumu kumsikiliza kila mtu anasema ndipo ufanye hivyo unatakiwa uwe na uamuzi wa mwisho ambao utakuwa ukikuongoza, tusisahau miluzi mingi hupoteza mbwa.

Na sisi wananchi tukumbuke kile haswa tunachokihitaji maana ukiomba upate dikteta utapewa dikteta hivyo uwe tayari kuishi na dikteta  na nafikiri kwenye hili kuna kitu tutajifunza, safari nyingine tukiomba viatu tuseme ni viatu vya aina gani tunataka, ukisema kiatu bila kutaja aina unaweza kuletewa buti ilhali ulitaka moka.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here